Namba Arubaini Ina Maana Muhimu Katika Uislamu?

 

Namba Arubaini Ina Maana Muhimu Katika Uislamu?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalam aleikum nimesikia jambo lakunishangaza ambalo nigeni kwangu! Kuna watu wanasifu arbaini na wasema lazma tuzingatie hili lina maana kubwa! Katika mifano wasema kua kuumbwa kwamwanadamu ni marhala ya sikuarbaini arbaini. Adam na hawaa walikaa peponi siku 40. Mwanamke ameamrishwa akaesiku 40 baada kuzaa. Nabiyallah yunus alayhi ssalam amekaa tumboni kwa hut siku 40. Mvua na maji ya nabiyallah Nuh yalikauka baada siku 40 mtume Muhammad ametumilizwa miaka 40 na mengi sitoeza kuandika yote! Nataka kufahamishwa kwa ufafanuzi hikma yake kwani wasema kuna hikma ndaniyake!!

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Kwa hakika ikiwa tutakuwa ni wenye kuchukua kila namba na kuifanyia utafiti wa kina kuhusu hilo huenda tukawa tunapoteza muda wetu mkubwa, kwani kama kungekuwa na umuhimu sisi tujue hekima yake, basi Allaah Aliyetukuka na Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wangetueleza ili tupate kujua hilo. Hata hivyo, ikiwa hatukuelezwa hatuna haja ya kutumia muda mrefu na mkubwa ili kutafuta hekima bali ni juu yetu kuchukua hiyo namba kama ilivyoelezwa. Allaah Aliyetukuka Anatuelezea yafuatayo:

 

هُوَ الَّذِي أَنزَلَ عَلَيْكَ الْكِتَابَ مِنْهُ آيَاتٌ مُّحْكَمَاتٌ هُنَّ أُمُّ الْكِتَابِ وَأُخَرُ مُتَشَابِهَاتٌ ۖ فَأَمَّا الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ زَيْغٌ فَيَتَّبِعُونَ مَا تَشَابَهَ مِنْهُ ابْتِغَاءَ الْفِتْنَةِ وَابْتِغَاءَ تَأْوِيلِهِ ۗ وَمَا يَعْلَمُ تَأْوِيلَهُ إِلَّا اللَّـهُ ۗ وَالرَّاسِخُونَ فِي الْعِلْمِ يَقُولُونَ آمَنَّا بِهِ كُلٌّ مِّنْ عِندِ رَبِّنَا ۗ وَمَا يَذَّكَّرُ إِلَّا أُولُو الْأَلْبَابِ ﴿٧﴾

Yeye Ndiye Aliyeteremsha kwako Kitabu humo mna Aayaat zenye maana wazi, hizo ndio msingi wa Kitabu, na nyinginezo zisizokuwa wazi maana zake. Basi wale ambao katika nyoyo zao mna upotovu hufuata zile zisizokuwa wazi maana zake kutafuta fitnah (upotofu) na kutafuta maana zake zilofichika, na hakuna ajuae maana zake isipokuwa Allaah. Na wenye msingi madhubuti katika elimu husema: Tumeziamini, zote ni kutoka kwa Rabb wetu. Na hawakumbuki ila wenye akili. [Aal-‘Imraan: 7]

 

 

Kwa minajili hiyo, utakuta kwamba zipo namba nyingi ambazo zimetajwa katika Qur-aan na Hadiyth sahihi. Kwa mfano, kumi na mbili (12) ina maana na hekima gani kwani imetajwa mara nyingi?

 

1.    Makabila ya Israili ni 12.

2.    Kabila za Quraysh pia nazo ni kumi na mbili.

3.    Chemichemi za maji jangwani kwa wana wa Israili zilikuwa 12.

4.    Katika vita vya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuelekea Najd walikuwa na ngamia 12.

5.    Kutakuwa na Makhalifa 12 kwa Ummah huu.

6.    Ijumaa imegawanywa masaa 12.

7.    Mwaka wa Kiislamu una miezi 12.

8.    Mahari kwa binti za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) haikuzidi uqiyah 12.

9.   Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwagawanya Swahaba zake makundi 12.

10. Katika khutbah moja ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) msafara  uliingia na watu wakatoka akabakia na watu 12 tu.

11. Katika Vita vya Uhud, ni watu 12 tu ndio waliobakia na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi  wa aalihi wa sallam).

12.   Mwenye kuadhini kwa miaka 12 ataingia Peponi.

13.   Mwenye kuswali rak’ah 12 za Dhuhaa ataingia Peponi.

14.   Mwenye kuswali rak’ah 12 za Sunnah kila siku atajengewa nyumba peponi.

15.   Malaika 12 kushindana kuchukua dhikr iliyotolewa na Swahaba.

 

Kwa hiyo, arubaini kama ilivyo hiyo 12, haina maana wala hekima yoyote isipokuwa ni namba kama namba nyengine zilizotajwa katika Qur-aan na Sunnah za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share