Zichume Sifa Kumi Njema - Sifa ya kwanza -Waislamu Wanaume na Waislamu Wanawake
30 Rabiy'ul Awwal 1427
Anasema Allaah سبحانه وتعالى :
((إِنَّ الْمُسْلِمِينَ وَالْمُسْلِمَاتِ وَالْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ وَالْقَانِتِينَ وَالْقَانِتَاتِ وَالصَّادِقِينَ وَالصَّادِقَاتِ وَالصَّابِرِينَ وَالصَّابِرَاتِ وَالْخَاشِعِينَ وَالْخَاشِعَاتِ وَالْمُتَصَدِّقِينَ وَالْمُتَصَدِّقَاتِ وَالصَّائِمِينَ وَالصَّائِمَاتِ وَالْحَافِظِينَ فُرُوجَهُمْ وَالْحَافِظَاتِ وَالذَّاكِرِينَ اللَّهَ كَثِيرًا وَالذَّاكِرَاتِ أَعَدَّ اللَّهُ لَهُم مَّغْفِرَةً وَأَجْرًا عَظِيمًا))
((Bila shaka Waislamu wanaume [wenye kufuata vizuri nguzo za Uislamu] na Waislamu wanawake [wenye kufuata vizuri nguzo za Uislamu], na Waumini wanaume [wanaoamini vizuri nguzo za Iymaan] na Waumini wanawake [wanaoamini vizuri nguzo za Iymaan], na wanaume wanaotii na wanawake wanaotii, na wanaume wasemao kweli na wanawake wasemao kweli, na wanaume wanaosubiri, na wanawake wanaosubiri, wanaume wanaonyenyekea na wanawake wanaonyenyekea, na wanaume wanaotoa [Zaka na] sadaka na wanawake wanaotoa [Zaka na] sadaka, na wanaume wanaofunga [Swawm] na wanawake wanaofunga [Swawm] na wanaume wanaojihifadhi tupu zao na wanawake wanojihifadhi tupu zao, na wanaume wanaomtaja Allaah kwa wingi na wanawake wanaomtaja Allaah [kwa wingi], Allaah Amewaandalia msamaha na ujira mkubwa)) [Al-Ahzaab:35]
Kama tunavyoona katika hiyo Aayah tukufu kuwa hizo ni sifa kumi Alizozitaja Allaah سبحانه وتعالى ambazo pindi Muislamu akizimiliki atapata kusamehewa makosa yake na juu yake atapata thawabu kubwa kutoka kwa Mola Mtukufu. Hivyo kila mmoja wetu ajiulize na ahesabu kama yumo katika kumiliki sifa hizi zote kumi au la. Na kama si zote, ikiwa ni moja tu au tatu tu au saba tu, basi tufanye juhudi ya kuzichuma sifa zilizobakia ambazo zimepunguka kwetu.
Tutaweka maelezo katika kila sifa moja hata tuweze kufahamu maana yake khaswa na kuwa kigezo bora cha mifano hiyo Insha Allaah سبحانه وتعالى huku tukimuomba Allaah سبحانه وتعالى Atuwezeshe kuzichuma sifa zote, na Atutakabalie amali zetu. Aamiyn.
Sababu ya kuteremshwa Aayah hii:
عن عبد الرحمن بن شيبة، سمعت أم سلمة زوج النبي صلى الله عليه وسلم تقول: قلت للنبي صلى الله عليه وسلم: ما لنا لا نُذْكَرُ في القرآن كما يذكر الرجال؟ قالت: فلم يَرعني منه ذات يوم إلا ونداؤه على المنبر، قالت، وأنا أسَرّح شعري، فلففت شعري، ثم خرجت إلى حُجْرة من حُجَر بيتي، فجعلت سمعي عند الجريد، فإذا هو يقول عند المنبر: ))يا أيها الناس، إن الله يقول: إن المسلمين والمسلمات والمؤمنين والمؤمنات )) إلى آخر الآية (الإمام أحمد)
Imetoka kwa 'Abdur-Rahmaan bin Shaybah kwamba: Nimemsikia Ummu Salamah رضي الله عنها mke wa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akisema: Nilimwambia Mtume صلى الله عليه وآله وسلم: kwa nini sisi wanawake hatutajwi (sana) katika Qur-aan kama wanavyotajwa wanaume? Kisha siku moja bila ya mimi kutambua, alikuwa akiita katika Minbar nami nilikuwa nikichana nywele zangu, nikazifunga nywele zangu nyuma kisha nikaingia chumbani katika vyumba vya nyumba yangu, nikaanza kusikiliza, naye alikuwa akisema kutoka katika Minbar: ((Enyi watu, Bila shaka Waislamu wanaume na Waislamu wanawake na Waumini wanaume na Waumini wanawake)) mpaka mwisho wa Aayah. [Imaam Ahmad]
SIFA YA KWANZA:
((نَّ الْمُسْلِمِينَ وَالْمُسْلِمَاتِ))
((Bila shaka Waislamu wanaume [wenye kufuata vizuri nguzo za Uislamu] na Waislamu wanawake [wenye kufuata vizuri nguzo za Uislamu]))
Kama tunavyojua sote kuwa nguzo za Kiislamu ni tano, hivyo kwanza kila mmoja wetu tuzitimize kama inavyotupasa kwa kadiri ya uwezo wetu. Nazo zimeelezwa katika Hadiyth ifuatayo:
عبدالله بن عمر قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم (( بُنِـيَ الإِسْلاَمُ علـى خَمْسٍ: شَهادَةِ أنْ لا إِلٰهَ إلا الله وأنَّ مُـحَمَّداً رَسُولُ الله وإِقامِ الصَّلاَةِ وإِيتاءِ الزَّكاةِ وَحَجِّ البَـيْتِ وَصَوْمِ رَمَضَانَ)) البخاري
Kutoka kwa ibnu 'Umar ambaye amesema: Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema: ((Uislamu umejengeka kwa matano; Kushuhudia (na kukiri kwa moyo) kwamba hakuna Mola Apasaye kuabudiwa (kwa haki) isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mjumbe wa Allaah na kuswali (Swalah tano), kutoa Zakah, kuhiji katika Nyumba (Makkah) na kufunga (mwezi wa) Ramadhaan)) [Al-Bukhaariy]
Lakini tujue nini maana ya Uislamu khaswa?
Uislamu unatokana na neno 'salaam' nalo ni maana ya 'amani'. Kwa hiyo tunapoamiliana na watu ikiwa ni Waislamu au wasio Waislamu inatupasa tuonyeshe sifa hii ya asili ya dini yetu kuwa ni dini ya amani na usalama na sio kama inavyodhaniwa siku hizi na makafiri wengi wa nchi za Magharibi. Na kudhihirisha sifa hii kwa makafiri huenda kukamtanabahisha mmoja wao akaipenda dini ya Kiislamu akasilimu kwa ajili tu ya kubainisha sifa hii njema. Mfano ni kama kisa kifuatacho:
Kisa cha Nabii Ibraahiym عليه السلام na Mmajusi kama kilivyosimuliwa na Shaykh Ash-Sha'arawiy (Allah Amrehemu)
Mmajusi mmoja alikwenda kwa Nabii Ibrahiym na kumuuliza kama anaweza kumpokea alale kwake. Nabii Ibraahiym عليه السلام akamuuliza: "Una dini gani?" Akajibu: "Dini yangu ni Mmajusi". Nabii Ibraahiym عليه السلام hakumpokea bali alimfungia mlango. Allaah سبحانه وتعالى Akamlaumu Nabii Ibraahiym عليه السلام kwa vipi anataka kumbadilisha dini yake ili tu ampokee kulala usiku mmoja? Na hali Yeye Allaah سبحانه وتعالى Ndiye Mwenye kumlisha huyo Mmajusi akiwa katika dini yake ya ukafiri? Nabii Ibraahiym عليه السلام akamkimbilia yule Mmajusi kumuomba msamaha. Mmajusi akamwambia: "Unanifuatia nini na hali umeziumiza hisia zangu?". Nabii Ibraahiym akamwambia: "Mola wangu Amenilaumu na kunigombesha kwa ajili yako". Yule Mmajusi akasema:
"نعم الرب رب يعاتب أحبابه في أعدائه "
"Mola Mzuri Alioje! Mola Anayewagombesha vipenzi Vyake kwa ajili ya maadui Wake!"
Hapo hapo akasilimu kuingia dini ya Nabii Ibraahiym عليه السلام ambayo ni dini hii hii yetu ya Kiislamu.
Huyu Mmajusi alimpenda Allaah سبحانه وتعالى baada ya kuona kwamba ni Mola Mwenye Rahma hata kwa makafiri, ndipo naye alipopenda Uislamu ndani ya moyo wake.
Shaykh Ash-Sha'araawiy anasema: "Baadhi ya watu wanatimzia sheria za Kiislamu kwa ajili ya khofu ya moto tu bila ya kuonja utamu wa Uislamu, na kama wangelionja utamu wa dini hii basi wangelipenda kufanya zaidi na zaidi kama khushuu (unyenyekevu) kwenye Swalah n.k."
************
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


