Zichume Sifa Kumi Njema - Sifa ya Pili - Waumini Wanaume Na Waumini Wanawake
07 Rabiy'ul Aakhir 1427 05-05-2006
Anasema Allaah سبحانه وتعالى:
((إِنَّ الْمُسْلِمِينَ وَالْمُسْلِمَاتِ وَالْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ …..))
((Bila shaka Waislamu wanaume [wenye kufuata vizuri nguzo za Uislamu] na Waislamu wanawake [wenye kufuata vizuri nguzo za Uislamu], na Waumini wanaume [wanaoamini vizuri nguzo za Iymaan] na Waumini wanawake……)) [wanaoamini vizuri nguzo za Iymaan ]
Katika Aayah hiyo tukufu, Allaah سبحانه وتعالى Ametaja sifa ya pili ambayo ni Waumini baada ya kutaja Waislamu. Kwa hivyo kuna tofuati baina ya Muislamu na Muumini.
Tofauti baina ya Muislamu na Muumini:
Tumepata mafunzo ya tofauti baina ya sifa mbili hizo kwanza kutoka katika Hadiyth ifuatayo:
عن عامر بن سعد بن أبي وقاص، عن أبيه قال: أعطى رسول الله صلى الله عليه وسلم رجالا ولم يعط رجلا منهم شيئًا، فقال سعد: يا رسول الله، أعطيت فلانًا وفلانا ولم تُعط فلانًا شيئًا، وهو مؤمن؟ فقال النبي صلى الله عليه وسلم: ))أو مسلم)) حتى أعادها سعد ثلاثا، والنبي صلى الله عليه وسلم يقول: ((أو مسلم)) ثم قال النبي صلى الله عليه وسلم: ((إني لأعطي رجالا وأدع من هو أحب إليّ منهم فلم أعطيه شيئًا؛ مخافة أن يكبوا في النار على وجوههم")) أحمد وأخرجاه في الصحيحين من حديث الزهري .
Imetoka kwa 'Aamir bin Sa'ad bin Abi Waqqaasw رضي الله عنه kutoka kwa baba yake ambaye amesema: Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alitoa (baadhi ya vitu) na kuwapa baadhi ya watu na akaacha kuwapa baadhi yao. Sa'ad akasema: "Ewe Mjumbe wa Allah, umempa fulani na fulani na fulani na fulani, lakini hukumpa chochote fulani ingawa naye ni Muumini". Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akasema: ((Au Muislamu)). Sa'ad akarudia kusema kauli hiyo mara tatu kila mara Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alijibu: ((Au Muislamu)). Kisha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akasema: ((Huenda nikawapa baadhi ya watu na nisiwape chochote wengine, ingawa wa mwisho ni kipenzi kwangu kuliko wa mwanzo. Siwapi vitu (hao) kwa khofu kwamba huenda wakatupwa katika moto)) [Ahmad na Al-Bukhaariy na Muslim wamesimulia kutoka kwa Az-Zuhriy]
Zama za Mtume صلى الله عليه وآله وسلم Mabedui walipoingia Uislamu walimjia Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na kumwambia kuwa wao wameamini. Lakini Allaah سبحانه وتعالى Anawajulisha kuwa kuna tofauti ya kusilimu na kuamini:
((قَالَتِ الْأَعْرَابُ آمَنَّا قُل لَّمْ تُؤْمِنُوا وَلَكِن قُولُوا أَسْلَمْنَا وَلَمَّا يَدْخُلِ الْإِيمَانُ فِي قُلُوبِكُمْ وَإِن تُطِيعُوا اللَّهَ وَرَسُولَهُ لَا يَلِتْكُم مِّنْ أَعْمَالِكُمْ شَيْئًا إِنَّ اللَّهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ))
((Mabedui wamesema: Tumeamini. Sema: Hamjaamini, lakini semeni: Tumesilimu. Kwani Iymaan haijaingia katika nyoyo zenu. Na mkimtii Allah na Mtume Wake, Hatakupunguzieni chochote katika vitendo vyenu. Hakika Allah ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu)) [Al-Hujuraat:14]
Aayah hii inathibitisha kuwa daraja ya Muumini ni ya juu kuliko ya Muislamu, na hii ni rai ya Maulamaa wa Ahlus-Sunnah wal-Jamaa'ah. Na Aayah hii imeonyesha kwamba kuamini ni kumtii Allah na Mtume Wake صلى الله عليه وآله وسلم. Kumuamini Yeye kwa kufuata yale yote Aliyotuamrisha na kujiepusha na yale Aliyotuharamisha katika Qur-aan.
Mfano kutofanya maasi yaliyotajwa katika Hadiyth ifuatayo iliyopokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه
((لا يزني الزاني حين يزني وهو مؤمن ، ولا يشرب الخمر حين يشربها وهو مؤمن ، ولا يسرق السارق حين يسرق وهو مؤمن)) البخاري
((Hazini mzinifu anapozini hali ya kuwa ni Muumini, wala hanywi pombe anapokunywa hali ya kuwa ni Muumini, wala haibi mwizi anapoiba hali ya kuwa ni Muumini)) [Al-Bukhaariy]
Na kumtii Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ni kufuata amri zake na mafunzo yote aliyotuletea katika Sunnah zake, hapo ndipo Iymaan itakuwa imeingia moyoni mwa Muislamu.
Kisa cha Julaybiyb na Swahaabiyah aliyemtii Mtume صلى الله عليه وآله وسلم
Swahaba aliyeitwa Julaybiyb alijulikana sana kuwa alikuwa ni mtu duni asiyemiliki mali na hakuwa ni mzuri kwa sura na umbo, na alikuwa ni mtu wa kuchekesha watu. Kwa hivyo hakuna aliyetaka kumuozesha binti yake. Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alimuuliza Julaybib kama anataka kuoa, naye akamjibu: "Ewe Mjumbe wa Allah, nani atakayekubali nimuoe mimi? Sina nyumba wala wala mali wala chochote katika mapambo ya dunia". Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akamtuma mtu mmoja aende nyumba ya Answaariy fulani ambao walikuwa ni familia yenye kujulikana kwa kabila lao maarufu kubwa lenye kujulikana kwa heshima na wenye hali nzuri. Alipopiga hodi, alifungua mlango mama wa binti huyo. Swahaba akamjulisha kuwa ametumwa na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kuleta posa kwa binti yake. Mama huyo alifurahi sana kudhania kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ndiye anayetaka kumposa binti yake. Swahaba Alipomjulisha kuwa sio kwa ajili ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم, bali ni kwa ajili ya Julaybiyb, mama huyo alisema: "Nani? Julaybib? Hapana! Hatumuozeshi yeye binti yetu!". Mara yule binti alisikia mazungumzo hayo akaja kuuliza vizuri: "Nani anayetaka kuniposa?" Mama mtu akamuelezea kuwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amemtuma mtu aje kumposa yeye kwa ajili ya Julaybiyb. Binti huyo alimwambia mama yake: "Vipi mama unakataa amri ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم? Fuata amri yake kwani hakuna kitakachonidhuru". (Katika usemi mmoja ni kwamba hapo hapo Aayah ifuatayo iliteremshwa [Ibnu Kathiyr 7:692-694]) na katika usemi mwingine aliwaambia wazazi wake: "Hamkusikia kauli ya Allaah سبحانه وتعالى:
((وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ وَمَن يَعْصِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا))
((Haiwi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke kuwa na khiari katika jambo, Allah na Mtume Wake Wanapokata shauri katika jambo lao. Na mwenye kumuasi Allah na Mtume Wake basi hakika amepotea upotofu ulio wazi))[Al-Ahzaab:36]
Ikabidi wamuozeshe binti yao kwa Julaybiyb. Kisha katika vita fulani alitoka Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na Maswahaba miongoni mwao ni Julaybiyb na baada ya ushindi wa vita hivyo, Mtume صلى الله عليه وآله وسلم aliwauliza Maswahaba kabla ya kurudi: ((Je, kuna mtu aliyekosekana?)) Wakataja baadhi ya Maswahaba waliokosekana kisha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akawauliza tena wakasema: "Hakuna mtu mwingine aliyekosekana: Lakini Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akasema: ((Lakini mimi naona kwamba Julaybiyb amekosekana)) yaani hayupo na sisi. (Nendeni mkamtafute miongoni mwa waliouliwa)). Wakaenda Maswahaba kumtafuta wakamkuta ameuawa akiwa karibu yake makafiri saba ambao aliwahi kuwaua yeye Julaybiyb. Maswahaba wakamjulisha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ambaye alikwenda na kusimama karibu naye kisha akasema: ((Ameua saba kisha wakamuua. Yeye ni wangu na mimi ni wake)).
Alisema hivyo mara mbili au tatu, kisha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akambeba kwa mikono yake na kwenda kumzika. Na akamuombea Du'aa mke wake:
((الَّلهُمَّ، صَبَّ عَلَيْهَا [الخير] صَبَّا، وَلاَ تَجْعَل عَيْشَها كَدَّا))
((Ewe Allah, Mjaze kheri (nyingi) zilizojaa na Usimjaaliye maisha yake kuwa ni ya shida [tabu na mashaka]))
Imesemekana kwamba hakuweko mjane aliyekuwa ana maisha mema kama maisha ya mke wa Julaybiy رضي الله عنه
[Kisa kimesimuliwa na Imaam Ahmad Muslim na An-Nasaaiy]
Baada ya Aayah hiyo katika Suratul-Hujuraat inayotujulisha kwamba kuamini ni kumtii Allaah سبحانه وتعالى na Mtume Wake صلى الله عليه وآله وسلم kisha Anaendelea Allaah سبحانه وتعالى Kutujulisha nani hasa ni Waumini wa kweli waliosadiki:
((إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا بِاللَّهِ وَرَسُولِهِ ثُمَّ لَمْ يَرْتَابُوا وَجَاهَدُوا بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ فِي سَبِيلِ اللَّهِ أُوْلَئِكَ هُمُ الصَّادِقُونَ))
((Hakika Waumini ni wale waliomuamini Allah na Mtume Wake tena wasitie shaka kabisa, na wakapigana Jihadi katika Njia ya Allah kwa mali yao na nafsi zao. Hao ndio wakweli)) [Al-Hujuraat:15]
Tutazame mfano wa wale walioamini kweli katika kupigana Jihaad kwa nafsi zao katika kisa kifuatacho:
Kisa Cha Handhwalah "Aliyeoshwa na Malaika"
Handhwala bin Abi 'Aamir ni Swahaba ambaye alifunga ndoa usiku ambao ulinadiwa vita vya Uhud. Aliwahi kulala na mke wake usiku huo mmoja lakini iliponadiwa sauti ya kutoka kwenda Jihaad hakuna chochote kilichomshughulisha wakati huo ila ni kutoka na kukimbilia vitani hata hakuwahi kukoga janaba.
Baada ya vita kumalizika Mtume صلى الله عليه وآله وسلم aliwaambia Maswahaba kwamba Malaika wamemuosha Handhwalah. Akawatuma wakaulize nyumbani kwake alitoka vipi? Mkewe akawajulisha kuwa alitoka bila ya kuwahi kukoga janaba. Walipokwenda kumtazama Handhwalah walimuona akichirizikwa na maji kama kwamba katokwa kukoshwa. Tokea siku hiyo akajulikana na kuitwa "Aliyeoshwa na Malaika".
Hao ndio Maswahaba walioamini kweli wakajitolea nafsi zao bila ya kuona umuhimu wa jambo lolote jengine mbele ya Jihaad katika Njia ya Allah.
************
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


