Skip navigation.
Home kabah

Zichume Sifa Kumi Njema - Sifa Ya Nne - Wanaume Wasemao Kweli Na Wanawake Wasemao Kweli

21 Rabiy'ul Aakhir 1427   19-05-2006


Anasema Allaah سبحانه وتعالى :

((إِنَّ الْمُسْلِمِينَ وَالْمُسْلِمَاتِ وَالْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ وَالْقَانِتِينَ وَالْقَانِتَاتِ وَالصَّادِقِينَ وَالصَّادِقَاتِ))

((Bila shaka Waislamu wanaume na Waislamu wanawake  na Waumini wanaume na Waumini wanawake  na wanaume wanaotii na wanawake wanaotii, na wanaume wasemao kweli na wanawake wasemao kweli)) [Al-Ahzaab:35]

 

Sifa ya nne ni 'wasemao kweli', nayo inakusudiwa katika usemi wao, vitendo vyao, na niya zao kama baadhi ya wafasiri wa Qur-aan walivyonukuu.

Vile Vile Allaah سبحانه وتعالى Ametunasihi tuambatane na wanaosema kweli:

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ اتَّقُواْ اللّهَ وَكُونُواْ مَعَ الصَّادِقِينَ))

((Enyi mlioamini! Mcheni Allah, na kuweni pamoja na wakweli)) [At-Tawbah:119]

Kusema kweli ni alama ya iymaan kama ambavyo kusema uongo ni alama ya unafiki.

Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema:

عَلَيْكُمْ بِالصِّدْقِ فَإِنَّ الصِّدْق يَهْدِي إِلَى الْبِرّ وَإِنَّ الْبِرّ يَهْدِي إِلَى الْجَنَّة وَإِيَّاكُمْ وَالْكَذِب فَإِنَّ الْكَذِب يَهْدِي إِلَى الْفُجُور وَإِنَّ الْفُجُور يَهْدِي إِلَى النَّار وَلَا يَزَال الرَّجُل يَصْدُق وَيَتَحَرَّى الصِّدْق حَتَّى يُكْتَب عِنْد اللَّه صِدِّيقًا وَلَا يَزَال الرَّجُل يَكْذِب وَيَتَحَرَّى الْكَذِب حَتَّى يُكْتَب عِنْد اللَّه كَذَّابًا)) مسلم

 ((Shikamaneni na ukweli, kwani ukweli unapeleka katika wema, na wema unapeleka Peponi. Na jihadharini na uongo, kwani uongo unapeleka kwenye uovu, na uovu hupeleka katika moto. Mtu huendelea kusema ukweli na kujitahidi kuendelea hivyo hadi itarekodiwa na Allah kuwa ni mkweli. Na mtu huendelea kusema uongo na ataendelea kufanya hivyo hadi itarekodiwa na Allah kuwa ni muongo)) [Muslim]

 

Baadhi ya Maswahaba رضي الله عنهم  wamejulikana kwamba hawajapata kusema uongo maishani mwao abadan, tokea siku za Ujaahiliyyah (zama za ujinga yaani kabla ya Uislam) wala hawakuwahi kusema uongo katika Uislam. Na mmojawao ni Abubakar رضي الله عنه  ambaye alipewa cheo cha 'As-Swiddiyq'.

Abubakar رضي الله عنه  na sababu za kupewa cheo cha  

'As-Swiddiyq' (Msema kweli )

Al-Imaam An-Nawawiy amesema: "Ummah umekubaliana kwa pamoja bila ya kupingana kwamba amepewa cheo cha 'As-Swiddiyq' kutokana na kuitikia kwake haraka kumuamini Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  bila ya kusita na kukubali maneno yake kwamba daima ni ya ukweli. Alibakia kuwa mkweli maishani mwake kote wala hajapata kusema uongo  hata mara moja". 

Ibn Kathiyr amesema: "Kuhusu cheo chake cha  'As-Swiddiyq', inasemekana kwamba alipewa tokea zama za Ujaahiliyyah kutokana na ukweli uliojulikana kwamba alikuwa ni mkweli. Vile vile imesemekana kwamba amepewa cheo hicho kwa sababu alikuwa daima yuko tayari kumuamini Mtume صلى الله عليه وآله وسلم katika kila jambo alilosema".

Baadhi ya matukio yaliyodhihirisha ukweli wake na wepesi wake wa kuamini lolote alilosema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم :

   1.     Katika kisa cha Israa Wal-Mi'raaj alipobakia kuwa thabiti na kuwaambia makafiri kwamba ikiwa Muhammad  صلى الله عليه وآله وسلم  mwenyewe ametamka maelezo hayo basi ni kweli!

Ibn Kathiyr amesema: "Al-Hasan Al-Baswriy na Qataadah wamesema: "Alijulikana kwa mara ya kwanza kwa cheo hiki asubuhi ya siku ya tukio la Israa". Al-Haakim amesimulia kutoka kwa Bibi 'Aishah رضي الله عنها  ambaye amesema: Washirikina walikuja kwa Abubakar wakamwambia: "Umemsikia rafiki yako anavyodai? Anadai kwamba amesafiri kwenda Baytul-Maqdis kwa usiku mmoja" Akauliza: "Je, amesema mwenyewe hivyo?". Wakajibu: "Ndio". Akasema: "Basi amesema ukweli! Naamini ukweli wake katika mambo yaliyo ya ajabu zaidi kuliko hayo, kama 'habari kutoka mbinguni asubuhi na jioni" (yaani wahyi wa Qur-aan). Tokea hapo Abubakar akapewa cheo cha 'As-Swiddiyq'.  [Ibn Kathiyr kasema Isnaad yake ni nzuri].

Al-Haakim amesimulia kutoka Nazaal ibn Swabrah ambaye amesema: "Tulimwambia 'Aliy: "Ewe kamanda wa waumini! Tuelezee kuhusu Abubakar". Akasema: "Ni mtu aliyepewa jina la 'As-Swiddiyq' na Allaah سبحانه وتعالى kwa kauli ya Jibriyl عليه السلام na kauli ya Muhammad  صلى الله عليه وآله وسلم . Alikuwa ni Khalifa  wa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم. Yeye Mtume صلى الله عليه وآله وسلم aliridhika naye katika dini yetu na aliridhika naye katika mambo yetu ya kidunia".  [Ibn Kathiyr kasema: Isnaad yake ni nzuri]

Na katika Hadiyth ya vita vya Uhud, Mtume صلى الله عليه وآله وسلم aliliambia jabali  la Uhud lilipotikisika (kwa kulipapasa)

((أثبت أحد فإنما عليك نبي وصديق وشهيدان))

((Tulia kwani juu yako yumo Mtume, As-Swiddiyq na mashahidi wawili)) (yaani Umar na Uthmaan رضي الله عنهم) [Al-Bukhaariy]

2.     Kuhama (Hijrah) kwake na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akiwa ameacha familia yake ili abakie na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم . Maswahaba wote waliruhusiwa na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kuhama (Hijrah kutoka Makkah kwenda Madiynah) isipokuwa Abubakar. Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akimwambia abakie ili awe swahib (rafiki) yake katika Hijrah na Allaah سبحانه وتعالى Akatimiza pendekezo la Mjume Wake  صلى الله عليه وآله وسلم . Kisha yaliyotokea walipokimbilia katika pango la At-Thawr na   Aayah iliyoteremeshwa kuelezea hivyo:

  ((إِلاَّ تَنصُرُوهُ فَقَدْ نَصَرَهُ اللّهُ إِذْ أَخْرَجَهُ الَّذِينَ كَفَرُواْ ثَانِيَ اثْنَيْنِ إِذْ هُمَا فِي الْغَار إِذْ يَقُولُ لِصَاحِبِهِ لاَ تَحْزَنْ إِنَّ اللّهَ مَعَنَا فَأَنزَلَ اللّهُ سَكِينَتَهُ عَلَيْهِ وَأَيَّدَهُ بِجُنُود لَّمْ تَرَوْهَا وَجَعَلَ كَلِمَةَ الَّذِينَ كَفَرُواْ السُّفْلَى وَكَلِمَةُ اللّهِ هِيَ الْعُلْيَا وَاللّهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ))

ِ

ٍ

((Ikiwa nyinyi hamtamnusuru Mtume, basi Allah  Alikwishamnusuru walipomtoa waliokufuru, naye ni wa pili katika wawili walipokuwa katika pango, naye akamwambia swahibu yake: Usihuzunike. Hakika Allah Yu pamoja nasi. Allah Akamteremshia utulivu wake, na Akamuunga mkono kwa majeshi msiyoyaona, na Akalifanya neno la waliokufuru kuwa chini, na Neno la Allah kuwa ndilo juu. Na Allah ndiye Mwenye nguvu Mwenye hikima)) [At-Tawbah:40

3.     Alipolia wakati Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alisema: ((Hakika kuna mja alipewa uchaguzi na Allaah سبحانه وتعالى   baina ya Duniya na Akhera, mja akachagua Akhera)). Abubakar alijua kuwa huyo mja ni Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na alitambua kauli hiyo imemaanisha kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  ataaga duniya karibuni. [Al-Bukhaariy]

4.      Alipobakia kuwa thabiti katika kifo cha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم wakati Maswahaba waliduwaa hawakujua la kufanya na khutbah yake aliyotoa ya kuwatuliza.

         5.       Kuthibitika kwake ingawa alikuwa pekee katika kupeleka jeshi na       kumfanya Usaamah bin Zayd awe mwenye kuongoza jeshi.

6.      Kung'angania kwake katika kupigana na watu waliotoka nje ya Uislam baada ya kifo cha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم

7.     Alipomchagua 'Umar ibnul-Khatwaab رضي الله عنه kuwa Khaliyfah wa      Waislam, jambo ambalo limeainishwa na Maulamaa kuwa ni jambo muhimu la mafanikio.

 

************