Zichume Sifa Kumi Njema - Sifa Ya Sita - Wanaume Wanyenyekevu Na Wanawake Wanyenyekevu
Anasema Allaah سبحانه وتعالى :
((إِنَّ الْمُسْلِمِينَ وَالْمُسْلِمَاتِ وَالْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ وَالْقَانِتِينَ وَالْقَانِتَاتِ وَالصَّادِقِينَ وَالصَّادِقَاتِ وَالصَّابِرِينَ وَالصَّابِرَاتِ وَالْخَاشِعِينَ وَالْخَاشِعَاتِ ))
((Hakika Waislamu wanaume na Waislamu wanawake, na Waumini wanaume na Waumini wanawake, na watiifu wanaume na watiifu wanawake, na wasemao kweli wanaume na wanawake, na wanao subiri wanaume na wanawake, na wanyenyekevu wanaume na wanawake ….))
Nini maana ya Khushuu?
Khushuu'u (unyenyekevu) ina maana; utulivu, ushwari, amani, kutahadhari, kuzungumza kwa taratibu kwa uangalifu, hadhi na unyenyekevu. Linalomtia mtu hamasa kuwa katika hali hiyo ni khofu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na utambuzi kuwa Mola Anatutazama tunayoyatenda kila wakati kama ilivyokuja katika Hadiyth ndefu alipokuja Jibriyl ('alayhis-salaam) kwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
((...أنْ تَعْبُدَ الله كَأَنَّكَ تَرَاهُ فإنْ لَمْ تَكُنْ تَرَاهُ فإنَّهُ يَرَاك))
((….. na umuabudu Allah kama kwamba unamuona, na kama humuoni basi Yeye Anakuona))
Khushuu' katika Swalah:
Khushuu (unyenyekevu) ni jambo gumu hakika hasa katika Swalah kwani shaytwaan ndipo mahali anapopenda sana kumharibia mja 'amali yake. Lakini inakupasa Muislam unaposwali au kuomba Du'aa, ujitahidi kumuepuka shaytwaan asikutie wasi wasi bali uwe ni mwenye kunyenyekea kwa unyonge. Akili na moyo wako uwe mtupu usioshughulika na mengine yoyote isipokuwa ni khofu ya kuwa mbele ya Mola wako ukiyatia akilini na moyoni yale unayoyasoma au kuomba na ukikumbuka kuwa Yeye Anakuona ingawa wewe humuoni.
Hivyo utambue kuwa unazungumza na Mola Mtukufu, Mwenye kumiliki yote yaliyo mbinguni na ardhini na utukufu wote Alionao pamoja na Sifa Zake zote zisizomhusu mwingine yeyote. Na hapo ndipo utakapokuwa umeipata sifa hiyo njema kabisa ya khushuu ambayo Ameitaja Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) katika Qur-aan pamoja na sifa nyingine ambazo pindi Muislam akizitimiza atapata fadhila za kupata Pepo ya Firdaws:
بِسْمِ اللّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ
قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ ﴿1﴾ الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ ﴿2﴾ وَالَّذِينَ هُمْ عَنِ اللَّغْوِ مُعْرِضُونَ ﴿3﴾ وَالَّذِينَ هُمْ لِلزَّكَاةِ فَاعِلُونَ ﴿4﴾ وَالَّذِينَ هُمْ لِفُرُوجِهِمْ حَافِظُونَ ﴿5﴾ إِلَّا عَلَى أَزْوَاجِهِمْ أوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَإِنَّهُمْ غَيْرُ مَلُومِينَ ﴿6﴾ فَمَنِ ابْتَغَى وَرَاء ذَلِكَ فَأُوْلَئِكَ هُمُ الْعَادُونَ ﴿7﴾ وَالَّذِينَ هُمْ لِأَمَانَاتِهِمْ وَعَهْدِهِمْ رَاعُونَ ﴿8﴾ وَالَّذِينَ هُمْ عَلَى صَلَوَاتِهِمْ يُحَافِظُونَ ﴿9﴾ أُوْلَئِكَ هُمُ الْوَارِثُونَ ﴿10﴾ الَّذِينَ يَرِثُونَ الْفِرْدَوْسَ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿11﴾
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. HAKIKA wamefanikiwa Waumini,
2. Ambao ni wanyenyekevu katika Swalah zao,
3. Na ambao hujiepusha na mambo ya upuuzi,
4. Na ambao wanatoa Zaka,
5. Na ambao wanazilinda tupu zao.
6. Isipokuwa kwa wake zao au kwa iliyowamiliki mikono yao ya kulia. Kwani hao si wenye kulaumiwa,
7. Lakini anayetaka kinyume cha haya, basi hao ndio warukao mipaka.
8. Na ambao wanazitimiza amana zao na ahadi zao,
9. Na ambao Swalah zao wanazihifadhi,
10. Hao ndio warithi
11. Ambao watairithi Pepo ya Firdawsi, wadumu humo.
[Al-Muuminuun: 1-11]
Abu Twalha Al-Answaariy na khofu yake ya kupoteza khushuu katika Swalah:
Alikuwa akiswali katika bustani yake siku moja, akamuona ndege anaruka ruka baina ya miti. Baada ya kumtazama na kurudisha macho yake na akili yake katika Swalah, alisahau ameswali Raka'ah ngapi. Akaenda kwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) huku akilia na kumwambia: "Ewe Mjume wa Allah! Hakika mimi nimejishughulisha akili yangu na ndege katika bustani yangu wakati nina swali hata nimesahau nimeswali Raka'ah ngapi. Kwa hiyo naitoa hii bustani iwe sadaka Fiy Sabili-Allah, ipokee ewe Mjumbe wa Allah na ifanye utakavyo labda Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atanighufuria".
Kisa cha 'Urwah bin Zubayr na khushuu ya ajabu aliyokuwa nayo katika Swalah:
Ni mtoto wa Asmaa bint Abubakar ambaye pia ni dada yake bibi 'Aishah mke wa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Baba yake ni Zubayr ambaye ndiye mume wa Asmaa bint Abubakar (Radhiya Allahu 'anha).
Alipatwa na maradhi ya saratani (cancer) katika mguu wake, akaambiwa na madaktari kuwa lazima akatwe mguu wake ili maradhi yasienee mwilini mwake. Kwa hivyo hana budi ila anywe pombe ili asihisi maumivu. (Zama hizo kulikuwa hakuna sindano au dawa za kisasa za kuondosha fahamu ya mtu anapofanyiwa operesheni). Alipoambiwa hivyo 'Urwah alijibu: "Moyo wangu na ulimi wangu upotee katika kumkumbuka Allah? WaLLahi sitoingia katika maasi kwa ajili hiyo". Wakamwambia: "Tutakupa kileweshacho (kuondosha fahamu) kama vile unusukaputi". Akasema: "Sipendi kuchomolewa kipande katika mwili wangu nikiwa katika hali ya kulala". Wakamwambia: "Tumlete mtu akukamate". Akasema: "Niachilieni mwenyewe hivi hivi" (yaani mnikate huu mguu hivi hivi bila ya kunipa chochote). Wakamwambia: "Hutoweza kuvumilia". Akasema: "Niacheni niswali. Mtakakaponiona sitingishiki nikiwa nimetuliza misuli yangu nikiwa niko imara nisubirini hadi nitakapokwenda kusujudu. Kisha nitakaposujudu hapo huwa sifikirii dunia. (Maana kwamba huwa sioni wala sisikii lolote, wa kuhisi chochote wala sina habari ya lolote isipokuwa niko na Mola wangu katika khushuu). Hapo tena fanyeni mnavyotaka kunifanya".
Akaja daktari akasubiri. Aliposujudu 'Urwah, daktari akaleta msumeno akamkata mguu wake. Hakuwa anasema kitu 'Urwah isipokuwa:
لا إلهَ إلاّ اللّه, رَضيـتُ بِاللهِ رَبَّـاً وَبِالإسْلامِ ديـناً وَبِمُحَـمَّدٍ صََلى الله عليه وسلم نَبِيّـاً وَرَسُولاً .
Laa Ilaa Illah Allah, Radhwiytu BiLLahi Rabba, wa bil-Islaami Diyna, wa bi Muhammadin Swalla Allahu 'alayhi wa wa sallam Nabiyyaw-wa Rasuula".
“Nimeridhika kuwa Allah Ndiye Mola wangu, na Uislamu ndio dini yangu, na Muhammad Swalla Allahu 'alayhi wa sallam kuwa ni Mtume na Mjumbe wangu”.
Akaendelea hivyo hadi akamaliza daktari kazi yake ya kumkata mguu, damu ikiwa inamchirizika. Hakupiga kelele 'Urwah wala kuugua kwa maumivu!
Alipozindukana 'Urwah, akaletewa mguu wake akautazama, huku akiuambia: "Naapa kwa Allah! Sijapata kukupeleka (kutembea nao mguu huu) katika mambo ya haram, na Allah Anajua. Mara ngapi nimesimama nawe usiku kwa ajili ya Allah!". Mmoja wao akamuambia: "Ewe 'Urwah! Bishara! (Au pongezi!) Kipande cha mwili wako kimetangulia Peponi!". Akasema: WaLLahi hajapata mtu kuniliwaza maliwazo bora kama haya!
************
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


