Skip navigation.
Home kabah

Umuhimu Wa Kukimbilia Kutekeleza Nguzo Ya Hajj

www.alhidaaya.com

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

 

 

((وَلِلّهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلاً وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ الله غَنِيٌّ عَنِ الْعَالَمِينَ))

 

 

((Na kwa ajili ya Allah imewajibikia watu wahiji kwenye Nyumba hiyo, kwa yule awezae njia ya kwendea. Na atakayekanusha basi Allah si mhitaji kwa walimwengu)) [Al-'Imraan:96-97]

 

 

Na kauli ya Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

 

((بني الإسلام على خمس شهادة أَنْ لا إلهَ إلا اللهُ وأَنَّ محمِّداً رسولُ الله وإقام الصلاة ، وإيتاء الزكاة، وصوم رمضان، وحج البيت))   متفق عليه

 

 

((Uislamu umejengeka kwa matano; Kushuhudia kwamba hakuna Mola apasaye kuabudiwa isipokuwa Allah, na Muhammad ni Mjumbe wa Allah, kusimamisha Swalah, kutoa Zakaah, kufunga Ramadhaan, na kuhijii katika Nyumba (tukufu))) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Tunatambua kutokana na kauli hizo za utangulizi kuwa kutekeleza ibada ya Hijjah ni fardh kwa kila mwenye uwezo. Hivyo asiyeharakisha kutekeleza ibada hii atakuwa amemuasi Mola wake Mtukufu na Mjumbe Wake (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na itakuwa ni dhambi kubwa kwake ikiwa kuacha huko ni kwa makusudi na hali alikuwa ana uwezo wa mali, siha n.k., sababu atakuwa amekanusha amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kama Anavyosema:

 

 

((وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ وَمَن يَعْصِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا))

 

((Haiwi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke kuwa na khiari katika jambo, Allah na Mtume Wake wanapokata shauri katika jambo lao. Na mwenye kumuasi Allah na Mtume Wake basi hakika amepotea upotofu ulio wazi)) [al-Ahzaab:36]

 

 

KWA NINI MUISLAM AHARAKISHE KUTEKELEZA HAJJ?

 

HUENDA AKAFIKWA NA MASAIBU:

 

 

Muislamu mwenye uwezo  wa fedha na siha inampasa afanye hima kutimiza fardhi hii kabla ya kufikwa na masaibu kwani huenda ukawa humiliki tena siku za mbele.

 

Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametuhimiza na kutuonya hayo:  

 

 

  (( مَنْ أَرَادَ الْحَجَّ فَلْيَتَعَجَّلْ )) . رواه الإمام أحمد وأبو داود وابن ماجه . وفي رواية أحمد وابن ماجه : (( فَإِنَّهُ قَدْ يَمْرَضُ الْمَرِيضُ ، وَتَعْرِضُ الْحَاجَةُ))  حسنه الألباني في صحيح ابن ماجه  

 

 

 ((Mwenye kutaka kufanya Hijjah basi aharakize)) [Imaam Ahmad, Abu Daawuud na Ibn Maajah] na katika riwaaya ya Ahmad na Ibn Maajah ((Kwani huenda akapata maradhi au

akafikwa na haja))  [Kaipa daraja ya hasan Shaykh Al-Albaani katika Swahiyh-Ibn Maajah]

 

 

Vile vile amesema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

 

  (( تعجلوا إلى الحج  (يعني الفريضة)  (( فإن أحدكم لا يدري ما يعرض له))    أخرجه الإمام أحمد رحمه الله   وحسَّنه الألباني في إرواء الغليل   .

 

((Harakizeni  Hajj, (yaani kutekeleza fardhi ya Hajj) ((kwani hajui mmoja wenu nini kitamsibu)) [Imaam Ahmad na kaipa daraja ya hasan Shaykh Al-Albaaniy katika Irwaau-l-ghaliyl]

 

HATUNA DHAMANA NA UMRI MREFU:

 

 

Waislamu wengi hawaifanyii hima ibada hii na aghalabu ya sababu ni:

 

 

Wengine huona kuwa ni bado vijana hivyo wanasubiri wawe na umri mkubwa ndio watimize. Hao wajiulize; je, wana uhakika gani kuwa wataruzukiwa umri mrefu? Bali wana dhamana gani kama wataishi hata mwaka mmoja zaidi? Au mwezi mmoja zaidi? Au wiki moja zaidi? Au hata siku moja zaidi? Hawasomi kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

(( وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ مَّاذَا تَكْسِبُ غَدًا وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ بِأَيِّ أَرْضٍ تَمُوتُ إِنَّ اللَّهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ))  

((Na haijui nafsi yeyote itachuma nini kesho. Wala nafsi yeyote haijui itafia nchi gani. Hakika Allah Ndiye Mwenye kujua, Mwenye khabari)) [Luqmaan:34]

Wengine wameshughulika na anasa za dunia na kujisahau kabisa kama huenda wakaondoka duniani wakiwa katika hali hizo za mapenzi ya dunia huku wameacha kutenda yaliyo muhimu kama ibada hii ya fardhi. Nafsi inayojidhulumu kama hivi hujuta wakati wa kutolewa roho yake, na hutamani arudi atende yale aliyoyakosa kutenda lakini kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

 

 

((حَتَّى إِذَا جَاء أَحَدَهُمُ الْمَوْتُ قَالَ رَبِّ ارْجِعُونِ))

 

(( لَعَلِّي أَعْمَلُ صَالِحًا فِيمَا تَرَكْتُ كَلَّا إِنَّهَا كَلِمَةٌ هُوَ قَائِلُهَا وَمِن وَرَائِهِم بَرْزَخٌ إِلَى  يَوْمِ يُبْعَثُونَ ))

((Mpaka yanapomfikia mmoja wao mauti, husema: Mola wangu Mlezi! Nirudishe))

((Ili nitende mema sasa badala ya yale niliyo yaacha. Wapi! Hii ni kauli aisemayo yeye tu. Na nyuma yao kipo kizuizi mpaka siku watapo fufuliwa)) [Al-Mu'minuun:99-100]

 

NI AMALI BORA KABISA:

 

  سئل النبي صلى الله عليه وسلم أي العمل أفضل؟ قال: ((إيمان بالله ورسوله)) قيل: ثم ماذا؟ قال:  ((الجهاد في سبيل الله))" قيل ثم ماذا؟ قال: ((حج مبرور))  متفق عليه

 

 

Aliulizwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Ipi amali njema kabisa? Akasema: ((Kumuamini Allah na Mjumbe Wake)) Akaulizwa: "Kisha nini"? Akasema: ((Jihaad katika Njia ya Allah)) Akaulizwa: "Kisha nini"? Aakasema: ((Hajj yenye kukubaliwa)) [al-Bukhaariy na Muslim]

 

HUFUTIWA MADHAMBI YOTE:

 

 

عن أبي هريرة رضي الله عنه  قال سمعت رسول الله صلى الله عليه وسلم يقول: ((من حج، فلم يرفث ولم يفسق، رجع كيوم ولدته أمه)) متفق عليه

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allahu 'anhu) ambaye amesema: "Nimemsikia Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Atakayefanya Hajj, kisha asiseme maneno machafu wala asitende vitendo vichafu atarudi akiwa kama siku aliyozaliwa na mama yake)) [al-Bukhaariy na Muslim]

 

JAZAA YAKE NI PEPO:

 

 

عن أبي هريرة رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: "((العمرة إلى العمرة كفارة لما بينهما، والحج المبرور ليس له جزاء إلا الجنة)) متفق عليه  

 

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (('Umrah hadi 'Umrah ni kafara (kufutiwa dhambi) baina yao, na Hajjul-Mabruur (Hajj yenye kukubaliwa) haina jazaa isipokuwa ni Pepo)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Awajaalie ndugu zetu wote Waislamu uwezo wa kutekeleza nguzo hii muhimu na Awalipe wote wanaojaaliwa kuitekeleza Pepo Yake Na'iym Aliyotuahidi. Aaamiyn.