Mwenye Kufanya Na Kuelimisha Sunnah Nzuri Katika Uislam Na Mwenye Kulingania Upotofu

Jibu la Shaykh 'Abdul 'Aziyz bin Baaz

Imetarjumiwa na Ummu Iyyaad

 

SWALI:  Kuhusu kauli ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) ((Atakayetenda kitendo kizuri (Sunnatun-hasana) katika Uislamu atapata ujira wake na ujira wa yule atakayekitenda….))

Je, kwanza hii ni Hadiyth (Swahiyh?) 

Pili, kama ni Hadiyth (Swahiyh) je, Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam) aliacha jambo (la Sunnah) kwetu ambalo hakulifanya yeye ili lije kutendwa baada yake katika Uislamu? Tunaomba utufahamishe kwa kutufafanulia wazi jambo hili.

Shaykh 'Abdul-'Aziyz bin Baaz (Rahihamu-Allaah) akajibu:

JIBU:

Hadiyth hii ni Swahiyh nayo inatuonyesha hukumu ya kuruhusu kuhuisha Sunnah, kuifundisha na kutahadharisha bid'ah na maovu. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) amesema:

((من سن في الإسلام سنة حسنة كان له أجرها وأجر من عمل بها من بعده لا ينقص ذلك من أجورهم شيئاً ومن سن في الإسلام سنة سيئة كان عليه وزرها ووزر من عمل بها من بعده لا ينقص من أوزارهم شيئاً)) خرجه مسلم في صحيحه

((Atakayetenda kitendo kizuri (Sunnatun-hasanah) katika Uislamu   atapata ujira wake na ujira wa yule atakayekitenda baada yake bila ya kupungukiwa thawabu zao. Na atakayetenda kitendo kibaya katika Uislamu atabeba (mzigo wa) dhambi zake na dhambi za yule atakayetenda wala hapungukiwi kitu katika (mzigo wa) dhambi hizo)) Muslim  

Mfano pia ni Hadiyth iliyotoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) kasema:

(( من دعا إلى هدى كان له من الأجر من أجور من تبعه لا ينقص من أجورهم شيئاً ومن دعا إلى ضلالة كان عليه من الإثم مثل آثام من تبعه لا ينقص ذلك من آثامهم شيئاً)) مسلم

((Atakayelingania uongofu atapata ujirwa wa yule atakayemfuata bila ya kupungukiwa chochote katika ujira huo, na atakayelingania katika upotofu atapata dhambi mfano wa dhambi za yule atakayefuata bila ya kupungukiwa chochote katika dhambi zao)) Muslim

Maana ya (Atakayetenda kitendo kizuri (Sunnatun-hasana) katika Uislamu) ni kuihuisha, kuidhihirisha na kuifichua Sunnah ambayo imefichika kwa watu (au imeghafiliwa na watu). Muislamu anapoidhihirisha kwa watu, hupata thawabu kama za atakayetenda kitendo hicho. Lakini haimaanishi kuzusha jambo kwa maana, kanzisha kitendo kipya. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) kakataza kuzusha jambo akasema: “Kila uzushi ni upotofu”, na Wanavyuoni wote wanakubaliana   kuhusu maneno ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) wala hawapingani kuhusu hukumu hii.

Kwa hiyo, ilivyokusudiwa katika Hadiyth ni kuihuisha Sunnah na kuidhihirisha kwa watu; mfano, mtu mwenye elimu kutokea katika nchi ambayo hakuna mafunzo ya Qur-aan au hakuna mafunzo ya Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) kisha yeye akayarudisha mafunzo hayo kwa kuwawekea walimu wafundishe mafunzo ya Qur-aan na Sunnah.  

Mfano mwingine, ni mtu kukuta katika nchi watu wanayoa  ndevu zao au wanazikata, kisha yeye akaamrisha wazifuge na wasinyoe. Hivyo basi atakuwa ameihuisha Sunnah hii tukufu katika nchi hiyo ambayo watu walikuwa hawaijui au imeachwa mpaka ikasahulika. Atapata thawabu sawa na thawabu za watakaojaaliwa kupata Uongofu wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  naye akawa ni sababu. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) amesema:

(( قصوا الشوارب وأعفوا اللحى وخالفوا المشركين)) متفق على

 ((Kateni masharubu na acheni ndevu, muwe tofauti na washirikina)) Hadiyth hii imesimuliwa na Al-Bukhaariy na Muslim kutoka kwa Ibn 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhumaa)  

Juu ya hivyo, pindi watu wakiona kwamba mwalimu mwenyewe kafuga ndevu, kisha wakamfuata, mwalimu huyo huwa pia amehuisha Sunnah hiyo kwao. Na kufuga ndevu ni Sunnah ya kuwajibika wala haifai kuiacha kwa sababu ya maamrisho yaliyomo katika Hadiyth iliyotajwa hapo juu.  Basi yeye kufuga ndevu ikawa ni kigezo kwa watu atapata thawabu sawa na thawabu za atakeyemuiga kufuga ndevu. 

Mfano mwenginei ni kukuta katika nchi fulani watu hawaswali Swalah ya Ijumaa kwa sababu ya kutokujua kwao (umuhimu wake), kisha yeye akawafundisha na kuwaswalisha, basi atapata thawabu na thawabu zao pia. Au pia kukuta watu katika nchi nyingine ambao hawatambui Swalaah ya Witr, akawafundisha kisha nao wakamfuata. Na mifano kadhaa kama hiyo kuhusu ibaada au amali njema zinazojulikana na kukubalika katika Shariy’ah (hukumu) ya Kiislamu, akazidhihirisha baada ya kuwa hazikutambulika kwao au zimesahaulika au hazifuatwi na watu.

Hivyo, atakayezifufua Sunnah hizo, akazidhihirisha na kuzieneza ndiye yule aliyekusudiwa katika Hadiyth kuwa 'kafanya kitendo kizuri (Sunnatun-hasanah) katika Uislamu  kwa maana; ameidhihirisha kwa watu, basi huyo mtu ndiye  atakayekuwa miongoni mwa wale walokusudiwa katika kauli: ((atakayetenda kitendo kizuri  (Sunnatun-hasanah) katika Uislamu))

Lakini haimaanishi kwamba aanzishe (azushe) jambo katika Dini lisiloamrishwa na Allaah.  Kwani uzushi ni upotofu kutokana na kauli ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) katika Hadiyth Swahiyh,

(( وأياكم ومحدثات الأمور فإن كل محدثة بدعة وكل بدعة ضلالة))

((Tahadharini na mambo ya uzushi kwani kila uzushi ni bid'ah na kila bid'ah ni upotofu))

Vile vile Mtume ((Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) amesema katika Hadiyth Swahiyh:

(( من عمل عملاً ليس عليه أمرنا فهو رد)) البخاري

((Atakayetenda kitendo kisichokuwa chetu basi kitarudishwa.)) Al Bukhari.

Na katika kauli nyingine,

( من أحدث في أمرنا هذا ما ليس منه فهو رد) متفق عليه.

((Atakayezusha katika mambo yasiyokuwa yetu basi (kitendo hicho) kitarudishwa)) Al-Bukhaariy na  Muslim. 

Na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) alikuwa akisema katika khutba za Ijumaa:

((أما بعد فإن خير الحديث كتاب الله وخير الهدى هدى محمد صلى الله عليـه وسلم وشر الأمور محدثاتها وكل بدعة ضلالة)) خرجه مسلم في صحيحه

((Amma ba'ad. Hakika lililokuwa bora kabisa la kuhadithia ni Kitabu cha Allaah, na Uongofu ulio bora ni Uongofu wa Muhammad ((Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) na jambo ovu kabisa ni uzushi wake na kila uzushi ni upotofu)) Muslim katika Swahiyh yake. 

Kwa hiyo ibaada yoyote isiyotokana na Allaah, haifai (kuifundisha) kuilingania, na atakayeifundisha hapati thawabu bali atakuwa anaeneza bid'ah kwa watu na huyo atakayeileta (kwa kuitangaza na kuieneza kwa watu) atakuwa ni katika yule anayeongoza katika upotofu na Allaah (Subhaana wa Ta'ala) Amemlaumu na kumhoji huyo mtu mwenye kutenda hivyo kwa kauli Yake: 

أَمْ لَهُمْ شُرَكَاءُ شَرَعُوا لَهُم مِّنَ الدِّينِ مَا لَمْ يَأْذَن بِهِ اللَّـهُ ۚ

((Je, wanao washirika waliowaamuru Dini yale ambayo Allaah Hakuyatolea kwayo idhini? …)) [Ash Shuwraa: 21]  

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share