Mume Hamtimizii Haki Yake Ya Tendo La Ndoa Japokuwa Wanalala Kitanda Kimoja, Hana Masikilizano Naye

SWALI:

 

ASALAM ALEYKUM; NDUGU ZANGU WAISLAMU:

MIMI NI MAM WA MTOTO MMOJA SASA NIMEOLEWA MIAKA MINNE SASA; TANGU NIJIFUNGU HADI SASA MTOTO WANGU ANA MIAKA MITATU (3) hadi sasa mimi na mume wangu hatuonani kimapenzi tunaishi pamoja na tunalala kitanda kimoja. Kwa kweli ninasikitika sana  sababu ninapomuuliza huwa ananipa sababu kila aina, mara hataki mtoto wa 2 mara amechoka, mara anashida nyingi, mara anakuja na mipira eti tuwe tunatumia ili tusipate mtoto mwengine lakini pia hataki kufanya mapenzi. Tumekaa sasa mda wa miaka mitatu na nusu hakuna kati yetu. Kwa kweli nimejaribu kuvumilia hadi sasa nimeshindwa naomba talaka pia kwa sababu hatuna amani tangu tuoane pia kila siku ni fujo na kelele na matusi nimejaribu vyote hadi sijafaulu naomba munisaidi na   Wasaalam aleykum.

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu mumeo kutokutimizia haki yako ya tendo la ndoa.

Kwanza tunakupongeza sana kwa subira yako iliyo kubwa kwa muda wote huo. Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akulipe malipo makubwa hapa duniani na Kesho Akhera kwa hilo huku tukikunasihi ufanye subira kwa muda mwengine mdogo ili kukamilisha uvumilivu wako. Allaah Aliyetukuka Anatuambia:

Kwa hakika pamoja na uzito upo wepesi” (Al-Inshiraah [94]: 5).

 

Katika muda huo sema kwa mfano, miezi minne au zaidi kidogo unaweza kufanya juhudi tena katika kufanya yafuatayo kwani huenda mumeo akaweza kubadilika. Mambo yenyewe ni:

 

1.     Tafuta wakati muafaka wa kuzungumza na mumeo kuhusiana na shida aliyonayo – ya kutotaka kufanya mapenzi nawe mbali na kuwa kuhusiana na kutotaka kupata mtoto ni suala ambalo mnaweza kuzungumza kwa makini. Wakati huo unapoupata, utakuwa ni wakati wa faragha baina yenu ambapo mtakuwa mnazungumza mambo tofauti na hilo litakuwa ni mojawapo. Jaribu katika mazungumzo yako kuwa makini, usiwe ni mwenye hasira bali mcheshi ili aone ni jambo tu la kawaida la kutakiana kheri na mema. Huenda suala hilo akalipokea kwa njia nzuri au kinyume chake. Ikiwa hatalipokea hilo basi kuwa makini vile vile wala usikasirike kwani kukasirika kwako ni kumpatia nguvu mumeo pamoja na Shaytwaan.

 

 

Njia hiyo ikishindikana basi tafuta njia ya pili ya kumpatia vitabu vinavyohusiana na namna wanandoa wanatakiwa waishi katika muono na msimamo wa Kiislamu. Mfano ni Adabu za Ndoa na kitabu hicho unaweza kukipata katika Alhidaaya au mawaidha yanayohusiana na mafundisho ya Uislamu kuhusiana na hilo. Na mawaidha hayo pia unaweza kuyapata katika tovuti ya Alhidaaya.

 

Vitabu hivi hapa vitawasaidia:

 

Zawadi Kwa Wanandoa

 

Adabu Za Ndoa Katika Sunnah Iliyotakasika (Aadabu Az-Zafaaf Fiy As-Sunnat Al-Mutwahharah)

 

Na video hizi pia:

JUMA AMIYR - Chumba Cha Ndani Cha Mtume - 1

JUMA AMIYR - Chumba Cha Ndani Cha Mtume - 2

 

 

 

2.     Tunawaombea muafaka katika kutatua tatizo hilo mlilonalo.

 

 

3.     Ikiwa njia hiyo ya pili pia umeitumia bila ya mafanikio itabidi uitishe kikao baina yako, mumeo, wazazi au wawakilishi wa mumeo na wale wako. Katika kikao hicho inabidi uelezee tatizo wazi wazi ili upatikane ufumbuzi wa tatizo hilo. Ikiwa kweli Niyah yenu nyote wawili ni kutaka suluhisho Allaah Aliyetukuka Atawatolea njia ya kupatikana kwa masikilizano baina yenu.

 

 

4.     Ikiwa njia hiyo ya hapo juu pia haikupatikana itabidi suala hilo mlipeleke kwa Qaadhi ambaye atawasikiliza na kutoa uamuzi muafaka kulingana na Uislamu. Hapo kwa sababu ya tatizo hilo alilo nalo mumeo atakuwa ni mwenye kulazimishwa kukutimizia haja zako za kimwili na ikiwa atashindwa basi Qaadhi huyo huyo atakuwa ni mwenye uwezo wa kuivunja ndoa hiyo.

 

Mara nyingi wanandoa huingia katika Sunnah hii kubwa bila kujua wajibu na haki zao, hivyo kuleta tatizo kubwa baina yao wanapokuwa ni wenye kuishi pamoja. Mume kutoweza kumtimizia mkewe haja zake za kimwili ni sababu tosha kwa mke huyo kuomba talaka kupitia kwa Qaadhi au mume mwenyewe anapoona labda hajiwezi akampatia talaka mkewe au akajaribu kutafuta ushauri wa Kidini kuhusiana na tatizo hilo au matibabu kwani mara nyingine huenda ikawa ni ugonjwa.

 

 

Tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo  zaidi:

 

 

Ikiwa Hawaridhiani Katika Kitendo Cha Ndoa Wafanye Nini?

 

 

Mume Au Mke Hawezi Tendo La Ndoa Kwa Zaidi Ya Miaka 5, Hukmu Ni Nini?

 

Mume Hamtoshelezei Matamanio Yake Ya Tendo La Ndoa, Anaomba Ushauri

 

Mume Kahama Chumba Kwa Miezi 3 Hafanyi Tendo La Ndoa, Akiulizwa Anasema Anachoka Kazini

 

Sina Raha Na Maisha Ya Ndoa Mume Hana Hamu Na Mimi Wala Hanishughulikii

 

Tunawaombea muafaka katika kutatua tatizo hilo mlilonalo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share