Mfano Wa Nabii Ismaa’iyl (‘Alayhis Salaam) Unafaa Kuigwa Katika Kutaliki Mke?

SWALI:

 

Assalam alaykhum ndugu zangu wa alhidaaya, Ninahitaji ufafanuzi juu ya suala hili; Je? ni sunnah kwetu tuwe tunawatariki wake zetu tunapokuwa na shida, dhiki, au karaka zinapotufika kwa muda mrefu kama alivyofanya Ismaiyl kutokana na maagizo ya baba yake, Ibrahiym hanifa .au kutokana na mke wa Ismaiyl hakuonyesha uvumilivu juu ya khali waliyokuwa nayo?


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu yaliyotokea baina Nabii Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) na mwanawe Ismaa’iyl (‘Alayhis Salaam) na agizo la baba kwa mama amtaliki mkewe. Hakika hili ni swali ambazo wengi wanatatizika nalo kwa sababu ya amri ya baba pasi na kuangalia suala hilo kwa kina.

 

Sote twaelewa kuwa Nabii Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) alikuwa ni Mtume tena miongoni mwa wateule miongoni mwa Mitume. Alikuwa pia yeye ni mtume aliyekuwa na azma kubwa sana. Tawafahamu kuwa Mitume yote haiwi ni yenye kutekeleza jambo pasi na muongozo na maelekezo kutoka kwa Allaah Aliyetukuka. Kwa hiyo agizo hilo lilikuwa haswa kwa tukio hilo la baba kwa mtoto wake ambaye pia alipatiwa Utume.

 

Tukio kama hilo lilitokea wakati wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pale ‘Umar al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipomuagizia mtoto wake, ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) amwache mkewe. Na mtoto alipokwenda kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumuuliza hilo akaambiwa amuache. Hii yote ni kumaanisha agizo linalotoka kutoka kwa Mtume yeyote ni wahyi kutoka kwa Allaah Aliyetukuka.

 

Ama sisi tumeagiziwa tuishi na wake zetu kwa wema na inapotokea tatizo basi tutafute ufumbuzi kwani unaweza kumchukia mkeo kwa ila au kasoro moja lakini upande mwengine akawa ana kheri nyingi sana. Kwa hiyo tunatakiwa tuwavumilie wake zetu kwa kiasi kikubwa sana mpaka iwe hakuna budi ila kutoa talaka.

 

Ama mzazi akikushauri au kukuamrisha wewe kumuacha mkeo kwa sababu za msingi za kishari’ah basi hakuna ubaya wala kizuizi cha kuwatii kwa hilo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

  

 

Share