Mke Havai Hijaab, Anaweza Kumtaliki?

SWALI:

  

 

Unaweza kumpa talaka mke wako kama hataki kujitandiya?

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu mke asiyevaa hijaab.

Hakika hili ni tatizo kwa wanandoa kuingia katika ndoa bila ya kujua au kufahamu wanataka nini. Mke huyu ambaye umemuoa bila shaka alikuwa havai hijaab nawe ukamchagua kuwa mshirika wako katika maisha. Na kwa ajili ya hiyo ni muhali kwake kubadilika mara moja. Hivyo, inatakiwa uwe na subira na uvumilivu pamoja na kumnasihi awe anashika msimamo wa kujisitiri.

 

Huenda mke wako huyo akawa ana mambo mengine mema na mazuri na huenda akabadilika kwa hilo pia.

Allaah Aliyetukuka Anasema:

Na kaeni nao kwa wema, na ikiwa mmewachukia, basi huenda mkakichukia kitu, na Allaah Ametia kheri nyingi ndani yake” (an-Nisaa’ 4: 19). Tunakuomba uwe mpole kwake, mpe mawaidha matamu, mnunulie vitabu vya Dini pamoja na kanda za mawaidha na huenda akabadilika utakavyo kwa wakati huu kulingana na misimamo ya Kidini. Na bila shaka ukitia bidii hiyo Allaah Aliyetukuka Atakutilia tawfiki.

 

Ikiwa umetekeleza hilo kwa muda kwa mwaka au ule uliojipangia naye hajabadilika itabidi umuache na wakati huo ukitaka kuoa lazima utazame sifa zilizowekwa na Uislamu katika kuchagua mwenzio wa maisha.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share