Wazazi Hawataki Mtu Kutoka Bara Amuoe Binti Yao Mpemba

SWALI:

 

Assalam Alaykum, mungu awajaze kheri na awabariki ninyi pamoja nasi ili tuwe miogoni mwa wenye kufaulu hapa duniani na huko akhera Inshaallah. Rafiki yangu (mtanzania bara) anataka kuoa binti wa kipemba kutoka maafia anayeishi Dar es salaam lakini wazazi wa binti hawataki binti yao aolewe na mswahili. Je afanyeje?

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu kwa swali lako kuhusu wazazi kutokubali binti yao kuolewa na mvulana wa bara.

Ndugu yetu umetueleza habari za upande mmoja bila ya kutueleza mambo ya upande wa pili. Ni vigumu kwetu tulio mbali kuweza kutatua matatizo ya mbali kama hayo lakini twaweza kutoa nasaha jinsi ya kuweza kutatua tatizo hilo. Na nasaha tulizo nazo InshaAllaah tunazitoa kwa ndugu zetu popote walipo.

 

Mwanzo kabisa ifahamike kuwa Uislamu ni Dini inayowaweka wanaadamu kuwa sawa sawa bila ubaguzi wa kitaifa, kikabila, kirangi, kilugha na mengineyo. Tofauti inakuja kwa Imani na Taqwa (ucha Mungu).

Allaah Aliyetukuka Anasema:

Enyi watu! Hakika Sisi Tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na Tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Allaah ni huyo aliye mcha Mungu zaidi katika nyinyi” (al-Hujuraat 49: 13).

 

Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

Hakuna ubora wa Muarabu kwa asiyekuwa Muarabu, wala mweupe juu ya mweusi ... isipokuwa kwa taqwa”.

Ndio kwa minajili hiyo Maquraysh wa kike walikuwa wanaolewa na hata waacha huru Waislamu abao walikuwa wanaonekana ni duni kabla ya kuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Nasi tunatakiwa tuige Sunnah hiyo ya kipenzi chetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Kwa mujibu wa swali inasemekana kuwa wazazi wa msichana wamekataa. Ikiwa wazazi wamekataa kwa sababu mvulana hajashika Dini au hana maadili mema basi wazazi watakuwa na haki katika shari’ah kukataa. Ikiwa wamekataa kwa sababu ya ukabila tu basi mvulana atakuwa na nguvu ya kuifikisha kesi yake mbele kama tutakavyotaja njia na taratibu hapa chini.

 

Njia ambazo mnatakiwa kuzifuata ni mwanzo kuyakinisha kuwa kweli msichana anataka kuolewa na huyo mvulana. Ikiwa msichana kweli anataka kuolewa basi fuateni taratibu zifuatazo kwa huyo rafiki yako kuzifuata:

 

1.     Aswali Swalaah ya Istikhaarah kumuomba Allaah Aliyetukuka ikiwa ni kheri kwake Amsahilishie na ikiwa ni shari Amuepushie.

 

2.     Atume wazazi wake kwenda rasmi kwa wazazi wa msichana kupeleka posa.

 

 

3.     Ikiwa imeshindikana atume wazee wengine waende kuzungumza na wazee wa msichana kwa njia ya ulaini, upole na kwa hekima.

 

4.     Ikiwa imeshindikana basi atume Mashaykh wenye busara na elimu kwenda kuzungumza na wazazi wa msichana.

 

5.     Ikiwa imeshindikana aachane na msichana huyo na atafute mwengine ambaye atakuwa na kheri naye kwani kumuoa huyo mbali na kwamba shari’ah inaruhusu ni kuingia katika matatizo na mivutano na wazazi wake ambao hawalitaki jambo hilo. Na hakuna haja wala maana ya kuja baadaye kutokuwa na maelewano au kuvunjika uhusiano wa binti na wazazi wake kwa sababu yako na hali kuna wasichana wengi wema wanaosubiri kuolewa na wanaoweza kumkubali kijana kama yeye pamoja na ubara wake na uswahili wake ambao anabaguliwa nao.

 

Kadhalika patumwe Mashaykh wa kuweza kuwanasihi hao wazazi wa binti huyo na wawaelimisha kuhusu ubaya na uchafu wa jambo hilo la ubaguzi wa kikabila na kitaifa na wawafahamishe kuwa hayo ni mambo ya kijahiliyah ambayo Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyaita kuwa ni ‘uvundo’.

 

Na ikiwezekana watoleshewe makala ifuatayo hapa chini na wapelekewe:

 

Utaifa Au Uislam?

 

Twamuomba Allaah Aliyetukuka Awafanyie lenye kheri na Awaepushie lenye shari.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share