Madhara Ya Ghiybah (Kusengenya) 2-Ulimi Ni Kufaulu Kwako Au Kuangamia Kwako
05- Swafar 1428 - 23-02-2007
Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ameuhifadhi Ulimi ndani ya mdomo, ili usiwe wazi kila mara ukanena maneno mengi ambayo huenda yakamuangamiza binaadamu kwa kumuharibia amali zake, au kukosa radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) japo kwa neno moja tu ovu kama anavyosema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
عن أبي عبد الرحمن بلال بن الحارث المزني رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: ((إن الرجل ليتكلم بالكلمة من رضوان الله تعالى ما كان يظن أن تبلغ ما بلغت يكتب الله له بها رضوانه إلى يوم يلقاه، وإن الرجل ليتكلم بالكلمة من سخط الله ما كان يظن أن تبلغ ما بلغت يكتب الله له بها سخطه إلى يوم يلقاه)). رواه مالك في الموطأ والترمذي وقال حديث حسن صحيح.
Abu 'Abdir-Rahmaan Bilaal bin Al-Haarith Al-Muzniy (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema: "Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Kwa hakika mja atazungumza neno linalomridhisha Allaah, wala asidhani kuwa litafikia lilipofikia, Allaah Amuandikie kwa neno hilo Radhi Zake hadi Siku ya Qiyaamah. Na Kwa hakika mja atazungumza neno linalomkasirisha Allaah, wala asidhani kuwa litafikia lilipofikia, Allaah Amuandikie kwa neno hilo hasira Zake hadi Siku ya Qiyaamah)) [Maalik katika Muwattwa na At-Tirmidhiy ambaye amesema Hadiyth hii ni Hasan Swahiyh]
Kutokana na Hadiyth hii, tunapata funzo kwamba, ulimi unaweza kuwa ni kiungo kizuri kabisa katika mwili wa binaadamu na unaweza kuwa ni kiungo kiovu kabisa vile vile.
Kisa kifuatacho cha Mzee Luqmaan kinatuthibitishia funzo hili:
Ibn Jariyr amenuku kwamba Khaalid ar-Rabaai alisema: "Luqmaan alikuwa mtumwa wa Kiethiopia aliyekuwa na ujuzi wa useremala. Bwana (Tajiri) wake alimwambia: "Tuchinjie kondoo huyu" Akamchinja, kisha akamwambia: "Niletee viungo viwili vilivyokuwa ni bora kabisa". Akampelekea ulimi na moyo. Baada ya siku kupita, alimtaka tena amchinjie kondoo, akachinja kisha Bwana wake akamwambia tena: "Niletee viungo viwili vilivyokuwa ni viovu kabisa". Akameletea vile vile ulimi na moyo. Bwana wake akamuuliza: "Nilipokutaka uniletee viungo bora kabisa umeniletea ulimi na moyo; na nilipokutaka uniletee viungo viovu kabisa umeniletea hivyo hivyo" Luqmaan akamwambia: "Hakuna vilivyo bora kuliko hivi vinapokuwa vizuri, na hakuna vilivyo viovu kabisa kuliko hivi vinapokuwa vibaya" [At-Twabariy: 20:135]
- Ulimi ni kipande kidogo cha nyama kisichokuwa na mifupa lakini kinaweza kumvunja mtu mifupa yake siku ya Qiyaamah.
- Ulimi ni kama nyoka itakayomtia sumu binaadamu, au ni kama mkuki utakaomuangamiza binaadamu siku ya Qiyaamah
- Hivyo hivyo, ulimi huenda ukawa ni sababu ya kumuingiza mtu Peponi japo kama hakuwa na vitendo vyema vingi.
- Ulimi ni kiungo kikuu katika mwili wa binaadamu kinachodhibiti viungo vingine vyote vya mwili wa binaadamu.
عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ رَفَعَهُ قَالَ : قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: (( إِذَا أَصْبَحَ ابْنُ آدَمَ ، فَإِنَّ الْأَعْضَاءَ كُلَّهَا تُكَفِّرُ اللِّسَانَ ، فَتَقُولُ : اتَّقِ اللَّهَ فِينَا ، فَإِنَّمَا نَحْنُ بِكَ ، فَإِنِ اسْتَقَمْتَ اسْتَقَمْنَا ، وَإِنِ اعْوَجَجْتَ اعْوَجَجْنَا)) أخرجه الترمذي وأحمد وابن خزيمة والبيهقي بسند حسن. رياض الصالحين
Kutoka kwa Abu Sa'iydil-Khudriyy (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Anapoamka binaadamu viungo vyote vinaulaumu Ulimi vikisema: Mche Allaah kwetu, kwani sisi tuko katika hifadhi yako; ukiimarika nasi tutaimarika, ukienda pogo, nasi tutakwenda pogo)) [At-Tirmidhiy, Ahmad, Ibn Khuzaymah, Al-Bayhaqiy ikiwa ni sanad hasan. Riyaadhwus-Swaalihiyn]
Ni bora kuzuia ulimi usitoke tu kuzungumza maneno yoyote ila kwa kuhitajika, kwani kuuachia ulimi mradi tu uzungumze utampeleka mtu kutoa porojo na kuzungumza yasiyofaa na kumharibia mja Akhera yake.
************
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


