Madhara Ya Ghiybah (Kusengenya) 7 - Vipi Kujiokoa Na Kuokoa Jamii Kutokana na Ghiybah
25 Rabiy'ul Awwal 1428 -
13-04-2007Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
((وَإِذَا رَأَيْتَ الَّذِينَ يَخُوضُونَ فِي آيَاتِنَا فَأَعْرِضْ عَنْهُمْ حَتَّى يَخُوضُواْ فِي حَدِيثٍ غَيْرِهِ وَإِمَّا يُنسِيَنَّكَ الشَّيْطَانُ فَلاَ تَقْعُدْ بَعْدَ الذِّكْرَى مَعَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ))
((Na unapowaona wanaoziingilia Aayah zetu, basi jitenge nao mpaka waingilie mazungumzo mengine. Na kama Shaytwaan akikusahaulisha, basi baada ya kutanabahi usikae pamoja na watu madhaalimu)) [Al-An'aam: 68]
Hiyo ni moja ya njia ya kujiokoa na maovu haya ya Ghiybah, nayo ni kujiepusha na wanaopendelea kuzungumza yasiyo na maana na yanayomkosesha mtu radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala). Njia nyingine nyingi tunazitaja chini ya Makala hii na inayofuatia.
Njia za kujiokoa na kuwaokoa wenzako na Ghiybah:
1. Kuwa na Taqwa na umkhofu Mola Wako na kusoma Aayah na Hadiyth zenye maonyo na adhabu za Ghiybah.
2. Fikiria khasara utakayopata kumalizikiwa amali zako njema zote na kujazwa madhambi badala yake kama inavyosema Hadiyth ifuatayo:
عن أبي هريرة رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال)) أتدرون ما المفلس قالوا المفلس فينا يا رسول الله من لا درهم له ولا متاع قال رسول الله صلى الله عليه وسلم المفلس من أمتي من يأتي يوم القيامة بصلاته وصيامه وزكاته ويأتي قد شتم هذا وقذف هذا وأكل مال هذا وسفك دم هذا وضرب هذا فيقعد فيقتص هذا من حسناته وهذا من حسناته فإن فنيت حسناته قبل أن يقتص ما عليه من الخطايا أخذ من خطاياهم فطرح عليه ثم طرح في النار)) ألترمذي
Imetoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mnamjua nani aliyefilisika?)) Wakasema (Maswahaba): Aliyefilisika ni yule miongoni mwetu asiyekuwa na Dirham au mali. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Aliyefilisika katika Ummah wangu ni yule atakayekuja siku ya Qiyaamah na Swalah zake, Swawm zake na Zakaah zake, lakini atakuja akiwa amemtukana huyu, amemtuhumu huyu, amekula mali ya huyu, amemwaga damu ya huyu na amempiga huyu, yatachukuliwa mema yake na kulipwa wale aliowadhulumu. Yatakapomalizika mema yake kabla ya kufidia madhambi aliyowakosea wenzake, zitachukuliwa dhambi za wale aliowakosea kisha atajaziwa yeye na mwishowe atakuwa ni wa kutupwa motoni)) [At-Tirmidhiy]
3. Fikiria aibu zako au aibu za ndugu, jamaa zako na uwaze kama utapenda aibu hizo zenu zidhihirike kwa wengine.
4. Mshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa kukuepusha na aibu kama za wenzako na muombe Asikupe mtihani wa aibu kama hizo au nyinginezo.
5. Jiepushe na watu waovu na vikao viovu na andamana na watu wema ambao watakuwa na mazungumzo ya kukupa faida badala ya kukuangamiza.
6. Atakapokupigia simu mwenzio kutaka kusengenya, aidha muelezee wazi kuwa hutaki tena kusikia umbeya kwani unamkhofu Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala), na umnasihi naye pia aache maouvu hayo kwa kumkumbusha adhabu zake. Anapokuanzia mfano, "Je umesikia habari ya fulani?" Mjibu: "Sijasikia na wala sitaki kusikia, tafadhali tuzungumze mengine".
7. Ikiwa huwezi kumuambia wazi wazi ingawa ni bora zaidi kufanya hivyo, basi kila anapotaka kumsengenya mtu, mfano anapokupigia simu jifanye una kazi na huna muda. Fanya hivyo siku ya kwanza, ya pili, ya tatu, endelea hatimaye atafahamu kuwa kumbe hutaki Ghiybah. Au anapokuanzia, babaisha kwa kumpa mazuri uliyojifunza ya dini, au maudhui yoyote nyingine ya kheri.
8. Jipe adhabu mwenyewe kila unapomsengenya mtu kama walivyokuwa wakifanya Salafus-Swaalih (wema waliotangulia);
-Funga Swawm ya siku moja kila unapomsengenya mtu, hatimaye utashindwa kukaa na njaa kila siku.
-Toa kiasi fulani cha pesa kila unapomsengenya mtu iwe ni sadaka, utakapojiona unafilikisha utaacha kusengenya.
9. Hifadhi ulimi wako usizungumze ila mema tu, jifunze pole pole hata kwa kujikumbusha, mfano uweke kitu mdomoni kama kijiwe au chembe ngumu isiyotafunika ili ibakie kukukumbusha kuzuia ulimi kusema yasiyo na maana.
10. Jiepushe na moto pindi utakapolinda heshima ya mwenzio, kumbuka Hadiyth ifuatayo:
عن أبي الدرداء رضي الله عنه عن النبي صلى الله عليه وسلم قال: ((من رد عرض أخيه رد الله عليه وجهه
من النار يوم القيامة)) رواه الترمذي وحسنه
Abu Ad-Dardaa (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema: (Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayetetea heshima ya nduguye (Muislamu), Allaah Atamuepusha uso wake na moto)) [At-Trimidhiy na amesema Hadiyth hii ni Hasan]
11. Utakaposikia uzushi au mtu atakapomsengenya mwenziwe mbele yako sema kama Anavyotufunza Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) katika kisa cha 'ifk'- uzushi wa kusingiziwa Mama wa Waumimi Bibi 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha):
Kwanza: Jifikirie nafsi yako kama wewe pia unaweza kufanya maovu hayo yanayozungumzwa? Kwa hiyo dhana nzuri iwe pia kwa Waumini wenzako.
((لَوْلَا إِذْ سَمِعْتُمُوهُ ظَنَّ الْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بِأَنفُسِهِمْ خَيْرًا وَقَالُوا هَذَا إِفْكٌ مُّبِينٌ))
((Kwa nini mliposikia khabari hii, wanaume Waumini na wanawake Waumini hawakuwadhania wenzao mema, na kusema: Huu ni uzushi dhaahiri?)) [An-Nuur: 12]
Pili: Kanusha kabisa uliyoyasikia nachukulia hayo kuwa ni uzushi na Mtukuze Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
((وَلَوْلَا إِذْ سَمِعْتُمُوهُ قُلْتُم مَّا يَكُونُ لَنَا أَن نَّتَكَلَّمَ بِهَذَا سُبْحَانَكَ هَذَا بُهْتَانٌ عَظِيمٌ))
((Na kwa nini mlipoyasikia msiseme: Haitufalii kuzungumza haya. Subhaanak Umetakasika! Huu ni uzushi mkubwa!)) [An-Nuur: 16]
************
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


