Skip navigation.
Home kabah

Fadhila Za Qiyaamul-Layl - 1 (Kusimama Kuswali Usiku)

 

 




Amesema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

   

 

((من قام رمضان إيماناً واحتساباً غفر له ما تقدم من ذنبه))  متفق عليه

 

((Atakayesimama (Kuswali) Ramadhaan kwa imaani na kutaraji malipo, ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Amesema Al-Haafidh ibn Rajab, "Tambua kuwa Muumini anajumuisha katika mwezi wa Ramadhaan jihaad mbili kwa ajili ya nafsi yake.  Jihaad ya mchana ya kufunga, na jihaad ya usiku kwa kusimama (kuswali), atakayejumuisha jihaad hizi mbili atapata ujira wake bila ya hesabu".

 

Amesema Ibn 'Uthaymiyn "Haimpasi Muislamu kuepukana na Swalah ya Tarawiyh katika Ramadhaan ili apate thawabu na ujira wake, na wala asiondoke mpaka Imaam amalize pamoja na Swalah ya Witr ili apate ujira wa Qiyaamul-Layl yote".

 

Ili kuipata ladha ya Ramadhaan na kuongeza Utiifu na Imaan ni muhimu Muislamu ajumuike na Waislamu wenzie kuswali Tarawiyh na kusikiliza Tilaawat ya Qur'aan inaposomwa katika Swalah hizi kupata utulivu wa moyo na nafsi na pia kujichumia thawabu tukufu zinazopatikana katika kisimamo hiki na kufutiwa madhambi yake kama tulivyoona kwenye hadiyth iliyopita.

 

 

KWA NINI MUISLAM ASWALI QIYAAMUL-LAYL?

 

 

Zifuatazo ni sababu ambazo zinampasa Muislamu azizingatie na afanye hima kuswali Swalah ya Qiyaamul-layl ili aweze kupata fadhila njema za kumfanya awe Muumini bora kabisa:

 

 

1-QIYAAMUL-LAYL NI AMRI KUTOKA KWA ALLAAH (Subhaanahu wa Ta'ala) 

 

}}يآ أَيُّهَا الْمُزَّمِّلُ{{  }} قُمِ اللَّيْلَ إِلَّا قَلِيلًا{{  }} نِصْفَهُ أَوِ انقُصْ مِنْهُ قَلِيلًا{{   }} أَوْ زِدْ عَلَيْهِ وَرَتِّلِ الْقُرْآنَ تَرْتِيلًا {{

 

{{Ewe uliyejifunika}} {{Kesha usiku kucha, ila kidogo tu!}} {{Nusu yake, au ipunguze kidogo}} {{Au izidishe - na soma Qur-aan kwa utaratibu na utungo}}[Al-Muzammil: 1-4]

 

 

}}أَقِمِ الصَّلاَةَ لِدُلُوكِ الشَّمْسِ إِلَى غَسَقِ اللَّيْلِ وَقُرْآنَ الْفَجْرِ إِنَّ قُرْآنَ الْفَجْرِ كَانَ مَشْهُودًا{{

 }} وَمِنَ اللَّيْلِ فَتَهَجَّدْ بِهِ نَافِلَةً لَّكَ عَسَى أَن يَبْعَثَكَ رَبُّكَ مَقَامًا مَّحْمُودًا{{

 

{{Shika Swalah jua linapopinduka mpaka giza la usiku, na Qur'ani ya alfajiri. Hakika Qu-aan ya alfajiri inashuhudiwa daima}}

{{Na amka usiku kwa ibada; ni ziada ya Sunnah khasa kwako wewe. Huenda Mola wako Mlezi Akakunyanyua cheo kinachosifika}} [Al-Israa 78-79]

 

Tahajjud ni Swalah inayoswalia baada ya kulala, tunaona katika Hadiyth mbalimbali kwamba Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alikuwa akiswali Tahajjud baada ya kulala. Nazo ni kutoka kwa Ibn Abbaas na 'Aishah. Taz.Fathul Baari 8.83 ,  3:39

 

Amesema  Mujaahid, "Qiyaam kwa haki ya Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni Naafilah (Ziada ya Sunnah) kwa sababu ameshafutiwa madhambi yake yaliotangulia na yaliyokuja.  Na kwa haki ya Umma wa Kiislamu Swalah ya  Qiyaamul-Layl huenda ikamfutia madhambi yake atakayotenda".  [At-Twabariy 17:525]

 

Na Amesema tena Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)    

 

 

}}فَاصْبِرْ عَلَى مَا يَقُولُونَ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ الْغُرُوبِ{{

}}وَمِنَ اللَّيْلِ فَسَبِّحْهُ وَأَدْبَارَ السُّجُودِ{{

 

{{Basi vumilia kwa hayo wasemayo, na mtakase kwa kumsifu Mola wako Mlezi kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuchwa}} 

{{Na katika usiku pia mtakase, na baada ya kusujudu}}. [Qaaf:39-40]

Amesema tena:

}}وَاذْكُرِ اسْمَ رَبِّكَ بُكْرَةً وَأَصِيلًا{{

 }} وَمِنَ اللَّيْلِ فَاسْجُدْ لَهُ وَسَبِّحْهُ لَيْلًا طَوِيلًا{{

 

{{Na likumbuke jina la Mola wako Mlezi asubuhi na jioni}}

{{Na usiku msujudie Yeye, na umtakase usiku, wakati  mrefu}}[Al-Insaan:25-26]

 

 

 

 

 2- KUMSHUKURU ALLAAH (Subhanaahu wa Ta'ala) 

    

 

     

Qiyaamul-Layl ni mojawapo ya njia ya kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  kwani kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  sio kwa kusema tu bali iwe shukurani ndani ya moyo na kukiri kwa ulimi na kwa viungo pia kama alivyokuwa akifanya Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

    

وعن عائشة رضي الله عنها قالت )) كان النبي يقوم من الليل حتى تتفطر قدماه. فقلت له: لِمَ تصنع هذا يا رسول الله،   وقد غُفر لك ما تقدم من ذنبك وما تأخر؟ قال: أفلا أكون عبداً شكوراً ؟ ((متفق عليه

 


 

((Imetoka kwa Bibi 'Aisha (Radhiya Allahu 'anha) kwamba Mtume   alikuwa akisimama usiku hadi ikivimba miguu yake, nikamwambia  kwa nini unafanya hivi ewe Mjumbe wa  Allaah, na hali umefutiwa madhambi yako yaliyotangulia na yatakayofuatia?  Akasema, "Nisiwe mja mwenye kushukuru?))  [Al-Bukhaariy na Muslim]

  

 

 

3- SWALAH BORA KABISA BAADA YA FARDH

 

 

         Amesema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  

 

((أفضل الصلاة بعد الفريضة صلاة الليل))  رواه مسلم.

 

((Swalah iliyo  bora kabisa baada ya Fardh ni Swalah ya usiku))  [Muslim]

 

 

 

 

4- KUFUFUA NA KUFUATA SUNNAH YA MTUME (Swalla Allahu 'alayhi wa alihi wa sallam)   NA MASWAHABA ZAKE

 

 

 

Badala ya kukesha usiku kwa mambo mengine ya kidunia yasiyo na  faida na sisi wala Akhera yetu na kupoteza umri wetu, ni bora kukesha kwa kumuelekea Mola Mtukufu kwa kufuata Sunnah za kipenzi chetu Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  na Maswahaba zake.

 

 

 

 

5- KUBADLISHA HALI ZIWE KAMA ZA SALAF SWAALIH (WEMA WALIOPITA)  

 

 

Ni mwendo wa Salaf Swaalih ambao uliendelea  hadi kutufikia sisi adabu ya kutekeleza Swalah hii ambayo ni mojawapo wa nyenzo bora kabisa kuzidisha imani zetu, kusafisha nyoyo zetu, kupata utulivu  na kupata Ridhaa ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) 

 

 

 

 

6- KUJIKURUBISHA NA ALLAH  (Subhanaahu wa Ta'ala)

 

 

((وعن عمرو بن عبسة رضي الله عنه أنه سمع النبي  صلى الله عليه وسلم  يقول: أقرب ما يكون الرب من العبد   في جوف الليل الآخر فإن استطعت أن تكون ممن يذكر الله تعالى  في تلك الساعة فك))رواه الترمذي وأبو داود

. 

((Imetoka kwa 'Amru bin 'Abasah (Radhiya Allahu 'anhu) kwamba kamsikia Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)    akisema: ((Wakati Allaah Anakuwa karibu kabisa na mja, ni wakati wa mwisho wa usiku, kwa hiyo ukiweza kuwa miongoni mwa wanaomkumbuka Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)   katika saa hiyo basi uwe)) [At-Tirmidhy na Abu Dawuud].  

 

 

   

7- KUJIKINGA NA UCHAFU WA SHAYTWAAN

 

 

 

ذكر عند النبي رجل نام ليلة حتى أصبح فقال:  ))ذاك رجل بال الشيطان في أذنيه    ((متفق عليه

 

 

 

Alielezwa Nabii kuwa kuna mtu alilala usiku wote hadi asubuhi bila kuswali, Akasema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((huyo ni mtu aliyekojolewa na Shaytwaan katika masikio yake)) [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

 

 

 

Inaendelea....../2