Zingatio: Hajuti Mwenye Kumshauri Allaah

 

Zingatio: Hajuti Mwenye Kumshauri Allaah

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Je unataka kuanzisha biashara yako mpya? Je unahitaji kuchagua mwenza wako wa maisha ya ndoa? Je unahitaji elimu gani uisome itakayokuletea manufaa duniani na Akhera? Je unahitaji kununua nyumba au ardhi? Je unataka kuchukua yatima na kumlea katika khayr?

 

Bila ya shaka yoyote, tulio wengi au tuseme wote katika Waislamu, ni wenye kukumbana na moja kati ya masuala hayo yaliyopo juu, ambayo hapana wasiwasi wowote kwamba yanahitaji majibu, jibu ambalo ni vyema kwanza ukapata ushauri, wala hakuna ushauri ulio bora kabisa kwa Muislamu kuliko ule unaotoka kwa Rabb Mlezi wa Mbingu na Ardhi.

 

Ukweli ni kwamba binaadamu ni mwingi wa harakati aliyejawa na matarajio mengi sio hapa duniani tu bali hata, kwa wengine, pale anapofariki. Wengi ya wanaadamu hawalengi bila ya shaka yoyote, kupata hasara hapa duniani wala Akhera. Ndio katika mitihani hii na njia ipi ya kuifuata, Rabb Akafungua mlango Wake wa ushauri. Ushauri ambao sio wa binaadamu wala wa mganga, ni ule wa siri kabisa baina ya mja na Rabb wake. Hiyo nafasi ambayo kila mwanaadamu na hasa Muislamu anahitajika kuielewa, kuitumia na kunufaika nayo.

 

Rabb Ametuhakikishia kwamba Yeye yupo karibu nasi, naye Anajibu du’aa zetu pale tunapomuomba:

 

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ ۖ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ ﴿١٨٦﴾

Na watakapokuuliza waja Wangu kuhusu Mimi, basi Mimi ni Niko karibu (kwa ujuzi); Naitikia du’aa ya muombaji anaponiomba. Basi waniitikie Mimi na waniamini Mimi, wapate kuongoka. [Al-Baqarah: 186]

 

Cha muhimu na cha kuzingatia katika aayah tuliyoinukuu hapo juu ni kumuamini Rabb kwa haki Anayostahiki kuaminiwa. Bila ya kutimiza sharti hili, ushauri utakaohitaji utakuwa ni sawa na kujaza maji kwenye pakacha

 

Katika matatizo mengi anayokutana nayo hapa duniani, basi Allaah Yupo wa kuyapatia ufumbuzi, na hasa pale inapotakikana jibu la moja kwa moja. Nayo ni njia ya kumtaka ushauri Allaah kwa kuswali rakaa mbili za istikhaarah. Hii ni Swalah  inayopendezeshwa kuswaliwa usiku, lakini yawezekana kuswaliwa nyakati nyengine yoyote.

 

Kilicho muhimu katika hapa ni kujikubalisha kwa Rabb kwamba Yeye ndiye anayesikia maombi na vilio vyetu. Yeye ndiye anayeelewa matatizo yetu yote, wala hakuna kubwa litakalomshinda Allaah kukupatia ushauri na ufumbuzi.

 

Hii ni nafasi adhimu kabisa, kwani hata kama halikutendeka lile unalolitaka, na hali ya kuwa ulimtaka ushauri Allaah kupitia njia hii, basi hutakuwa ni mwenye kujuta. Hii ni kwasababu ya kujikubalisha kwako kwamba lililokuwa ni kwa matakwa ya Rabb na lililoshindikana nalo pia limekosekana kwa kukubali kwake Rabb.

 

Muislamu hana haja ya kuwa depressed ‘kujilaumu kwa fikra kupita mpaka’ hadi akawa sawa na chizi. Dunia yetu hii Rabb ndiye Anayeielewa juu chini, chini juu. Yeye ndiye Aliyejaalia kuwepo kheri na shari. Ni juu yetu sisi Waislamu kukubali kwamba kalamu imeshamaliza kuandika yote yatakayojiri duniani, kwetu sisi ni kukubali tu matokeo bila ya kujuta.

 

Share