Kitangulizi
MATARI NA FIRIMBI ni ngoma zilizoanza huko Arabuni kabla ya kuja Uislamu. waarabu walikuwa wakistarehesha kwa ngoma hizo katika tarabu zao na pumbao lao, katika maarusi, makilabu na mikutano ya ulevi na pumbao. Na sikuzote waliokuwa wakipiga matari walikuwa ni wanawake, vijakazi au watoto wa kike, kama zinavyoonesha Hadithi tutakazozitaja.
Ulipokuja Uislamu yaliuhusiwa matari kwa ajili ya kutangaza arusi kama utakvyoona. Kwa bahati mbaya baadhi ya Waislamu waliitumia vibaya ruhusa hiyo hata matari yakafanywa ni namna ya ibada, yakapigwa ndani ya miskiti, na katika kuzuru maiti; na yakaongezwa na firimbi na vigoma ili mdundo uzidi kuwa mtamu!
Katika miji yetu matari yalianza kutumiwa katika ngoma za arusi kama tari-la-ndia, diriji n.k. Kisha yakatumiwa katika ngoma za pepo na gungu; na baadae yakatumiwa katika maulidi. (Na hivi karibuni kumezuka tapo la Wakristo wanaojiita “Waisraili” ambao wanatumia TARI katika ibada zao).
Huko Lamu, na baadhi ya miji ya Pwani, wanavyuoni walipinga kwa nguvu wakati matari yalipoambukizwa katika misikiti lakini waliosimama kuwatetea hao wenye kuhalalisha jambo hilo walikuwa na nguvu kuliko wenye kupinga. Ndipo wenye kupinga waliposhindwa kuyazuia, na wengine wakakhitari kugura na kutoka Lamu. Ama nje ya Lamu, kama Mombasa na Zanzibar, karibu mashekhe wote waliokuwako zama hizo, kama Sayyid Ahmed bin Sumeyt, Sheikh Abdalla Bakathir, Sheikh Mohamed bin Kassim, Maamiry, Sheikh Suleman bin Aly Al-Mazrui na mashekhe wote wa Takaungu na wengineo katika wanavyuoni wakubwa wakubwa wote walipinga kwa nguvu khasa kupigwa ndani ya msikiti!
Pengine wanaonijua wataniuliza: -
a) “Walioanza kutumia ngoma hizi katika maulidi na ibada ni babu zako masharifu wa Hadhramout, huoni vibaya kupingana na wazee wako?”
Na pengine watauliza: -
b) “Wewe si mwanachuoni yakuhusu nini mambo haya?”
Jawabu yangu ni hii: -
a) Sisi tumeamrishwa kuwafuata wazee katika yanayofaa kufuatwa tu. Huko Akhera hakuna mzee atakayemuokoa mwanawe, wala hakuna mwana atakayemwokoa mzee wake. Na Mwenyezi Mungu Ametuamrisha yukubali makosa ijapokuwa tunayafanya sisi wenyewe. Na zaidi ya hayo inafaa tufahamu kuwa wazee walikuwa na mema mengi ya kuwafinikia mabaya yao ambayo sisi hatuna.
b) Kusema la sawa ni wajibu wa kila Muislamu. Si kazi ya wanazuoni peke yao. Na mimi ijapokuwa si mwanachuoni. Laini nimekaa nao, nimehudhuria daraa zao, na nimezungumza nao kwa uhuru kamili, na hata nimejadiliana nao katika mambo ya mishikili ya dini. Sikutukiwa a mishikili nikaogopa kumuuliza mwanachuoni. Na mpaka leo huo ndio mwendo wangu. Kwa hivyo ikiwa simo katika kumbo la wanavyuoni, sitoki katika kumbo la “MTEGEMEA NUNDU HAWATI KUNONA”.
Wassalaam
Shariff Abdalla Salim El-Husseiny
- Login or register to post comments
- Email this page


