Zingatio: Mutashitakiana Wenyewe Kwa Wenyewe

 

Zingatio: Mutashitakiana Wenyewe Kwa Wenyewe

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Hicho ndicho kizaazaa cha Siku ya Qiyaamah, siku ambayo sio tu kwamba mwanaadamu atashtakiwa na Rabb wake, bali pia atapata mashtaka kutoka kwa wanaadamu wenziwe. Basi nakuusia kuchunga haki za watu na zaidi kwa Waislamu wenzio.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anatuambia ndani ya Qur-aan tukufu:

 

ثُمَّ إِنَّكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ عِندَ رَبِّكُمْ تَخْتَصِمُونَ ﴿٣١﴾

Kisha hakika nyinyi Siku ya Qiyaamah mtakhasimiana mbele ya Rabb wenu. [Az-Zumar: 31]

 

Rabb wetu (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ni Kariym, Mwenye kuisimamisha haki na wala sio Mwenye kumdhulumu mja Wake. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Aliyetukuka katika Hadiyth Al-Qudsiy Anasema: “Enyi waja Wangu! Mimi Nimejiharamishia dhuluma juu ya Nafsi Yangu na nikaifanya ni haramu baina yenu basi musidhulumiane.” [Imepokewa na Muslim]

 

Yale masharti aliyoyatoa Sayyidna Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) wakati wa khutbah yake ya kukabidhiwa ukhalifa, ndiyo yale yale ambayo Atayasimamia Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa upana na kwa haki isiyopungua hata chembe ya khardal. Sayyidna Abu Bakr alisema: “Wadhaifu miongoni mwenu watapata nguvu mpaka nitakapowapoka haki zao; ambao watu wenye nguvu miongoni mwenu ni dhaifu kwangu mpaka nitakapowapoka haki yao, Allaah Akipenda.”

 

Kwa kila tendo tunalofanya, ni vyema tukajichunga kwani mara nyingi huwa ni lenye kumuathiri mwanaadamu mwengine. Iwapo unajenga nyumba ukaengeza ghorofa, jirani yako ana haki ya kupata upepo, na ni wajibu kumuomba ruhusa kabla ya kunyanyua nyumba yako.

 

Kwa yule msengenyaji, aelewe kwamba msengenywaji atakuja siku ya Qiyaamah akiwa na njaa ya kuzipata thawabu za mtu kwa kila hali anayoijua. Wala hataiwacha fursa hii muhimu kwani atakushtakia mbele ya Muumba na malipo yake ni wewe kuchukuliwa thawabu zako na kupatiwa yeye, iwapo thawabu zako zimeisha, basi yatachukuliwa madhambi yake na kupatiwa msengenyaji.

 

Anasema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Mnajua muflis? Wakasema (watu): “Muflis kwetu sisi ni yule miongoni mwetu asiyekuwa na dirhamu (pesa) wala vyenye kumnufaisha yeye hapa duniani”. Akasema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Hakika muflis katika Ummah wangu ni yule atakayekuja Siku ya Qiyaamah na Swalah, Funga na Zakaah, lakini amemtusi huyu, kumsingizia huyu mwingine kuwa amezini, amekula mali ya huyu, amemwaga damu ya mwingine na kumpiga mwengine. Thawabu zake zitapatiwa huyu na yule mpaka zimalizike. Na zinapokwisha basi madhambi ya hao (aliowadhulumu) atabandikwa nayo, hivyo kuingizwa Motoni.” [Imepokewa na Muslim]

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) hifadhi Yake, Atuongoze njia ya haki tuione na kuweza kuifuata, na kwa baatwil tuigundue na tuweze kuiacha.

 

 

Share