Mjadala Wa Mwandamo Wa Mwezi
Vijana wa Salafiyya - Dar-es-salaam
KWA NINI TUNATOFAUTIANA KATIKA KUFUNGA?
Tunamshukuru Allah (Subhaanahu wa Ta'ala), Swala na amani juu ya Mtume wetu Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Aali zake Maswahaba zake, na ba’ad, huu ni mtazamo kwa ufupi jinsi ya kuingiya kwa mwezi wa Ramadhaan na kufunga na kutoka kwa mwezi wa Ramadhaan na kufunguliya.
Ndugu Muislamu mas-ala ya mwandamo wa mwezi yameleta mijadala na mipasuko mikubwa miongoni mwetu Waislamu kila mmoja anajaribu kuleta hoja zake kuhalalisha mitazamo yake namna ya kufunga wengine wanasema kufunga ni mwezi ukionekana popote pale ulimwenguni wengine wanasema kila nchi ina machimbuko yake ya mwezi. InshaAllah katika makala hayo uliyo nayo mbele yako hivi sasa tutajaribu kukaguwa hoja za pande zote mbili ili nyinyi wenyewe Waislamu mjionee haki iko wapi bila kujiingiza katika ushabiki usiyo na maana yoyote. Tafadhali soma kwa makini hoja zote ili uchukuwe maamuzi mwenyewe.
Wapendwa Waislamu, mas-ala ya kufunga na kufunguwa yametundikwa kwa kuonekana mwezi haturuhusiwi waislamu kufunga na kufunguwa mpaka uonekane mwezi au tukamilishe siku 30. Na huu mwezi una kazi kubwa sana na manufaa mengi katika maisha ya mwanadamu miyongoni mwa manufaa ni hili suwala la kutekeleza Ibada na funga ya mwezi wa Ramadhaan na kuna manufaa mengine mengi lakini hatuwezi kuelezeya manufaa yote hayo kwa kuwa siyo dhumuni letu.
(Ndiye Anayepambazuwa asubuhi na Ameufanya usiku kuwa mapumziko na jua na mwezi kwenda kwa hesabu…) Qur-aan 6:96.
Ushahidi juu ya aya hii kuwa mwezisayari umeumbwa kwa ajili ya mahesabu. Kasema tena:
(Yeye Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyelifanya jua kuwa mwanga na mwezi kuwa nuru na akaupimia vituo (huwo mwezi) ili mjue Idadi ya miaka na hesabu (nyinginezo)…) Qur-aan 10:5
Hapa tunapata wazi kuwa mwezisayari una vituo na madhumuni ya kuumbwa kwake tupate kujuwa idadi ya miaka kwa kupitia hesabu za kila mwezi siku kwa kuonekana kwa huo mwezisayari. Kasema tena Mwenyeezi Mungu:
(Na mwezi kadhalika ni alama kwao tumeupimiya vituo (hiki baada ya hiki) mpaka unakuwa (mwembamba)
Hapa vile vile Mwenyeezi Mungu Anatuelezeya kuwa mwezisayari una vituo na hivyo vituo ndiyo Idadi ya hesabu ya masiku yetu. Na kasema tena:
(Na jua na mwezi (huenda) kwa hesabu (yake)).Qur-aan 55:5
Hapa vile vile tunapata kuwa huu mwezisayari hutembea katika vituo vyake alivyovipangilia Mwenyezi Mungu. Kasema tena:
(Na kwa mwezi unapokamilika) Qur-aan 84:18
Hapa Mwenyezi Mungu Anaapa kwa mwezisayari unapokamilika, kwa hiyo hapa kuna dalili ya wazi kuwa mwezisayari unakuwa mdogo mpaka unakamilika na halafu unarudi kuwa mdogo Kasema tena Mwenyezi Mungu:
(Na kwa mwezi unapoliandama) Qur-aan 91:2.
Hapa vilevile Mwenyezi Mungu Anaapa kwa mwezisayari unapoandama unapokamilisha mahesabu ya vituo vyake na kuanza upya. Ndugu Muislaam sasa tuvitazame vituo vya mwezisayari je kuna vituo vingapi?
Majina ya vituo 10 vya mwezisayari
Ndugu Muislam mwezisayari una vituo 10 katika mwezi mzima kama Alivyosema Mwenyezi Mungu:
(…Na mwezi kuwa nuru na akaupimiya vituo….)
na vituo vyote kwa lugha ya kiarabu kila kituo kina jina lake, tukianza kituo 1-3 kinaitwa Ghurar, kituo 4-6 kinaitwa Nuqal, kituo cha 7-9, kinaitwa Tus’u, na kituo 10-12 ‘Ushru, kituo 13-15, kinaitwa Albiidh, kituo 16-18 Dur’u kituo cha 19-21 kinaitwa Dhulum, kituo 22-24 kinaitwa Hinas, kituo 25-27 kinaitwa Daadi na kituo cha mwisho 28-30 kinaitwa Muhaq.
Ndugu Muisilam hizi ndizo aya na vituo zenye kuonesha sisi tuzingatiye sana hesabu za siku zetu kwa kutumiya mwezi sayari ili tupate Idadi na hesabu ya siku tunazozihitaji na vilevile tumepata fundisho lingine kuwa hapa Mwenyezi Mungu Ameumba mwezi mmoja tu si zaidi ya mmoja kwa hiyo utakapoandama popote pale ndipo hesabu zake zinapoanza na kuelekea katika vituo vyake kama Yeye Mwenyewe Alivyosema kuwa Ameumba mwezisayari na Akaumba vituo vyake. Kutokana na mafundisho haya hatudhani kuwa mwezisayari utakapo onekana nchi ya mbali na nchi nyingine haikuuona kuwa eti vituo na hesabu zitatofautiana. Kwa Mfano nchi hiyo iliyouona mwezisayari itakuwa tarehe moja kwao na nchi ya pili itakuwa wao bado wapo tarehe 29 au 30. Hili ni muhali halitewezekana kamwe katika maumbile ya Mwenyezi Mungu ama katika mafundisho yake ya Qur-aan kama tulivyoona aya za nyuma.
Nini maana ya saumu
Kilugha saumu ni kujizuiya na kutenda kitu ambacho unaweza kukitenda au kujitowa katika hali fulani na ukajiweka katika hali nyingine, na mtu kiziwi anaitwa kwa kiarabu ”Assam” na anaambiwa aliyenyamaza “saum” kwa kuwa kajizuiya na kuongeya kama pale ilipotwambiya Qur-aan:
(…sema hakika mimi nimeweka nadhiri kwa Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma ya kufunga, kwa hiyo leo sitasema na mtu) Qur-aan 19:26
Kisheriya saumu ni kujizuiya Muisilam kula na kunywa na kumuingiliya mkeo kuanziya alfajir inapotoka mpaka jua linopozama na hiyo saumu itatimia na kukamilika kama imeepukana na mambo yaliyoharamishwa.
Lini ilifaradhishwa hii saum ya Ramadhaan?
Saumu ya Ramadhan ilifaradhishwa tarehe 15 Shaaban mwaka wa 2 Hijiriya, na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe katika maisha yake kafunga Ramadhan 9 kauona mwezi kwa macho yake mara 2 kaletewa habari za mwezi mara 3 toka Madina na mara 4 toka nje, na akawa amefariki mwezi Rabii’ul awwal mwaka 11 Hijiriya.
Dalili ya kufaradhishwa Mwezi wa Ramadhan
Saumu ya Ramadhaan imefaradhishwa kutoka ndani ya Qur-aan na Sunnah sahihi ya Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Kasema Mwenyezi Mungu:
(Enyi mlioamini mmelazimishwa kufunga saum)
Na katika Sunnah kasema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) {Uislam umejengeka katika nguzo tano kushuhudia ya kwamba hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mungu mmoja tu ambaye ni Allah na Muhammad ni Mtume wa Allah na kusimamisha sala (tano ), na kutoa zaka, na kufunga saum ya Ramadhaan, na kwenda kuhiji kwa mwenye uwezo wa kwenda} Al-Bukhaariy
Tunathibitisha vipi kuingiya kwa mwezi wa Ramadhaan?
Kuingiya mwezi wa Ramadhaan kunathibitishwa kwa njia 6 kuu.
1] Kuona mwezisayari mtu peke yake itamlazimu nafsi yake afunge
2] Wakiona mwezisayari watu wengi itawalazimu watu wote wafunge
3] Wakiuona mwezisayari watu wachache na wakamueleza Kiongozi wa Kiislam itawalazimu watu wote wafunge
4] Akiona mwezisayari mtu mmoja na akatoa habari kwa wengine katika eneo lina kiongozi wa Kiislam itawalazimu watu wote wafunge
5] Akiona mwezisayari mtu mmoja na akatoa habari katika eneo lenye Kiongozi wa Kiislam lakini hashughulikii mambo ya Waislam itawalazimu watu wote wafunge
6] Kuelekea katika mji ambao umeonekana kwao mwezisayari, tazama kitabu cha “At- Talkhiys” kasema Imam Ibn Hajar.
Dalili za kufunga Ramadhaan kwa kuonekana mwezisayari popote pale duniyani
Waislam watawajibika kufunga Ramadhaan kama utaonekana mwezisayari popote pale duniyani maadamu tu uonekane huo mwezisayari na Muislam hata kama aliyeuona ni mtu mmoja pasina kuweka kiwango cha masafa fulani, au kwenda kiwango cha kutofautiyana machomozo ya mwezisayari, haya yote hayana dalili ndani ya mafundisho ya Qur-aan na Sunnah na hata Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliyefaradhishiwa hii funga alipokuwa akiletewa taarifa ya kuonekana mwezisayari hakuwauliza waliomleteya habari hizo kuwa wanatokeya umbali gani au machomozo ya mwezi wao vipi, alikuwa akitosheka na ile taarifa ya kuonekana huo mwezisayari. Wala hayakupatikana mafundisho kutoka kwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaambiya Waislam eti kila nchi ina muandamo wake.
Wakati wa uhai wake nchi ya Yemen na Sham zilishaingiya Uislam na maeneo mengine mbalimbali uliingia Uislam, hatukuona wala kusikia eti walikuwa wanatafutiana kufunga kama utakavyokuja kuona mafundisho ya Mtume hapo mbele, na kama hawakuuona mwezisayari au hawakupata taarifa alikuwa akikamilisha Shaabani siku 30, haya ndiyo mafundisho ya Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Na kuna hadithi nyingi
Hapa tumeona kuwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametosheka na taarifa ya mtu mmoja wala hakumuuliza umeonekana wapi na umbali gani.
Na kutoka kwa Rabi’i ibn Harash kutoka kwa mtu mmoja miyongoni mwa Masahaba wa mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema:
{Wamekhitalifiyana watu siku moja juu ya siku ya mwisho wa Ramadhaan kuendelea kufunga au kufunguliya, wakaja mabedui wawili wakashuhudiya mbele ya Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)kuwa wameona mwezi jana jiyoni, palepale akawaamrisha Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) watu wafungulie} Ahmad na Abu Dawuud
Vile vile Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwauliza mbona sisi hatukuuona na mmetoka umbali gani au mbona machomozo yenu siyo sawa na sisi na kadhalika imekuja hadith kutoka kwa Abu Hurayra(radhiya Allahu 'anhu) Kasema Mtume: “ suumuu liruuyatihi, waaftiruu liruuyatihi’’ yaani “Fungeni kwa kuonekana kwake [mwezi] na funguweni kwa kuonekana kwake”.
Hadithi hii ni amri yenye kueneya kwa umma mzima ilipotamkwa “suumuu” tamko hili linafidisha umuum katika qaida za Usuulul fiqhi linaitwa “Al-Amru liljam’i biswighatil Jam’i” tazama kitabu Irshaadul Fuhuul uk. 121-122.
Na amesema Imam Ibn Qayyim kuwa maneno yote anayosema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni yenye kueneya kwa umma mzima madamu tu hakukusudiya kwa Fulani pekee. Tukitazama hadith hiyo anasema Mtume tufunge utakapoonekana mwezi na siyo tutakapouona sisi ndiyo tufunge na kufunguwa bali utakapoonekana na Waislamu popote pale ulimwenguni watu wafunge wala hakusema watu wa nchi Fulani wakiuona mwezi sayari haiwalazimu watu wa nchi nyingine kufunga. Kwani kama tulivyoona Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) yeye mwenyewe katika maisha yake kafunga Ramadhan 9 kauona mwezi mara 2 tu mara 7 zote kaletewa taarifa.
Hoja na majibu kwa wale wanaohalalisha kuwa kila nchi ina machimbuko yake ya mwezi
Hoja yao kubwa siyo Qur-aan wala Sunnah ya Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambavyo ndiyo dira yetu tunapokhitilafiyana kama alivyosema Allah Taa’ala katika Qur-aan “… Na kama mkikhitilafiyana juu ya jambo lolote basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, hiyo ndiyo kheri nayo ina matokeo bora kabisa” [Qur-aan 4:59]
Hoja kubwa ya wenye kuhalalisha kila nchi kuwa na mwezi wake ni moja tu nayo ni kisa cha Kuraybu mtumwa wa Ibn ‘Abbaas walipojadiliyana na Ibn ‘Abbaas mwenyewe anasema Kuraybu kuwa “Ummul Fadhli bint Harith [mama yake huyu Ibn ‘Abbaas] alinituma kwa Muawiyya katika mji wa Shamu nikafika Shamu na kutekeleza haja zake [zote] na ukaonekana mwezisayari wa mwezi wa Ramadhaan, na mimi nipo Shamu, tukauona mwezisayari usiku wa kuamkiya Ijumaa, baada ya hapo nikarudi Madina mwisho wa mwezi [wa Ramadhaan] akaniuliza Ibn ‘Abbaas, kisha akautaja mwezi akasema : lini mliuona mwezi? nikamwambiya usiku wa kuamkiya Ijumaa. Akasema kuniuliza wewe umeuona usiku wa kuamkiya Ijumaa? Nikajibu ndiyo na wameuona watu [wote] na wakafunga, na akafunga Muawiyya [piya] akasema Ibn ‘Abbaas lakini sisi tumeuona mwezi usiku wa kuamkiya Jumamosi na tutaendeleya kufunga mpaka tukamilishe siku 30, au tuuone[wenyewe], nikamwambiya [Ibn ‘Abbaas] je, hukutosheka kwa kuuona Muawiyya na kufunga kwake akajibu kwa kusema, “hivi ndivyo alivyotuamrisha Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).”
Ndugu Waislamu hii ndiyo dalili kubwa ya wenye kuhalalisha kila nchi kuwa na mwezi mwandamo wake kwa hakika hawana dalili nyingine zaidi ya kisa hiki, hebu tukichambuwe kwa undani sote ili kila mmoja wetu apate faida je kinafaa kuwa ni dalili ya kutegemeya?
Kumjadili Kuraybu na uchambuzi wa kisa hiki
Kwanza watukufu Waislam kabla hatujasogeya kwenda mbali inabidi mpate faida kumjuwa huyu Kuraybu ni nani? Hili jina la Kuraybu ni la baba yake ambaye na wanachuwoni wa hadith wanamkubali huyu baba yake kuwa alikuwa mtu mkweli sana na anategemewa katika upokezi wa hadithi tazama kitabu 'Tahdhibu' cha Imam Ibn Hajar Al ‘Asqalani [jalada la 3 uk 468 chapa ya Beirut tazama mahala pa herufi kaaf]
Na tazama vile katika Taqribu Tahdhibu cha huyu huyu Ibn Hajar Al Asqalani jalada la 2, uk 28. lakini huyu aliye katika kadhiya hii na Ibn ‘Abbaas jina lake kamili ni Muhamad Ibn Kuraybu Ibn Abi Muslim Al Hashimiy alikuwa ni mtumwa wa Ibn ‘Abbaasi na mama yake Ibn ‘Abbaasi Umul Fadhli alikuwa akimtuma sana kwenda Shamu kwa Muawiyya.
Na yeye huyu si Sahaba bali ni katika tabiin na si mtu wa kuaminika katika elimu ya hadith hakubaliki.
Hebu tuwasikilize wanachuwoni wetu wa hadith wanavyomchambuwa huyu Muhamad Bin Kuraybu.
Amesema Athram toka kwa Ahmad bin Hanbal kuwa, "Huyu Muhammad Bin Kuraybu hadith zake ni 'Munkar"
Na amesema Ad Duuriyu toka kwa Ibn Maiyn kuwa "Hadith zake huyu si chochote".
Na amesema Ibn Numair; "upokezi wake haufai kabisa ni dhaifu".
Na amesema Ibn Hatim toka kwa baba yake kuwa "Huyu Muhamad Bin Kuraybu hazitolewi hoja hadith zake".
Na amesema Abi Zur’a kuwa "Hadith zake ni laini mno".
Na amesema Imam Al Bukhaariy kuwa "Hadith zake huyu ni za kuchunguzwa sana".
Na akaendeleya kusema Imam Al Bukhaariy kuwa "Hadith zake huyu ni Munkar hazikubaliki".
Kumbuka ndugu Muislamu pindi imam Al Bukhaariy anaposema kuwa hadith za mtu Fulani ni munkar basi wanachuwoni wote wa hadith wamekubaliyana kuwa zinawekwa upande wa dhaifu.
Na amesema Imam An Nasaaiy "Huyu Muhamad Ibn Kuraybu ni dhaifu". Na vivyo amesema Imam Adaara Qutni [Tamaza Tah-dhibu Tah-dhibu ya Imam Ibn Hajar Al Asqalani jalada la 3 uk 684-685 chapa ya Beirut. Tazama mahala pa herufi mimu] piya Taqribu Tah-dhibu jalada la 2 ukurasa 86.
Na amesema Abubakar Al Athram: "Nilimuuliza Imam Ahmad Bin Hanbal kuhusiyana na hadith za huyu Muhamad Bin Kuraybu akasema 'Ni Munkar kwa sababu analeta hadith za ajabu kabisa". [tazama Al Jarhu Wataadil cha Imam Ibn Abi Hatim jalada la 8 uk.68 chapa ya India]
Na amesema Imam Ibn Hibbaan kama alivyonukuliwa katika Mizanul i’tidali ya Imam Adh Dhahabi kuwa "Huyu Muhamad bin Kuraybu alikuwa ni mudalisi [mrongo]". Na amesema Abu Na’im Ad Damishqi kuwa, "Huyu Muhammad Bin Kuraybu alikuwa anachanganya hadith sahihi na dhaifu".
Kumbuka ndugu Muislamu hakuna hata mwanachuwoni mmoja wa hadith aliyemtaja huyu Muhamad Ibn Kuraybu kuwa ni mkweli.
Baada ya kumaliza kumkaguwa huyu Kuraybu ebu sasa ndugu Muislamu tuje kukikaguwa kisa chenyewe , tukianza na qauli ya Ibn ‘Abbaas kukataa kufunguliya kwa mwezi ulioonekana katika mji wa Shamu kasema Imam Alqarafi katika kitabu cha “Adhakhira” ya kuwa, "Siku ile habari ya mwezi alipopewa Ibn ‘Abbaas kutoka kwa Kuraybu kulikuwa hakuna mawingu yaliyotandaa katika mji wa Madina, na wala haukuonekana mwezi siku hiyo, Ibn ‘Abbaas akatanguliza kuuona yeye mwezi kuliko ile habari au taarifa alioletewa na Kuraybu, na ndiyo maana akasema: “Hivi ndivyo alivyotuamrisha Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa maana tusichukuwe habari za dhana na tukaacha yakini, japokuwa hakuna tafauti ya kuutazamiya mwezi kukiwa kuna mawingu au hakuna mawingu, lakini yeye alihukumu kwa kuuona mwezi. Anasema Imam Alqarafi kuwa "Hiki kisa kishakuwa na utata mkubwa" tazama J. 2 uk 490.
Na qauli ya Ibn ‘Abbaas ya kukataa kufunguliya mwezi ulioonekana Shamu na kusema hivi ndivyo alivyotuamrisha Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na akaishiya hapo hakuendeleya na wala hakufafanuwa zaidi na kisa hiki kikaishiya hapo. Na utata ukawa mkubwa katika safu za Waislamu kutokana na kutokupatikana ufafanuzi zaidi juu ya kisa hiki.
Sasa basi tujiulize sote kwa pamoja kaamrishwa na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) nini? Wamekhitilafiyana wanazuwoni katika makundi manane juu ya hii amri anayosema Ibn ‘Abbaas kaamrishwa na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
1) Kundi la kwanza la wanazuwoni wanasema kaamrishwa na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) asifunge wala kufunguwa katika siku itakayokuwa mawingu yametanda angani wakamilishe 30 Shaabaan au 30 Ramadhaan
2) Kundi la pili wao wanasema: “Kaamrishwa na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) asipokee taarifa ya kufunga au kufunguwa kutoka kwa mtumwa kwa sababu wale wote walioleta habari ya mwezi wa kufunga au kufunguwa zama za Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) walikuwa si watumwa, na Kuraybu alikuwa ni mtumwa wa Ibn ‘Abbaas (radhiya Allahu 'anhu)
3) Kundi la tatu wao wanasema kaamrishwa na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) asipokee taarifa au habari ya mwezi kutoka kwa mtu mmoja tu mpaka apatikane mwingine mwenye kumshuhudiya huyo mtowa habari.
4) Kundi la nne wanasema kaamrishwa na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa yeyote yule atakayesafiri kutoka katika mji ambao haukuonekana mwezi na kuelekeya katika mji ambao umeonekana, basi hukumu yake atafunga pamoja na watu wa mji huo na atakuwa ni mmoja kati ya watu wa mji huwo. Kwa mujibu ya mafundisho haya ya Kuraybu, atatakiwa afunge siku 31.
5) Kundi la tano wao wamesema kaamrishwa na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) asikubali mwezi aliyouona Muawiyya kwa sababu mtazamo wake yeye Ibn 'Abbaas (radhiya Allahu 'anhu) alikuwa hautambui utawala wa Muawiyya na alisimama pamoja na Aliy bin Abi Twalibu dhidi ya Muawiyya. Kwa mafundisho haya asikubali mwezi ulioonekana na kiyongozi asiyetambulika.
6) Kundi la sita wamesema kaamrishwa na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) asikubali kufunguwa na kulipa siku badala yake ile waliokula mchana na isipokuwa kwa mashahidi wawili kwa hilo kuhofiya kuwalipisha watu funga ya siku moja iliyowapita kutokana na taarifa ya mtu mmoja.
7) Kundi la saba wanasema kaamrishwa na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kila nchi ina machomozo ya mwezisayari wake na masafa yake, na masafa yanayokusudiwa ni KM 133.056.
QAULI YA MADHEHEBU MANNE JUU YA QADHIYA HII
Ndugu Muislamu kuna madai ya uwongo kabisa yaliyozoeleka midomoni mwa baadhi ya ndugu zetu kuwa eti wanazuwoni wengi wamesema kila nchi ifunge kwa machomozo ya mwezi wake wasitegemee machomozo ya wenzao. Qauli hii si sahihi kabisa. Kwa kweli mwenye kueneza qauli ya namna hii hana uaminifu katika elimu kwani anaeneza qauli ya upande mmoja ambao ambao ndiyo mtazamo wake yeye na anaficha huja za upande mwingine. Tafadhali mpendwa Muislamu ebu soma kwa makini tunataja misimamo ya madhehebu manne na wewe mwenyewe pima kwa akili yako bila matamaniyo ya nafsi au ushabiki je wanazuwoni wengi wapi wameegemeya:
a) Tukianza na wanazuwoni wa ki-Hanafi wao wanasema: "Kutafautiyana kwa machomozo ya mwezi haizingatiwi katika madhehebu yetu, na ndiyo wanazuwoni wengi walikwenda hivi, na hii ndiyo fatwa yetu, inawalazimu watu mashariki kufunga kwa kuonekana mwezi na watu wa Magharibi kama itathibiti kwao wameuona huo mwezi, kwa njiya za kisheriya".
b)Wanazuwoni wa Ki-Maliki wao wanasema: "Utakapoonekana mwezi, itaeneya uwajibu wa kufunga nchi zote, iwe nchi hiyo ya karibu au mbali, wala haizingatiwi katika hilo umbali wa masafa, na vile vile haitazingatiwa kuwafikiya machomozo au kutafautiyana machomozo, wajibu kufunga kila atakaeletewa taarifa ya kuonekana mwezi wawe walioleta taarifa hiyo, mashahidi wawili au watu wachache au hata watu wengi."
c) Wanazuwoni wa Ki-Hanbali wao wamesema "Iitakapothibiti kuonekana kwa mwezi sehemu Fulani, iwe karibu au mbali, italazimu watu wote wafunge, na hukumu ya wasiouona ni hukumu ya waliouona".
d) Wanazuwoni wa Ki-Shafi’i wao wamesema: "Utakapoonekana mwezi katika mji itawalazimu hukumu ya kufunga watu wa mji wa karibu si watu wa mbali kwa kadiri ya tafauti yao ya machomozo ya mwezi, na tafauti ya machomozo kati ya sehemu moja na nyingine isipunguwe chini ya Farsakh 24 sawa sawa na kama Kilometa 133.056".
Kwa maana hiyo nchi kama ya Tanzaniya ina mikoa 26 na kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine haiupunguwi chini ya Kilometa 200 kama tutafuwata madhehebu haya ya Kishafi’i itabidi katika mikoa 26 kila mkoa utakuwa na funga yake. Kwa mfano Dar es salaam kwenda Morogoro ni Kilometa 198 hawa watakuwa wamevuka kiwango cha kufunga pamoja kwa kipimo cha madhehebu ya Kishafi’i ambacho ni Kilometa 133.056, kwa maana hiyo Morogoro wao watafunga pamoja na watu wa Kibaha kwa kuwa masafa kati ya Morogoro na Kibaha ni Kilometa 148 takriban. Sasa je ndugu Muislamu hili linawezekana na linaingiya akilini? Mpendwa Muislamu tumiya akili yako kujadili hoja hizo maana wewe mwenyewe ndiye utaulizwa kesho akhera na si sheikh Fulani au Imamu fulani.
Wabillah Tawfiiq Waswalallahu ala Muhammad waala ali Muhamad
Kama una hoja yoyote au maswali basi tuandikie:
Vijana wa Salafiyah
Lukwati @yahoo.co.uk
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha
