Mke Kukutana Na Mume Baada Ya Eda

SWALI:

Je inaruhusiwa mume akishamtaliki mkewe talaka moja kukutana nae ilikutafuta njia ya maelewano hata kama eda imekwisha?na je inaruhusiwa mke huyo kujipamba ili apate kumvutia mumewe katika hali yakutafuta maelewano?

 


 

 

JIBU: 

 

 

 Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum)  na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Ndio mke anaruhusiwa kukutana na mtalaka wake baada ya Idda ya talaka ya kwanza kumalizika. Bali ni jambo zuri kutafuta maslahi na kupatana, lakini mkutano huu haufai kuwa wa faragha yaani wao wawili peke yao, kwa sababu wao sasa ni ajnabi kama ajnabi mwengine yeyote. Kwani Mtume Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam amesema:   “Mwanamume asikae na mwanamke faragha isipokuwa kuwe na mahrimu yake”)) (al-Bukhari kutoka kwa Ibn ‘Abbaas Radhiya Allaahu 'anhumaa)

Maalik amesema, “Mwanamke wakati mwengine hula na mumewe na watu wengine wanaokula na mumewe au na kaka zake kwa njia hiyo hiyo. Lakini haifai kabisa kwa mwanamke kuwa peke yake na mwanamume ambaye hana uhusiano wa kidamu, kindoa au kunyonya pamoja kitu ambacho kitamfanya mwanamume asiweze kumuoa kisheria". Amesema Mtume Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam:  “Hakutani mwanamume na mwanamke peke yao isipokuwa shetani ni watatu wao”)) (at-Tirmidhy kutoka kwa ‘Umar bin al-Khatwaab Radhiya Allaahu 'anhu. Katika riwaya nyengine imeongeza: ((“Naye (shetani) hutembea katika mwili wa binadamu kama damu”)).

Zipo njia ambazo mwanmke anaweza kuzitumia kisheria ili kupata upatishi huo baada ya Iddah kama kumtuma kaka yeke au babake au mamake na watu wengine katika jamaa zake kuwa ndio wasitah baina yake na mtalaka wake. Si hilo tu bali baba anaweza kumtafutia mume bintiye kama alivyofanya ‘Umar Radhiya Allaahu 'anhu baada ya mume wa bintiye Hafswa kufariki na Iddah kumalizika alikwenda kwa Abubakr na baadae ‘Uthman Radhiya Allaahu 'anhu ili wamuoe binti yake.

Kujipamba inatakiwa kabla ya idda kumalizika, ama ikimalizika hairuhusiwi tena kwa sababu kama ambavyo mapambo hayaruhusiwi yaonekane na ajnabi mwengine yoyote

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share