Je, Mtu Anaweza Kutuma Pesa Akachinjiwe Nje Ya Nchi Aliyoko? Na Wakati Gani Kuchinjwe?

 

SWALI:

Assalaam aleikum warahmatullahi wabarakatuhu. Allah atawajaza kila la kheri kwa kutuilimisha zaidi, amin! Swali langu ni:- Unaruhusiwa kutuma pesa nyumbani ukachinjiwa ama ni lazima uchinje nchi ile unapoishi? Jazak Allah kheir

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

 

Tunashukuru kwa swali lako.


Mtu anapaswa achinje pale alipo ikiwa hakuna makatazo ya sheria za nchi ya kuchinjia pale alipo kama ilivyo hali katika baadhi ya nchi za Ulaya. Lakini ikishindikana mtu kuchinja pale alipo, basi hakuna makatazo kutuma pesa akachinjiwa nchi nyingine.

Na kumbuka, ukiwa umeweka Niyyah ya kuchinja kabla mwezi wa Dhul-Hijjah haujaingia, basi unatakiwa ujizuie kukata kucha na nywele za aina zote mwilini hadi siku ya tarehe 10 Dhul-Hijjah ambapo mtu utakapokuwa umeshaswali Swalah ya 'Iyd na ukwajulisha wale wenye kuchinja, wakuchinjie wakati huo. Si  wao wachinje wakishamaliza Swalah ya 'Iyd huko kwao, bali ni wewe utakapomaliza Swalah ya 'Iyd hapo ulipo kwani wewe ndiye mwenye kuweka Niyyah ya kuchinja na wewe ndiye uliyejizuia kukata kucha zako na nywele zako hadi kuchinjwe.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share