Tathmini Mwezi Wako Wa Ramadhaan

Mkusanyaji: Abu Faatwimah

 

Kila sifa njema inamstahikia Allaah Aliyetukuka Muumba wa ulimwengu na walimwengu wake, ambae Alituwafikisha kuukamilisha mwezi wa Ramadhaan kwa kufunga Swawm yake nyakati za mchana, kusimama visimamo nyakati za usiku, kuisoma Qur-aan iliyoteremsha ndani yake na kutekeleza kila tulilowafikishwa kulitekeleza kadiri ya uwezo wetu.

 

Swalah na Salamu zimfikie kipenzi cha Waumini Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Sahaba zake kiraam (Radhiya Allaahu 'anhum) na kila anaewafuata kwa ihsaan mpaka Siku ya Mwisho.

Masiku ya Ramadhaan yaliyotunukiwa kila aina ya neema na baraka ndio yamekwishapita mpito wa usiku na mchana, na ndio hivyo hivyo unavyopita umri wetu, leo tuko hai juu ya ardhi na kesho wafu ndani yake.

Ndugu yangu katika iymaan, umemaliza Swawm ya Ramadhaan na yote yaliyoambatana na Ramadhaan, mambo ambayo utekelezaji wake ulitarajiwa uwe wenye Ikhlaasw: kwamba hapakusudiwi katika utekelezaji wa hicho kinachotekelezwa chochote kile isipokuwa Wajhi wa Allaah; na Al Mutaaba’ah: kwamba hicho kinachotekelezwa kinaendana na Sunnah; kwa kufuata na kuuigiza mafundisho ya Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwamba katika utekelezaji wa hiyo amali kunafuatwa vile alivyotekeleza au amrisha, au fundisha, au elekeza, au fafanua, au idhinisha Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Ndugu yangu katika iymaan, yote uliyoyatekelza ni siri baina yako na Mola wako Ar-Rahmaan, ulikuwa mja mwenye moyo safi, uliojaa huruma, mwenye nafsi iliyojitenga na kujiweka mbali umbali wa mbingu na ardhi na kila aina ya machafu na kila chenye kukatazwa, ulikuwa mwenye nafsi iliyojaa hamasa na pupa ikitekeleza kila iliyowafikishwa katika yenye kukurubisha waja kwa Allaah na yenye kumridhisha.

Ndugu yangu katika iymaan, sasa Ramadhaan ndio imekwishatuaga kwa kutuambia: “Nawaacha katika Amana ya Allaah Ambaye Kwake hakupotei amana”. Nini tumefanya au tunatarajiwa kukifanya baada ya kupokea au kusikia matamshi hayo kutoka kwa Ramadhaan?

Ndugu yangu katika iymaan, waraka huu unajaribu kukuzinduwa na kukushauri kuwa uwe na desturi ya kujitathmini na kutathmini utekelezaji wako baada ya kuwafikishwa kutekeleza ulichokitekeleza; tathmini ambayo itakusaidia kufikia kuelewa ubora wa ulichotekeleza, athari ilizoziacha katika nafsi yako na manufaa uliyonufaika au kinyume chake; jambo litalokupeleka kufikiria kujuta na kurudi kwa Mola wako mrudio wa kweli kweli.

Ndugu yangu katika iymaan, kwa kuwa umeshauaga mwezi wa Ramadhaan, mwezi wa baraka na rehma, umeziaga siku zake za mchana ukiwa katika Swawm, na siku zake za usiku ukiwa katika visimamo, umeuaga mwezi wa Qur-aan, umeuaga mwezi wa Taqwa, umeuaga mwezi wa Maghfirah na mwezi wa kutolewa watu kwenye Moto wa Jahannam, mwezi unaowekwa wazi milango yote ya Jannah; hivyo ni vizuri na ndio ilivyo hasa ujitathmini na utathmini kile ulichokikadimisha kwa kuangalia kama uliweza kufikia daraja ya kufaulu.

Ndugu yangu katika iymaan, sote tunamuelewa aliyefaulu, ni yule aliyetekeleza ibadah ya Swawm ilivyopaswa kutekelezwa na kutakabaliwa Swawm yake; aliyefaulu ni yule aliyechuma mema mengi na akajitahidi katika kuchuma mema kwenye mwezi wa Ramadhaan; aliyefaulu ni yule aliyeweza kufikia kughufuriliwa madhambi yake yote na kukubaliwa tawbah yake; aliyefaulu ni yule aliye epushwa na kuwekwa mbali na Moto wa Jahannam; Allaah Anasema:

Kila nafsi itaonja mauti. Na hakika mtalipwa kikamilifu ujira wenu Siku ya Qiyaamah. Basi atakayewekwa mbali na Moto na akaingizwa Jannah kwa yakini amefuzu” [Aal –‘Imraan 3: 185].

Ndugu yangu katika iymaan, hapa nitapendekeza baadhi ya maswali ya kujiuliza nafsi yangu na yako kama ni tathmini kwa kile tulichowafikishwa kukitekeleza, tathmini ambayo lengo lake kuu ni kuweza kufikia kuwa na kawaida ya kujitathmini kwa kila tunachotekeleza na kuweza kufikia kujihisabu wenyewe kabla hatujahesabiwa na Mola; basi natuingie katika tathmini yetu:

 

SWAWM

Allaah Anasema:

“Enyi mlioamini! Mmeandikiwa Swawm kama iliyoandikwa kwa wale ambao wa kabla yenu mpate kuwa na taqwa” [Al-Baqarah: 183].

Ndugu yangu katika iymaan ulifunga; vipi ilikuwa hali yako wakati ukiwa kwenye Swawm?

A.     Amesema Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) “Kila amali –njema- ya mwanaadamu inalipwa mara kumi na inaongezewa thawabu kutoka kumi hadi mia saba; Allaah Akasema: “Isipokuwa Swawm, kwani hiyo ni kwa ajili Yangu na Mimi Ndiye Nitakayemlipa; ameacha matamanio yake na chakula chake na maji yake kwa ajili Yangu. Kwa aliyefunga atapata furaha mbili; furaha anapofuturu na furaha atakapoonana na Mola wake, harufu inayotoka kinywani mwa aliyefunga ni nzuri mbele ya Allaah kuliko harufu ya misk” Imepokelewa na Muslim, kitabu cha Swawm, mlango wa fadhila ya Swawm, Hadiyth namba 1949 na 1956].

B.     Amesema Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) “Asiyeacha kusema uongo (maneno mabaya, kusengenya, kufitinisha, kutoa ushahidi wa uongo- na vitendo vibaya); basi ajue kuwa Allaah hana haja na Swawm yake katika kuacha chakula chake na kinywaji chake” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha Swawm, mlango wa asiye acha kutoa ushahidi wa uongo na kuufanyia kazi, Hadiyth namba 1780; na Muslim katika kitabu cha Swawm, mlango wa Kuhifadhi ulimi kwa Mfungaji, Hadiyth namba 1948].

C.    Amesema Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) “Mwenye kufunga Ramadhaan na akaielewa mipaka yake –Ramadhaan- na akajihifadhi na yale yenye kutakiwa kujihifadhi nayo, husamehewa yaliyokuwa kabla ya Ramadhaan” [Imepokelewa na Ibn Hibbaan, kitabu cha Swawm, mlango wa fadhila za Ramadhaan, Hadiyth namba 3515].

D.    Amesema Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:“Mwenye kufunga Ramadhaan kwa iymaani na akatarajia malipo atasamehewa madhambi yake aliyoyatanguliza” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha Swawm, mlango wa mwenye kufunga Ramadhaan kwa iymaan na ihtisaab, Hadiyth namba 1778].

Ndugu yangu katika iymaan; baada ya kumaliza kutathmini hali yako uliyokuwa nayo wakati wa Swawm, hebu sasa tathmini daraja ya Swawm yako?

A.     Swawm yangu ilihusisha kujizuilia kula, kunywa na matamanio pekee na wala sikuhisi badiliko lolote lile lenye kuonyesha kuwa kuna tofauti baina ya siku ninayokuwa na Swawm na siku nyingine za kawaida.

B.      Swawm yangu ilihusisha Swawm ya viungo vyote vya mwili wangu: mdomo wangu ulifunga, kwani sikuwa nikizungumza isipokuwa ya heri pekee kama sina cha kusema basi hujinyamazia kimya; macho yangu pia yalikuwa katika Swawm, kwani sikuwa natazama isipokuwa kilicho halali kwangu mpaka wengine wakanidhania kuwa ni kipofu; mikono yangu pia ilikuwa kwenye Swawm, kwani sikuchukuwa isipokuwa changu; miguu yangu pia ilikuwa kwenye Swawm, kwani sikuwa nakwenda isipokuwa kwenye heri; masikio yangu pia yalifunga, kwani sikuwa nasikiliza muziki wala uzushi wowote ule, moyo wangu pia ulifunga, kwani sikuwa nabeba chui wala ubaya wala chochote kile dhidi ya waumini wenzangu.

C.     Swawm yangu ilihusisha kujifunga na kujitenga na kila kitu isipokuwa Allaah.

 

 

TAQWA

Allaah Anasema:

“Enyi mlioamini! Mmeandikiwa Swawm kama iliyoandikwa kwa wale ambao wa kabla yenu mpate kuwa na taqwa[Al-Baqarah: 183]

Aayah inabainisha kuwa anayeingia katika Swawm ya Ramadhaan huwa ameingia katika chuo kikuu cha taqwa; hivyo basi kama ulikuwa hunayo hiyo taqwa hata chembe, kwa kuingia kwenye Swawm ya Ramadhaan ulitarajiwa kwa namna moja au nyingine kujinyakulia japo chembe ya taqwa na kuweza kufikia kuwa na daraja fulani ya taqwa; na kama kabla ya kuingia katika Swawm ya Ramadhaan ulikuwa nayo, basi ilitarajiwa kuongezeka na sio kupungua; suala hapa ni hili, nini hiyo Taqwa? Taqwa au kuwa na taqwa ni kutekeleza yale yaliyoamrisha na Allaah kadiri ya uwezo wako na kujiepusha bali kuwa mbali kwa kuachana na makatazo Yake.

Ndugu yangu katika iymaa, jitathmini nafsi yako na tathmini matunda ya taqwa yako uliyoichota kwenye mwezi wa Ramadhaan, je, umeweza kufikia daraja iliyotarajiwa kama hii iliyoelezwa:

Kutoka kwa Abu Dharr (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema kuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliniambia:

“Mche Allaah popote pale ulipo, na fuatisha kitendo kibaya kwa kitendo kizuri kitafuta (kitendo kibaya), na ishi na watu kwa uzuri.” [Imepokelewa na At-Tirmidhiyy katika Kitabu cha al Birri wasw Swillah, mlango wa yaliyokuja katika kuishi na watu kwa wema, Hadiythi namba 1907, na amesema kuwa: hii Hadiythi ni Hasan Sahihi].

 

     A. Ndio.

     B. Hapana.

C. Sielewi.

Ndugu yangu katika iymaan, jaribu kutathmini athari au matunda ya taqwa yako uliyoichota kwenye mwezi wa Ramadhaan, je, imeengezeka na kuweza kukufikisha wapi?

A.     Imeengezeka, kwani siku hizi naziswali Swalah zangu zote.

B.      Nahisi imeengezeka kwa kuwa kuna mabadiliko na maendeleo kiasi fulani katika dini yangu.

C.    Kwa mara yangu ya kwanza ndio nina hisia ya kuwa na taqwa ya Allaah na kuiogopa Siku ya kurudishwa Kwake.

D.    Imeengezeka kwani nimeachana na maasi fulani niliyokuwa nimeshikamana nayo.

 

QUR- AAN

Allaah Anasema:

Mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan...” [Al-Baqarah 2: 185].

Mjumbe wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wasallam) amesema:

“Mfano wa yule (katika Riwaya ya Muslim: mfano wa Muumin) ambae anaisoma Qur-aan ni kama tunda la Utrujjah –balungi- ladha yake tamu na harufu yake nzuri. Na yule (katika Riwaya ya Muslim: na mfano wa Muumin) ambae hasomi Qur-aan ni kama tende ladha yake tamu na wala haina harufu...” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Fadhaail za Qur-aan, mlango wa Ubora wa Qur-aan mbele ya maneno mengine, Hadiyth namba 4659; na Muslim, katika Kitabu cha Swalah ya Wasafiri na upunguzwaji wake, mlango wa Ubora wa Haafidh –mwenye kuhifadhi- Qur-aan, Hadiyth namba 1334].

 

Ndugu yangu katika iymaan; tathmini uhusiano wako na Qur-aan katika mwezi ulioteremshwa hiyo Qur-aan; uliisoma mara:

 

A. Moja.

B. Mbili.

C. Zaidi ya mbili.

D. Sikuwahi kuhitimisha.

 

E. Sikuisoma hata mara moja, kwani sijuwi kusoma Qur-aan.

 

 

Ndugu yangu katika iymaan; tathmini mahusiano yako na Qur-aan katika mwezi ulioteremshwa hiyo Qur- aan; unajihisi uko katika kundi lipi?

 

A. Mjumbe wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wasallam) amesema: “Hakika Allaah Anao watu Wake wa karibu -Anaowapenda- katika watu.” Akasema: Pakasemwa: Ni nani hao ee Mjumbe wa Allaah? Mjumbe wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wasallam) akasema:Ahlul Qur-aan -watu walioiandama Qur-aan kwa kuisoma na kuifuata- hao ndio Ahlu Allaah –watu wa Allaah- na Khaaswatuh.[Imepokelewa na Ahmad, kitabu Musnad ya Kumi waliobashiriwa Jannah, Baaqiy Musnad Mukthiriyna katika Swahabah, Musnad Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu), Hadiyth namba 12065; na Ibn Maajah, katika Kitabu cha Ibn Maajah, milango ya Fadhaail za Swahabah wa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), mlango wa fadhila za mwenye kujifunza Qur-aan na kuifundisha, Hadiyth namba 211; na Al-Mustadrak ‘Alaa Asw-Swahiyhayn, katika Kitabu cha Imaamah na Swalah ya Jama’ah, mlango wa Ta-amiyn, Hadiyth namba 1981].

 B. Mjumbe wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Yule aliyekuwa hodari wa kusoma Qur-aan atakuwa pamoja na Malaika Waandishi wa Allaah watukufu; na yule ambaye anaisoma Qur-aan kwa mashaka na huku anajitahidi kwa kudodosa atapata ujira mara mbili” [Imepokelewa na Muslim, katika Kitabu cha Swalah ya Wasafiri na Kupunguzwa kwake, mlango wa fadhila za aliye hodari katika Qur-aan na yule ambae..., Hadiyth namba 1335].

 

C.Mjumbe wa Allaah(Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitujia wakati tulikuwa katika Suffah akauliza: “Kuna yeyote miongoni mwenu anayetaka kwenda soko la But-haan-Al-'Aqiyq na akapata humo ngamia wawili (wa thamani kabisa wa kike) bila ya kutenda dhambi au kukata udugu? Tukajibu kwamba sote tunapenda kufanya na kupata hivyo. Kisha akasema, basi aende mmoja wenu msikitini akajifunze au asome Aayah mbili katika kitabu cha Allaah, basi akifanya hivyo ni bora kuliko ngamia (wa thamani kabisa wa kike). Na Aayah tatu ni bora kuliko ngamia watatu, na Aayah nne ni bora kuliko ngamia wanne, na mfano wa hivyo hivyo wa Aayah kwa ngamia” [Imepokelewa na Muslim, katika Kitabu cha Swalah ya Wasafiri na Kupunguzwa kwake, mlango wa fadhila ya kusoma Qur-aan katika Swalah na kujifunza, Hadiyth namba 1342].

 

D. Allaah Anasema: “Hakika wale wanaosoma Kitabu cha Allaah, na wakasimamisha Swalah, na wakatoa katika vile Tulivyowaruzuku kwa siri na kwa dhaahiri, hao hutaraji biashara isiyododa.  Ili Yeye Awalipe ujira wao kwa ukamilifu, na Awazidishie kutokana na fadhila Zake. Hakika Yeye ni Ghafuurun Shakuurun [Mwenye kusamehe Mwenye shukrani]” [Faatwir: 35:29-30].

 

 

Ndugu yangu katika iymaan; hebu sasa tathmini athari na matunda ya usomaji wako wa Qur-aan:

 

A. Tabia zangu zimekuwa zinakwenda sambamba na mafundisho ya Qur-aan kama ilivyothibiti katika hadiythi ya Ummul Muuminiyna ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anhaa) alipouliza muulizaji kuhusu akhlaaq za Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), alimjibu kwa kusema: “Wewe si unasoma Qur-aan? Muulizaji akajibu: Ndio. Ummul Muuminiyna ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anhaa) akasema:“Hakika khuluqu (tabia) za Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ilikuwa Qur-aan” [Imepokelewa na Ahmad, Musnad Kumi waliobashiriwa Jannah, Saadis ‘Ashara Al-Answaaar, Hadiyth Ummul Muuminiyna ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anhaa), Hadiyth namba 23714; na Abu Daawuud, katika Kitabu cha At-Tatwawu’, milango ya Qiyaamul Layl, Hadiyth namba 1146].

B. Usomaji wangu umeweza kunifikisha kuwa kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Al-Ashja’iy: “Usiku mmoja nilisimama -kuswali- pamoja na Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), basi alisoma Suuratul Baqarah; -usomaji wake ulikuwa kama hivi- hapiti kwenye Aayah ya rahma isipokuwa husita kusoma na kuomba –hiyo rahma-; na wala hapiti kwenye Aayah ya adhabu isipokuwa husimama kusoma na kujikinga –na adhabu-; kisha akasema: Kisha (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akarukuu –namna ilivyokuwa rukuu yake- kadiri -urefu wa- ya kisimamo chake; alikuwa akisema katika rukuu yake: Subhaana dhil Jabaruuti wal-Malakuuti wal-Kibriyaa wal-‘Adhwamah” (Ametakasika Mwenye Utawala, na Ufalme, na Ukubwa, na Utukufu); kisha (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) husujudu –namna ilivyokuwa sujudu yake- kadiri ya kisimamo chake; alikuwa akisema katika sujudu mfano wa hivo...” [Imepokelewa na Ahmad, kitabu Musnad ya Kumi waliobashiriwa Jannah, Musnadul Answaar, Hadiyth namba 23350; na Abu Daawuud, katika Kitabu cha Swalah, mlango wa Tafriygh milango ya Rukuu na Sujuud na kuweka mikono miwili juu ya mapaja mawili, Hadiyth namba 740].

 

C. Sasa nina shauku na hamu ya kutaka kuisikia Qur-aan kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Ibn Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimtaka Ibn Mas’uud (Radhiya Allaah ‘anhu) amsomee Qur-aan ili aisikilize, Ibn Mas’uud (Radhiya Allaah ‘anhu) akamwambia: “Ee Mjumbe wa Allaah vipi nikusomee Qur-aan na wewe ndiye uliyeteremshiwa?” Mjumbe wa Allaah (Swalla Alaahu ‘alayhi wa aalihi wasallam) akaniambia: "Mimi napenda kuisikiliza ikisomwa na mwengine.” Ibn Mas’uud (Radhiya Allaah ‘anhu) akasema: Nikasoma Suuratan-Nisaa hadi nilipofikia “Basi itakuwaje (siku hiyo) tutakapoleta kutoka katika kila Ummah shahidi, na tukakuleta wewe uwe shahidi juu yao (Ummah wako)?” [An Nisaa: 41] Mjumbe wa Allaah (Swalla Alaahu ‘alayhi wa aalihi wasallam) akaniambia: “Hasbuk –basi-hapo hapo, inatosha.” Nilipomuangalia usoni (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), nikaona macho yake yanabubujika machozi” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha Fadhaail za Qur-aan, mlango wa Kulia wakati wa kusoma Qur-aan, Hadiyth namba 4694 na 4695; na Muslim, katika Kitabu cha Swalah ya Wasafiri na Kupunguzwa kwake, mlango wa fadhila za kuisikiliza Qur-aan na kuomba isomwe na Haafidhi wa Qur-aan kwa ajili ya kuisikiliza na kulia, Hadiyth namba 1338 na 1339].

 

 

 

 

QIYAAM

 

Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Atakayesimama Ramadhaan -usiku kwa kuswali- kwa iymaan na kutaraji malipo ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia” [Imepokelewa na Muslim, kitabu cha Swalah ya wasafiri na kupunguzwa kwake, mlango wa Tar-ghiyb katika Qiyaam cha Ramadhaan nayo ni Taraawiyh, Hadiyth namba 1272].

 

Ndugu yangu katika iymaan, Hadiythi inaashiria kusimama Ramadhaan –kwa maana kuwa mwezi wote; tokea siku iliyotangazwa kuingia kwake siku ambayo Swalah ya Tarawiyh huanza mpaka siku iliyotangazwa kutoka kwake, siku ambayo huwa hakuswaliwi Swalah ya Tarawiyh- na sio baadhi ya siku zake wala vyenginevo, ulikuwa ukihudhuria kwenye msikiti au misikiti kwa kutekeleza Swalah ya Tarawiyh; sasa vipi yalikuwa mahudhurio yako, na vipi ulikuwa utekelezaji wa Swalah kulingana na msikiti uliojichagulia? 

 

Mahudhurio: 

Unajipa daraja gani kwa mahudhurio yako?

A. Kila siku nilikuwa nikihudhuria kwa wakati.

B. Kwa wakati, mara nyingi.

C. Hayakuwa kwa wakati mara nyingi.

         

          D.Swalah ya ‘Ishaa nikiiswali kwa jamaa ya Swalah ya Tarawiyh.

 

E.     Siku nyingi sikuhudhuri

 

F.     Nilikuwa na shauku na hima katika siku za mwanzo kisha nikafanya uvivu na kutohudhuria.

 

G.    Nilishindwa kuhudhuria katika masiku kumi ya mwisho kwani nilikuwa nikijitayarisha na sikukuu.

 

Utekelezaji wa Swalah:

Unajipa daraja gani katika utekeleza wa Swalah zako zote kwa ujumla na Swalah ya Tarawiyh hasa.

 

A.    Daraja ya wenye kustahiki kuambiwa rudi ukaswali kwani hukuswali, kama ilivyothibiti katika Hadiythi ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) pale aliposema kuwa: “Kuna mtu aliingia msikitini, ambao Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa amekaa. [Yule mtu] Akaswali rakaa mbili, kisha akaja kwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na akatoa salamu. Mjume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaijibu salamu yake, na akasema, “Rudi, ukaswali [tena] kwani hukuswali.”… . Hadi kufikia mara tatu; yule mtu akasema: “Naapa kwa Yule Ambaye Amekutuma wewe kwa Haki, Ewe Mjumbe wa Allaah, sijui namna nzuri yoyote ile isipokuwa hivi, tafadhali nifundishe.”. [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Adhana, milango ya sifa ya Swalah, mlango amri ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa yule asiyetimiza rukuu kurejea kuswali, Hadiyth namba 755; na Muslim, katika Kitabu cha Swalah, mlango wa wajibu wa kusoma Al Faatihah katika kila rakaa, Hadiyth namba 607].

 

B.     Daraja ya wenye kufuata mafundisho ya Swalah kama alivoyafundisha na kuyatekeleza Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama yalivyothibiti katika sehemu ya mwisho ya Hadiythi ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) pale Mjumbe wa Allaah alipomfundisha yule aliyekuwa akiswali kwa kuondosha jukumu na kuipururuwa Swalah kwa kusema kuwa : “…Ukisimama kwa ajili ya Swalah, sema: “Allaahu Akbar”, kisha soma ambacho kitakujia kwa wepesi katika Qur-aan, kisha rukuu mpaka utakapohisi kwamba umetulia katika rukuu yako, kisha, simama mpaka uwe umesimama wima kisawa sawa, kisha sujudu mpaka uwe umetulia katika sujudu yako, kisha kaa mpaka uwe umetulia katika kikao chako, kisha sujudu -sijida ya pili- mpaka uwe umetulia katika sujudu yako; na uwe unafanya hivi ndani ya Swalah yako yote”.. [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Adhana, milango ya sifa ya Swalah, mlango amri ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa yule asiyetimiza rukuu kurejea kuswali, Hadiyth namba 755; na Muslim, katika Kitabu cha Swalah, mlango wa wajibu wa kusoma Al Faatihah katika kila rakaa, Hadiyth namba 607].

 

C.    Daraja ya wenye kustahiki kuitwa wezi waovu wenye kuiba Swalah zao, kama ilivyothibiti katika Hadiythi kuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:“Mwizi muovu kuliko wote ni yule ambaye anaiba katika Swalah yake”. Swahaaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) wakauliza: “Ewe Mjumbe wa Allaah, mtu huwa anaibaje katika Swalah yake?” Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Hakamilishi rukuu na sujudu zake” [Imepokelewa na Ibnu Hibbaan, katika Kitabu cha Swalah, mlango wa sifa ya Swalah, Hadiyth namba 1925; na Ad Daarimuy, katika Kitabu cha Swalah, mlango wa katika yule ambae hatimizi/hakamilishi Rukuu na Sujudu, Hadiythi namba 790]. 

 

D.    Daraja ya Waumini kama ilivyothibiti katika Suuratu Muuminiyna; Allaah Anasema:Kwa yakini wamefaulu Waumini.  Ambao katika Swalaah zao huwa wananyenyekea. Na ambao wanajiepusha na (mambo, maneno na vitendo vya) upuuzi. Na ambao wanatoa Zakaah. Na ambao wanazihifadhi tupu zao (kutokana na faahishah). Isipokuwa kwa wake zao, au kwa iliyowamiliki mikono yao ya kuume (kulia), basi hao hawalaumiwi. Lakini atakayetaka kinyume ya hayo; basi hao ndio wanaoruka mipaka. Na ambao amana zao na ahadi zao wanazichunga (wanazitimiza). Na ambao wanazihifadhi (wanasimamisha ipasavyo na itakiwavyo) Swalaah zao.” [Al Muuminuwna 23:1-9]

 

 

Swadaqah:

Amesema Ibnu ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu)maa) kwamba: “Alikuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ajwad (mkarimu) wa watu, na alikuwa ajwad zaidi katika Ramadhaan wakati anapokutana na Jibriyl (‘Alayhis Salaam), alikuwa -Jibriyl (‘Alayhis Salaam)- akimjia Swalla Alllaahu ‘alayhi wa aalihi wasallam kila usiku wa Ramadhaan akimdurusisha Quraan” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha Swawm, mlango alikuwa (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mkarimu/mbora zaidi katika Ramadhaan, Hadiyth namba 1179].

 

Pia Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ni juu ya kila Muislamu Swadaqah; pakaulizwa: Ee Mtume wa Allaah! Asiyekuwanayo je? Akasema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): Afanya kwa mkono wake, ainufaishe nafsi yake na atoe Swadaqah; pakaulizwa ikiwa hakupata je? Akasema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): Amsaidie mwenye haja malhuuf; pakaulizwa ikiwa hakupata je? Akasema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): Afanye kwa ma’aruuf na aachane na shari kwani hakika hayo kwake ni Swadaqah” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha Zakaah, mlango juu ya kila Muislamu Swadaqah na asiyekuwa nayo...., Hadiyth namba 1360; na Muslim, katika Kitabu cha Zakaah, mlango wa ubainifu kuwa neno Swadaqah linatumika pia kwa kila aina ya ma’aruuf, Hadiyth namba 1682].

 

Ndugu yangu katika iymaan, Swadaqah katika mwezi wa Ramadhaan mwezi wa kutoa, kwa watoaji ni fursa ya pekee na adhimu kwa kila aliyewafikishwa kutoa chochote kile katika yenye kutolewa kulingana na hali yake na pia kulingana na kinachohitajika na pahala alipo na wakati anapotoa, na kuelewa kuwa unapotoa huwa unatoa na kumpa Al-Ghaniyyul Kariymu; kwa kuelewa hayo ndio ukawa unatoa; sasa tathmini utoawaji wako wa Swadaqah na mengineyo katika yenye kustahiki kutolewa; jitathmini hali ya nafsi yako kwa kile ulichokitowa pale ulipotoa na baada ya kutoa na mpaka hii leo:

A.    Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Saba Allaah Atawafunika katika kivuli Chake siku ambayo kutakuwa hakuna kivuli isipokuwa kivuli Chake: Imaam –kiongozi- muadilifu, na kijana aliyekulia katika kumwabudu Allaah, na mwanaume ambae moyo wake umesehelea kwenye misikiti; na watu wawili wapendanao kwa ajili ya Allaah kukutana kwa ajili ya Allaah na kuachana kwa ajili ya Allaah, na mwanaume aliyeitwa na mwanamke mwenye cheo na mzuri kwa kutaka kufanya tendo la haramu, akasema: “La, hakika mimi namuogopa Allaah, na mwanaume anayetoa swadaqah kwa siri ya hali ya juu mpaka ikafikia kuwa mkono wake wa kushoto hauelewi kile kilichotolewa na mkono wa kulia -atoae swadaaah bila ya wengine kujua-, na mwanaume anayemkumbuka Allaah kwa faragha mpaka macho yake yakatokwa na machozi.” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Adhana, milango ya Swalah ya Jamaa’ah na na Imaamah, mlango wa aliyekaa msikitini kungojea Swalah, Hadiyth namba 624; na Muslim, katika Kitabu cha Zakkah, mlango wa fadhila za kuficha Swadaqah, Hadiyth namba 1718].

B.     Allaah Anasema:Wale ambao wanatoa mali zao katika njia ya Allaah kisha hawafuatishii kwa waliyoyatoa masimbulizi wala udhia watapa ujira wao kwa Mola wao, na wala hakuna khofu juu yao na wala hawatohuzunika.” [Al Baqarah 2:262].

C.     Allaah Anasema: Ambao wanaotoa katika (hali ya) wasaa na katika (hali ya) shida, na wanaozuia ghadhabu, na wenye kusamehe watu. Na Allaah Anawapenda Al-Muhsiniyn. [Aal ‘Imraan 3:134].

D.     Allaah Anasema: Enyi mlioamini! Msibatilishe swadaqah zenu kwa masimbulizi na udhia kama yule ambaye anatoa mali yake kwa riyaa-a (kujionyesha) kwa watu, wala hamwamini Allaah na Siku ya Aakhirah. Basi mfano wake ni kama jabali juu yake pana udongo, kisha likapigwa hilo jabali na mvua kubwa ikaliacha tupu. Hawatakuwa na uwezo juu ya lolote katika waliyoyachuma. Na Allaah Haongoi watu makafiri.” [Al Baqarah 2:264].

E.     Allaah Anasema: Wanafiki wanaume na wanafiki wanawake, wao kwa wao. Wanaamrisha munkari (maovu) na wanakataza ma’aruwf (Uislamu, mema) na wanafumba mikono yao (wasitoe katika Njia ya Allaah); wamemsahau Allaah (kwa kupuuza Amri Zake), basi Naye Amewasahau. Hakika wanafiki wao ndio mafasiki.” [A Tawbah 9:67]

 

Allaah Anasema:

Na wala usifanye mkono wako (kama) uliofungwa shingoni mwako (kama bakhili), na wala usiukunjue wote kabisa (ukatoa tu mali bila ya kipimo), ukaja kubakia mwenye kulaumiwa, mwenye kufilisika. Hakika Mola wako Anakunjua riziki kwa Amtakaye na Anadhikisha. Hakika Yeye daima kwa waja Wake ni Khabiyram-Baswiyraa (Mjuzi wa undani na ukina wa mambo - Mwenye Kuona yote daima).” [Al Is-raa 17:29 -30].

 

Ndugu yangu katika iymaan, sasa tathmini kile ulichotowa, je, kweli kilikuridhisha na uliridhika nacho?

A.     Allaah Anasema: Enyi mlioamini! Toeni katika twayyibaat (halaal, vizuri) mlivyochuma na katika ambayo Tumekutoleeni kutoka katika ardhi. Na wala msikusudie vibaya kutoka humo mkavitoa na hali nyinyi (wenyewe) si wenye kuvichukuwa isipokuwa kuvifumbia macho. Na jueni kwamba hakika Allaah ni Ghaniyyun-Hamiyd (Mkwasi, Hahitaji lolote - Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa na Kushukuriwa kwa yote daima.”. [Al-Baqarah 2:267].

B.     Allaah Anasema: Ni nani atakayemkopesha Allaah mkopo mzuri kisha (Allaah) Amzidishie mzidisho mwingi. Na Allaah Anakunja na Anakunjua, na Kwake mtarejeshwa”. [Al-Baqarah 2:245].

C.    Allaah Anasema: Mfano wa wale ambao wanatoa mali zao katika njia ya Allaah ni kama mfano wa punje moja (ya mbegu) iliyotoa mashuke saba, katika kila shuke kuna punje mia. Na Allaah Humzidishia Amtakaye; na Allaah ni Waasi’un-‘Aliym (Mwenye Wasaa, Mkunjufu- Mjuzi wa yote daima)”. [Al-Baqarah 2:261].

         

D.   Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:"Anapokufa mwanaadamu humkatikia amali zake isipokuwa –amali za aina- tatu: Swadaqatun Jaariyah (Swadaqah inayoendela), au elimu inayonufaisha, au mtoto mwema anayemuombea". [Imepokelewa na Muslim, katika Kitabu cha Waswiyyah, mlango wa yale yenye kumfuata mwanaadamu katika thawabu baada ya kufa kwake, Hadiythi namba 3092].

E.    Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hatotoa Swadaqah mja yeyote yule Muumin kutokana na twayyib -chumo la halali- na Allaah Hakubali isipokuwa twayyib, na wala hakipandi mbinguni isipokuwa twayyib, -anapoitoa hiyo Swadaqah huwa- anaiweka katika Mkono wa Ar-Rahmaan au kwenye kitanga cha Ar-Rahmaan [na katika Al-Bukhaariy]: Na Allaah huipokea kwa Mkono Wake wa kulia), basi Allaah Atamzidishia hadi itafikia kuwa kokwa ya tende mfano wa mlima mkubwa” [Imepokelewa na Ahmad, katika Musnad wa Kumi waliobashiriwa Jannah, Musnad iliyobakia katika Mukthiriyna katika Sahabah, Hadiyth namba 9219, na Al-Bukhaariy, kitabu cha Zakaah, mlango wa Swadaqah kutokana na chumo zuri, Hadiyth namba 1327].

 

E.     Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Tabasamu lako usoni kwa nduguyo ni Swadaqah, kuamrisha kwako mema na kukataza kwako maovu ni Swadaqah; kumuongoza kwako njia mtu katika ardhi (nchi) ya upotevu, hilo kwako ni Swadaqah; kuondosha kwako njiani udhia, mwiba na mfupa, hilo kwako (nalo) ni Swadaqah; kumtekea kwako maji nduguyo, kwako ni Swadaqah na kumsaidia kwako mtu dhaifu wa uoni kuongoza njia, (hilo nalo) kwako ni Swadaqah” [Imepokelewa na At Tirmidhiyyu, katika Kitabu cha Ijumaa, milango ya safari, Hadiythi namba 1876].

 

Allaah Anasema:

 Hakika Allaah Amenunua kwa Waumini nafsi zao na mali zao kwamba watapata (badala yake) Pepo. Wanapigana katika Njia ya Allaah, wanaua na wanauawa. Hii ni ahadi ya haki Aliyojiwekea (Allaah kuitimiza) katika Tawraat na Injiyl na Qur-aan. Na nani atimizae zaidi ahadi yake kuliko Allaah? Basi furahieni kwa biashara yenu mliyouziana Naye. Na huko ndiko kufuzu kukubwa. .” [A Tawbah 9:111]

 

Ndugu yangu katika iymaan, sasa tathmini kiasi ulichotowa, je, kweli ulichokitowa kinathibitisha kujiuzwa kwako na mali yako kwa aliyekupa hicho ulichokitowa baada ya kuelewa kuwa bidhaa ya Allahn ni ghali?  Je, ulichotoa kiliweza kufikia kiwango cha kustahiki hiyo bidhaa ya Allaah? Kwani ulitoa kiasi gani?

 

A.      ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema kuwa: “Alituamrisha Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoa Swadaqah, ilisadifu kuwa nina mali, nikasema: Leo nitamshinda (nitamtangulia) Abu Bakr..., akasema: Nikaja na nusu ya mali yangu; Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaniuliza: Umewabakishia nini ahli zako? Akasema: Nikamjibu: Mfano wake –nusu-; akaja Abu Bakr na kila alichokimiliki; Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaniuliza: Umewabakishia nini ahli zako? Akasema: Nimewabakishia Allaah na Mjumbe Wake; nikasema: WaLlaahi sitomtangulia kwa kitu cho chote abadan.” [Imepokelewa na At-Tirmidhiy, katika Kitabu cha ad Da’awaat, milango ya Manaaqiyb, mlango katika Manaaqiyb ya Abi Bakr na ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhumaa), Hadiyth namba 3638 na Abu Daawuud, katika Kitabu cha Sujuud za Qur-aan, Hadiyth namba 1432].

 

B.     Thalathini; kwa kiwango cha moja kwa kila siku ya Ramadhaan.

 

C.Sitini; kwa kiwango cha mbili kwa kila siku ya Ramadhaan.

 

C.    Tisini; kwa kiwango cha tatu kwa kila siku ya Ramadhaan.

 

D.     Nimetoa, lakini sikumbuki kiasi nilichotoa.

 

E.     Kwa kweli sikutoa kitu , kwani sina kawaida ya kutoa swadaqah.

 

 

 

Kufutarisha na kulisha Masikini:

Allaah Anasema:

”Na huwalisha chakula, juu ya kukipenda kwake, masikini, na yatima, na wafungwa Hakika Sisi Tunakulisheni kwa wajhi Allaah. Hatutaki kwenu malipo wala shukrani. Hakika sisi tunaiogopa kwa Mola wetu hiyo siku yenye shida na taabu. Basi Allaah Atawalinda na shari ya siku hiyo na Kuwakutanisha na neema na furaha. Na Atawajazi kwa vile walivyosubiri Jannatan na maguo ya hariri.” [Al-Insaan: 8-12]

 

Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Atakayemfuturisha aliyefunga, atapata ujira kama ujira wake -aliyefunga- bila ya kupungua chochote katika ujira wa yule aliyefunga.” [Imepokelewa na Ahmad, katika Musnad ya Kumi waliobashiriwa Jannah, Musnadush Shaamiyiyna, zilizobakia katika hadoytho za Zayd bin Khaalid Al-Juhayniy Radhiya Allaahu ‘anhu), Hadiyth namba 16713; na At-Tirmidhiy, katika Ijumaa, milango ya Safar, Hadiyth namba 734].

Ndugu yangu katika iymaan, sasa tathmini idadi ya watu uliofutarisha au lisha kwenye mwezi wa Ramadhaan, kwa kuelewa kuwa ulikuwa na uwezo wa kila siku au kila wiki angalau kupata thawabu za watu watatu waliofunga kwa hesabu kuwa uliweza kupata ujira wa funga nne ukijumuisha na yako; je, ulifutarisha watu wangapi?

 

A.     Watatu kwa kila wiki.

 

B.     Mmoja kwa wiki.

 

C. Sikuwa na wakati wa kufutarisha mtu.

 

 

Hitimisho:

 

Ndugu yangu katika iymaan, ulitarajiwa kuitumia fursa ya kukutana na mwezi wa Ramadhaan kujichumia mengi ya heri ambayo thawabu zake huanzia tokea kumi hadi zaidi ya mia saba pamoja na malipo maalum yatokayo kwa Allaah kwa mfungaji; katika hayo mengi ya heri lipi uliwafikishwa kulitekeleza:

 

A.     Allaah Anasema:

“Hakuna heri katika minong’ono yao mingi isipokuwa anayeamrisha kutoa swadaqah, au (kuamrisha) ma’aruwf (mema), au kusuhulisha baina ya watu. Na yeyote yule atakayefanya hivyo kutaka Radhi za Allaah, basi Tutampa ujira mkubwa.” [An-Nisaa 4:114].

 

B.     Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:”Yeyote yule anaetoka pamoja na Janazah kutokea nyumba yake –nyumba iliyotoka hilo Janazah-, na akaswalia, kisha akalifuata mpaka kuzikwa, atakuwa amepata qiyraatwaan katika ujira; kila qiyraatw mfano wa jabalí Uhud…” [Imepokelewa na Muslim, katika Kitabu cha Janaaiz, mlango wa fadhila ya Swalah ya Janaazah na kulifuata, Hadiythi namba 1580].

C.     Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mwenye kumuondolea Muumini shida miongoni mwa shida za ulimwengu, Allaah Atamuondolea shida miongoni mwa shida za Siku ya Qiyaamah; na mwenye kumsahilishia mwenye mazito, Allaah Atamsahilishia mazito yake duniani na Aakhirah; na mwenye kumsitiri Muislamu, Allaah Atamsitiri duniani na Aakhirah; … [Imepokelewa na Muslim, katika Kitabu cha Dhikr na Du’aa na Tawbah na Istighfaar, mlango wa fadhila ya kukusanyika kwa ajili ya kusoma Qur-aan, Hadiythi namba 4874].

 

 

Share