14-Umuhimu Wa Tawhiyd Na Fadhila Zake: Tawhiyd Ni jambo La Kwanza Walolingania Rusuli Wote

 

Umuhimu Na Fadhila Za Tawhiyd

 

14-Tawhiyd Ni jambo La Kwanza Walolingania Rusuli Wote

 

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

 وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ ﴿٢٥﴾

Na Hatukutuma kabla yako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) Rasuli yeyote isipokuwa Tulimfunulia Wahy ya kwamba: “Hakika hapana mwabudiwa wa haki ila Mimi; basi Niabuduni.” [Al-Anbiyaa: 25]

 

Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ

Na kwa yakini Tulituma katika kila ummah Rasuli (alinganie) kwamba: “Mwabuduni Allaah na jiepusheni na twaghuti.” [An-Nahl: 36]

 

Na Anasema pia (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 

 وَاسْأَلْ مَنْ أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رُّسُلِنَا أَجَعَلْنَا مِن دُونِ الرَّحْمَـٰنِ آلِهَةً يُعْبَدُونَ﴿٤٥﴾

 “Na waulize wale Tuliowatuma kabla yako miongoni mwa Rusuli Wetu; je, Tulifanya badala ya Ar-Rahmaan  waabudiwa wengine ili waabudiwe?” [Az-Zukhruf: 45]

 

 

 ‘Allaamah Swaalih Al-Fawzaan (Hafidhwahu Allaah) amesema katika mhadhara wake: “At-Tawhiyd Yaa Ibaada Allaah”: “Manabii wote kuanzia wa mwanzo wao hadi wa mwisho wao, walianza kulingania kwao watu kwa Tawhiyd, kwa kuwa Tawhiyd ndio msingi ambao Dini imejengeka. Tawhiyd ikiwa imara, nyumba itasimama vizuri na kuwa imara. Na huu ni mfano wa misingi ya majumba na majengo; kwanza huanza kwa kujenga msingi ukawa imara kisha ndio kukajengwa nyumba na kupandishwa. Nyumba haiwezi kusimama bila ya msingi imara. Lau utajenga nyumba bila ya msingi imara wenye nguvu, basi nyumba itaporomoka na kuangamia waliomo humo ndani. Hali kadhalika Dini ikiwa haikujengeka katika  ‘Aqiydah swahiyh, inakuwa ni dini isiyomfaa mtu na wala haimnufaishi chochote, hata kama atajitaabisha vipi kufanya juhudi. Dini yake haitomfaa kitu, kwa kuwa haikujengeka juu ya msingi swahiyh, nao ni Tawhiyd. Kwa ajili hio, kitu cha kwanza walichoanza Rusuli (‘Alayhimus-Salaam) kuwalingania watu wao, ilikuwa ni Tawhiyd, nayo ni kabla ya kuwaamrisha Swalaah, Zakaah, Swawm n.k. Na ilikuwa ni kabla ya kuwakataza zinaa, wizi, kunywa pombe na maasi mengine, walianza kwanza kwa msingi ambao ni Tawhiyd. Na kila Nabiy alimwambia kaumu yake:

 

 يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ

“Enyi kaumu yangu! Mwabuduni Allaah, hamna mwabudiwa wa haki ghairi Yake. 

 [Mwisho wa kunukuu maneno ya ‘Allaamah Al-Fawzaan].

 

 

Dalili hizo zimo katika kauli za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kuhusu Rusuli Wake Wafuatao:

 

 

Nabiy Nuwh (‘Alayhis-Salaam):

 

وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا نُوحًا إِلَىٰ قَوْمِهِ فَقَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ ۖ أَفَلَا تَتَّقُونَ ﴿٢٣﴾

Kwa yakini Tulimpeleka Nuwh kwa kaumu yake, akasema: “Enyi kaumu yangu! Mwabuduni Allaah, hamna mwabudiwa wa haki ghairi Yake. Je, basi hamtokuwa na taqwa?” [Al-Muuminuwn: 23]

 

 

 

Nabiy Huwd (‘Alayhis-Salaam):

 

وَإِلَىٰ عَادٍ أَخَاهُمْ هُودًا ۗ قَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ ۚ أَفَلَا تَتَّقُونَ ﴿٦٥﴾

Na kwa ‘Aad (Tuliwapelekea) kaka yao Huwd.  Akasema: “Enyi kaumu yangu! Mwabuduni Allaah, hamna mwabudiwa wa haki ghairi Yake. Je basi hamtokuwa na taqwa?”  [Al-A’raaf: 65]

 

 

Nabiy Swaalih ('Alayhis-Salaam):

 

وَإِلَىٰ ثَمُودَ أَخَاهُمْ صَالِحًا ۗ قَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ

 

Na kwa Thamuwd (Tuliwapelekea) kaka yao Swaalih. Akasema: “Enyi kaumu yangu! Mwabuduni Allaah, hamna mwabudiwa wa haki ghairi Yake. [Al-A’raaf: 73]

 

 

Nabiy Shu’ayb ('Alayhis-Salaam):

 

وَإِلَىٰ مَدْيَنَ أَخَاهُمْ شُعَيْبًا ۗ قَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ

Na kwa (watu wa) Madyan (Tuliwapelekea) kaka yao Shu’ayb.  Akasema: “Enyi kaumu yangu! Mwabuduni Allaah, hamna mwabudiwa wa haki ghairi Yake.  [Al-A’raaf: 85]

 

 

 Nabiy Ibraahiym ('Alayhis-Salaam):

 

وَإِبْرَاهِيمَ إِذْ قَالَ لِقَوْمِهِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاتَّقُوهُ ۖ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿١٦﴾

Na Ibraahiym pale alipowaambia kaumu yake: “Mwabuduni Allaah na mcheni. Hivyo ni kheri kwenu mkiwa mnajua. [Al-‘Ankabuwt: 16]

 

 

Nabiy Muwsaa ('Alayhis-Salaam):

 

وَإِذْ قَالَ مُوسَىٰ لِقَوْمِهِ يَا قَوْمِ إِنَّكُمْ ظَلَمْتُمْ أَنفُسَكُم بِاتِّخَاذِكُمُ الْعِجْلَ فَتُوبُوا إِلَىٰ بَارِئِكُمْ

 

Na pindi Muwsaa alipowaambia kaumu yake: “Enyi kaumu yangu! Hakika nyinyi mmedhulumu nafsi zenu kwa kuabudu kwenu ndama, basi tubuni kwa Muumbaji wenu.  [Al-Baqarah: 54]

 

Nabiy ‘Iysaa ('Alayhis-Salaam):

 

 لَقَدْ كَفَرَ الَّذِينَ قَالُوا إِنَّ اللَّـهَ هُوَ الْمَسِيحُ ابْنُ مَرْيَمَ ۖ وَقَالَ الْمَسِيحُ يَا بَنِي إِسْرَائِيلَ اعْبُدُوا اللَّـهَ رَبِّي وَرَبَّكُمْ ۖ إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ ۖ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ﴿٧٢﴾

 

Kwa yakini wamekufuru wale waliosema: “Hakika Allaah ni Al-Masiyh mwana wa Maryam.” Na Al-Masiyh alisema: “Enyi wana wa Israaiyl! Mwabuduni Allaah, Rabb wangu na Rabb wenu. Hakika mwenye kumshirikisha Allaah bila shaka Allaah Atamharamishia Jannah, na makazi yake yatakuwa ni motoni. Na madhalimu hawatopata yeyote mwenye kunusuru.” [Al-Maaidah: 72]

 

Na Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye aliwalingalia watu wake waliokuwa wakiabudu masanamu, miaka kumi na tatu alipokuwa Makkah kwa Tawhiyd kabla ya kufaridhishwa Swalaah, Zakaah, Swawm au Hajj. Akaamrishwa apigane na watu mpaka watu washuhudie kuwa laa ilaaha illa Allaah kama ilivyotajwa katika Hadiyth ifuatayo:

 

عن ابنِ عُمَرَ رضي الله عنهما أنَّ رسُوَل الله صلى الله عليه وسلم قال: ((أُمِرْتُ أَنْ أُقاتِلَ النَّاسَ حتَّى يَشْهَدُوا أنْ لا إلَهَ إلاَّ اللهُ وأنَّ محمداً رسوُل اللهِ، ويُقِيمُوا الصَّلاَةَ، ويُؤتُوا الزَّكاةَ، فإذا فَعَلوا ذَلِكَ عَصَموا منِّي دِماءَهُمْ وأمْوَالَهُمْ إلا بِحَقِّ الإِسْلامِ، وحِسابُهُم على اللهِ تعالى)

Imepokelewa kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhwiyaa Allaahu ‘anhumaa) ambaye amesema: “Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Nimeamrishwa nipigane na watu mpaka washahadie: “laa ilaaha illa Allaah” (hakuna mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah), na kwamba Muhammad ni Rasuli  wa Allaah mpaka watakaposwali, na wakatoa Zakaah na wakifanya hivyo, watakuwa wamepata himaya kwangu ya damu yao na mali yao isipokuwa kwa haki ya Uislamu. Na hesabu yao itakuwa kwa Allaah Ta’aalaa)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Share