Nasaha ´Adhimu Ya Shaykh Rabiy´ Kwa Salafiyyuun Wanaopetuka Mipaka Na Kuiharibu Salafiyyah

Nasaha ´Adhimu Ya Shaykh Rabiy´ Kwa Salafiyyuun Wanaopetuka Mipaka Na Kuiharibu Salafiyyah

 

Swali:

Vipi tutamuabudu Allaah (´Azza wa Jalla) kwa elimu ya Jarh wat-Ta´diyl ambayo ni katika elimu bora?

 

 

Jibu:

Utapofikia katika ngazi hii, katika elimu, uchaji Allaah, kuipa nyongo dunia na kumtakasia Allaah ´Ibaadah kwa kutafuta Uso wa Allaah, basi utajua ni vipi utajikurubisha kwa Allaah kwa hilo na namna utavyoilinda Dini hii. Elimu ya Jarh wat-Ta´diyl ni elimu kubwa. Hakuna mwenye kuiongelea isipokuwa wachache katika watu. Hata wengi katika wanachuoni wakubwa wa Hadiyth, wanachuoni hawakuwahesabu kuwa katika wanachuoni wa Jarh wat-Ta´diyl.

 

Mimi ninawaambia ya kwamba sio katika wanachuoni wa Jarh wat-Ta´diyl. Ninawanasihi ndugu zangu waache al-Ghuluu (uchupaji wa mipaka). Mimi ni mkosoaji. Nimekosoa idadi kubwa ya watu binafsi kwa makosa yao. Watu wakafanya hilo kuwa kubwa. Mimi najitenga kwa Allaah kutokana na Ghuluu. Msisemi Shaykh Rabiy´ ni Imaam wa Jarh wat-Ta´diyl. Kamwe. Ninamshuhudisha Allaah kuwa mimi ninachukia maneno haya.

 

Acheni uchupaji wa mipaka huu. Wa-Allaahi mimi tokea zamani umbile langu nachukia maneno haya. Wakati nilikuja kwa hilo kwa Ibn Khuzaymah ambaye ni Imaam wa wanachuoni - na yeye kweli ni Mwanachuoni. Lakini kusema ya kwamba ni Imaam wa wanachuoni, hili ni jambo kubwa, wallaahi. Maneno kama hayo yameingia pia kwa Waislamu. Tazama Maswahabah wanavyoelekezana [kwa wengine] "Amesema `Umar, amesema ´Uthmaan, amesema ´Aliy na kadhalika." Hatukuona majivuno (kati ya Maswahabah). Acheni mapambo haya. Yule mwenye elimu na akawa anajua Manhaj ya Salaf, akosoe. Wanachuoni wa Jarh wat-Ta´diyl wamekwishatubainishia hali za wanaume, waongo, wenye kuachwa, wenye hifdhi dhaifu, wadhaifu na kadhalika. Hali kadhalika ni nani mwaminifu, makini, mwenye kuhifadhi na kadhalika. Sisi ni wakosoaji. Mimi ni mkosoaji ambaye ni dhaifu. Nimekosoa makosa ambayo wengine wameyanyamazia au wameghafilika kwayo.

 

Acheni mambo haya. Yule mwenye elimu na akawa anajua Manhaj ya Salaf na akaona kuna Bid´ah ya wazi mbele yake, aiweke wazi kwa kutafuta Uso wa Allaah. Atoe nasaha kwa kutafuta Uso wa Allaah (Tabaaraka wa Ta´ala) kwa kuilinda Dini hii. Anakuja Mubtadiy´, mzushi na kuiharibu Dini kwa Bid´ah yake na anaongea juu ya Allaah pasina elimu na anaeneza upotevu wake kwa jina la Dini, sawa ikiwa kosa lake ni katika ´Aqiydah, ´Ibaadah, Manhaj, siasa, uchumi na kadhalika. Hivi sasa Ghuluu na uongezaji chumvi unaenea katika Da´wah ya Salafiyyah. Mpaka baadhi yao wamefikia katika daraja ya Rawaafidhw na Suufiyyah kwa Ghuluu. Sisi tunajitenga mbali kwa Allaah na Ghuluu hii. Fuateni Manhaj ya Salaf katika kuwa na ukati na kati na uadilifu na kuwaweka watu katika manzilah zao pasina kitu chochote katika Ghuluu.

 

Hivi sasa tuko katika uwanja wa Da´wah kama wanafunzi. Kama wanafunzi tumekosoa baadhi ya makosa, tuko na kitu katika ufahamu (elimu). Enyi ndugu! Ninawausia kupita katika njia ya Salaf-us-Swaalih, katika kujifunza, tabia na Da´wah. Pasina kuwa na ukali wala Ghuluu. Da´wah ikiongozwa na watu walio na subira, huruma na tabia nzuri kabisa. Wallaahi kwa haya Da´wah ya Salafiyyah itasambaa. Da´wah ya Salafiyyah kwa sasa inaliwa na wale wanaojinasibisha - sisemi Salafiyyuun - wanaojinasibishwa, na baadhi yao wanajinasibisha kwa dhuluma katika Manhaj hii. Wanaila mbele ya watu. Wameitia sura mbaya Da´wah ya Salafiyyah kwa njia kama hii. Ninamnasihi mtu kama huyo amche Allaah (´Azza wa Jalla) na ajifunze elimu ya manufaa, atende ´amali njema na awalinganie watu kwa elimu na hekima.

 

Ndugu, tovuti (websites) za kwenye intaneti zimekuwa nyngi hivi sasa. Kila mtu anafanya maskhara na wale wanaojiita Salafiyyuun. Wanafanya maskhara nao na wanapiga makofi kwa kufurahi. Yeyote katika nyinyi atakayejifunza na akaifahamu Tafsiyr (ya Qur-aan), basi awawekee watu makala ya Tafsiyr. Aayah zinazohusiana na Ahkaam, tabia, ´Aqiydah n.k. Wasambazie watu haya. Hii ndio Da´wah. Mwenye kuwa imara katika Hadiyth, awasambazie watu makala kuhusiana na Hadiyth. Maana ya Hadiyth, Ahkaam, halali, haramu, tabia n.k. Ijazeni dunia elimu. Kwani hakika watu wako na haja ya elimu hii. Ukhalifu kama huu unaipa picha mbaya Manhaj ya Salaf na unasababisha watu kuikimbia.

 

Acheni mambo haya, sawa ikiwa ni kwenye intaneti au uwanja mwingine miongoni mwa uwanja au nchi yoyote miongoni mwa nchi. Wapeni watu elimu ya manufaa. Mambo ya mijadala na ugomvi yasiingie kwa watu wala kwenu. Mmesoma kitabu hichi ambapo Salaf walikuwa wakijiepusha mbali na mambo ya majadiliano. Msijadiliane na yeyote isipokuwa katika hali ya dharurah na wala asifanye mjadala isipokuwa mwanachuoni ambaye anaweza kuwashinda Ahl-ul-Bid´ah (watu wa Bid´ah).

 

Vilevile msiingie katika ugomvi nyinyi kwa nyinyi. Kukipitika kitu katika kosa, basi lirudisheni kwa wanachuoni. Msiingie ndani ya matatizo haya na uongo, kwa kuwa mambo haya yanaidhuru Da´wah ya Salafiyyah na kuipa madhara makubwa ambayo hayajapatikana katika historia. Hizi njia za ukhalifu zimesaidia, intaneti ya kishetani imesaidia matatizo haya. Kila mwenye kuwa na uwezo anaanza kuweka kichwa chake na kuanza balaa zake kwenye intaneti.

 

Acheni mambo haya. Ongeeni kwa elimu itawapa heshima na kuipa heshima Da´wah yenu. Yule asiyekuwa na elimu asiwaandikie watu lolote, si kwenye intaneti wala sehemu nyingine. Jiepusheni mbali na wivu na uadui. Vinginevyo wallaah, mtaifisha Da´wah hii. Natumai hakuna yeyote miongoni mwenu hapa ambaye ameshiriki katika balaa hizi. Ninamuomba Allaah Atuthibitishe sisi na nyinyi katika Sunnah.

 

Sikilizeni ndugu! Yule mwenye elimu na akawa imara juu yake, muache awaandikie watu kwenye intaneti yale ambayo yatawapa manufaa watu, katika Tafsiyr na yeye akawa na uhakika (wa anachokiandika), ´Aqiydah, tabia, Ahkaam na kadhalika. Tafsiyr ni bahari (ya elimu). Wallaah, unapoongea basi uko unaongea kutoka kwenye bahari. Hadiyth zote ambazo uko nazo zifafanue kwa ufafanuzi (maelezo) ya wanachuoni, ufafanuzi ulio na nguvu kisha baadaye wasambazie watu. Hali kadhalika katika ´Aqiydah, ´Ibaadah, tabia, kwa usulubu mzuri, haya yatawafaa watu. Wallaahi, mtaona wenyewe jinsi Salafiyyah itaendelea, kukuwa na kuwafaa watu na jinsi dunia itakuwa na mwanga (wa Da´wah ya Salafiyyah). Ama hivi leo, Salafiyyah inakandamizwa kwa sura hii.

 

Ninawanasihi kuacha mijadala na ugomvi kwenye intaneti na katika uwanja (wa Da´wah). Ninawanasihi kwa hili. Yule mwenye elimu aongee kwa elimu. Andika na kulingania kwa elimu. Aite kwa hoja na dalili na jiepusheni mbali na tofauti na sababu za kugawanyika. Msiziwashe baina yenu. Kukipitika kwa mtu kosa, lipelekwe kwa wanachuoni waliangalie vipi watalitatua.

 

 

 

Share