Kukaribisha Mwezi wa Ramadhwaan – Shaykh ‘Abdur-Razzaaq bin ‘Abdil-Muhsin Al-Badr

Ummah wote wa Kiislam katika siku chache zijazo watampokea mgeni mtukufu na ujumbe wa heshima; nyoyo zinajifakharisha naye kwenye ujio wake na nafsi zinasubiria kuwasili kwake, kwani huyo ni mpendwa wa nyoyo za Waumini,  mtukufu kwa nafsi zao, wanapeana bishara nzuri kwa kuja kwake na wanapongezana baadhi yao kwa wao kwa kufika kwake. Kila mmoja wao anatarajia kufika huyu mgeni na kupata kheri na Baraka zilizomo ndani yake.

Tanabahi! Huo ni mwezi wa Ramadhaan uliobarikiwa, mwezi wa kheri na baraka, mwezi wa utii na kujikurubisha, mwezi wa Swawm na Qiyaam (kuswali usiku),  kusoma Qur-aan. Ni mwezi wa kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kuomba maghfira na kuomba du’aa na kuomba kuokoka. Ni mwezi wa ukarimu na wema na juhudi na mwezi wa kutunuku na kufanya ihsani.  Mwezi uliojaa kheri na kila aina za baraka na faida kubwa. Huo ndio mwezi wenu wa Ramadhaan ambao Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameufanya mahususi kwa mambo matukufu, mwezi ambao unatofautiana na miezi mingine.

Mtume (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anawabashiria Maswahaba wake kwa kuja mwezi wa Ramadhaan na akiwabainishia mambo yake mahususi na fadhila zake na akiwahimiza juu ya kujipinda na kujitahidi ndani yake kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kujikurubisha kwake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa mambo Anayoyaridhia.

Imethibitika katika Musnad wa Imaam Ahmad kwa isnadi nzuri toka kwa Anas bin Malik (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema; Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

هذا شهر رمضان قد جاءكم فيه تفتّح أبواب الجنة وتغلَّق أبواب النار وتصفّد الشياطين

Mwezi huu wa Ramadhaa umekufikieni, milango ya Pepo humo hufunguliwa na milango ya Moto hufungwa na mashaytwaan hufungwa minyororo.

Na imethibiti katika Sunan at-Tirmidhiy na wengine kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa amesema:  

 

  إِذَا كَانَ أَوَّلُ لَيْلَةٍ مِنْ شَهْرِ رَمَضَانَ صُفِّدَتْ الشَّيَاطِينُ وَمَرَدَةُ الْجِنِّ وَغُلِّقَتْ أَبْوَابُ النَّارِ فَلَمْ يُفْتَحْ مِنْهَا بَابٌ وَفُتِّحَتْ أَبْوَابُ الْجَنَّةِ فَلَمْ يُغْلَقْ مِنْهَا بَابٌ وَيُنَادِي مُنَادٍ يَا بَاغِيَ الْخَيْرِ أَقْبِلْ وَيَا بَاغِيَ الشَّرِّ أَقْصِرْ وَلِلَّهِ عُتَقَاءُ مِنْ النَّارِ وَذَلكَ كُلُّ لَيْلَة

Inapofika usiku wa mwanzo wa mwezi wa Ramadhaan, mashaytwaan na majini waovu hufungwa minyororo, milango ya Moto hufungwa hakuna hata mlango mmoja unaofunguliwa, na Milango ya Pepo hufunguliwa hakuna hata mlango mmoja unaofungwa, na mwenye kunadi anaita: “Ee mtafuta kheri! Njoo mbele (uwe tayari kutenda)! Na ee mtafuta shari! Zuia! Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Huacha huru watu wengi. Na hivyo ni kila usiku (wa Ramadhaan).

Hadiyth hizi zinaonyesha fadhila za mwezi huu na ukubwa wa shani yake. Na utukufu wa daraja yake mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Kwa hiyo wajibu kufurahia upeo wa furaha yetu kwa kuja mwezi huu kwa sababu ya kheri zake nyingi. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

قُلْ بِفَضْلِ اللَّـهِ وَبِرَحْمَتِهِ فَبِذَٰلِكَ فَلْيَفْرَحُوا هُوَ خَيْرٌ مِّمَّا يَجْمَعُونَ ﴿٥٨﴾

Sema: “Kwa fadhila za Allaah na kwa Rahmah Yake basi kwa hayo wafurahi.” Hayo ni kheri kuliko wanayoyakusanya.  (Yuwnus: 58)

Tuelewe heshima yake, na tuchunge utukufu wake, na kusimamia uzuri wa ujumbe na ugeni wake.

Kwa hakika kufurahia ujumbe wa mwezi huu na kujua fadhila zake ni katika mambo matukufu yalioainishwa ndani yake. Watu wengi hawapotezi utiifu ndani ya mwezi huu mtukufu na kuelekea kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) isipokuwa ambaye asiyejua thamani na hadhi yake. Vinginevyo, lau Muislamu angejua mwezi huu kikweli kweli angejiandaa kwa ajili yake maandalizi mazuri, na angetoa mwisho wa juhudi yake katika kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kusimama kwa ‘ibaada yake juu ya njia ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anairidhia.

Swali ambalo anaiulizia nafsi yake mtu katika siku hizi ni: “Vipi nitaipokea mwezi huu mtukufu? Vipi nitajiandaa kwa ajili yake msimu huu mtukufu?”.  Vipi basi tutajiandaa kwa mwezi huu uliobarikiwa?

Kuupokea mwezi huu sio kwa kubadilisha maeneo kwa mawaridi na maua, wala kwa nashiyd na kughani mashairi, wala kwa kuandaa michezo, wala kwa kukusanya aina za vyakula na vinywaji,  kwani kujiandaa kwa mwezi huu ni kujiandaa kwa utiifu na ‘ibaada na kuelekea kikweli kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), na toba ya kweli kwa dhambi zote na makosa.

Hakika msimu wa Ramadhaan ni fursa ya kuelekea kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kutubia madhambi, kwani mwenye kuangalia hali yake na mwezi huu, kila mmoja wetu atajua kuwa kasoro zake ni kubwa kwa kauli ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

  كُلُّ بَنِي آدَمَ خَطَّاءٌ وَخَيْرُ الْخَطَّائِينَ التَّوَّابُونَ  

Kila binaadamu ni mkosa, lakini wakosa bora kabisa ni wenye kutubia.

Kwa hiyo dhambi ni nyingi, na upungufu upo, na mbele yetu kuna msimu mtukufu kwa ajili ya kutubia kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).   

Nafsi zisiposhughulika kwa toba na kujuta kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kutokana na kufanya dhambi, basi lini zitashughulikia hayo? Imeswihi katika Hadiyth kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

رَغِمَ أَنْفُ رَجُلٍ دَخَلَ عَلَيْهِ رَمَضَانُ ثُمَّ انْسَلَخَ قَبْلَ أَنْ يُغْفَرَ لَهُ  رواه الترمذي وأحمد  

Amekhasirika mtu ambaye Ramadhaan imemfikia kisha ikaondoka kabla ya kughufuriwa  At-Tirmidhiy na Ahmad.

Hivyo ni kwa sababu ni musimu mkubwa wa kutubia; nyoyo hutingisika kwa ajili ya kutubia kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kurudia Kwake na kuelekea katika utiifu wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

Miongoni mwa ya kupokelea mwezi huu mtukufu ni du’aa ya kweli na mafungamano mazuri kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kuelekea kwa ukamilifu Kwake Yeye Subhaanahu wa Ta'aalaa  Amsaidie mja katika utiifu wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika mwezi huu wenye fadhila, kwani  mja hana uwezo wa kusimama kwa utiifu na kuhakikisha ‘ibaada na kuifanya kwa ukamilifu wake isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atakapomsaidia

لَوْلَا اللَّهُ مَا اهْتَدَيْنَا وَلَا صُمْنَا وَلَا صَلَّيْنَا

Lau kama si Allaah Tusingeongoka wala tusingelifunga Swawm wala tusingeliswali.  Al-Bukhaariy 5/430

Kwa ajili hii, ni wajibu kwa Waumini kuelekea kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) wakimuomba na kumtarajia msaada Wake kwa kuwarahisishia Swawm ya Ramadhaan, na kuwasaidia kuusimamia na kuwaandikia kheri na baraka ndani yake na kuwafanya ni walio huru na moto; hakuna uwezo wala nguvu isipokuwa kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), na Atakayo Allaah huwa na Asiyoyataka hayawi.

Na miongoni mwa yanayopokelewa mwezi wa Ramadhaan ni Muislamu kuangalia vizuri mambo mahususi ya mwezi huu na fadhila zake, na ajifunze pia anayotakiwa kuyafanya katika mwezi huu, kama vile kufunga Swawm na kusimama usikuwa kuswali, na kujikumbusha hukumu zinazohusiana nao. Aangalie pia faida ya Swawm na manufaa yake na yaliyomo ndani yake kuhusu mazingatio na mafunzo na mawaidha. Na pia azingatie fadhila za kusimama usiku kuswali (Qiyaamul-Layal; tarawiyh, tahajjud) na ujira mkubwa Aliouandaa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa ajili ya wenye kusimama ndani yake. Imethibiti  katika Swahiyh mbili kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

مَنْ صَامَ رَمَضَانَ إِيمَانًا وَاحْتِسَابًا غُفِرَ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ وَمَنْ قَامَ لَيْلَةَ الْقَدْرِ إِيمَانًا وَاحْتِسَابًا غُفِرَ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ

Atakaeyfunga Swawm Ramadhaan kwa imani na kutaraji malipo ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia. Na Atakayesimama usiku wa ‘Laylatul-Qadr’ kwa imani na kutaraji malipo ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia.

Miongoni mwa yanayopokewa mwezi huu mtukufu ni Muislamu kufanya juhudi ya nafsi kwa kutengeneza moyo wake na kuondoa uchafu wote uliokuwemo humo kama vile mafundo, uhasidi, au chuki na mengine yasiyokuwa hayo.

Enyi waja wa Allaah! Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

  صَوْمُ شَهْرِ الصَّبْرِ وَثَلَاثَةِ أَيَّامٍ مِنْ كُلِّ شَهْرٍ يُذْهِبْنَ  وَحَرَ الصَّدْرِ

Swawm katika mwezi wa subira na siku tatu kila mwezi (Ayaamul-Biydhw – masiku meupe) huondosha chuki katika nyoyo.

Hakika ndani ya nyoyo kuna uhasidi, chuki na hikdi, basi unapokuja msimu huu wa baraka, inakuwa fursa tukufu ya kuondoa yote yaliyo ndani ya moyo kama vile mafundo au hikdi, au hasadi. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 لَا تَحَاسَدُوا وَلَا تَنَاجَشُوا وَلَا تَبَاغَضُوا وَلَا تَدَابَرُوا وَلَا يَبِعْ بَعْضُكُمْ عَلَى بَيْعِ بَعْضٍ وَكُونُوا عِبَادَ اللَّهِ إِخْوَانًا  

Msihusudiane, wala msiongezeane bei pasi na kuwa na haja ya kununua wala msichukiane wala msipeane nyongo wala wasinunue baadhi yenu kilichokwisha kuuziwa wenzenu, lakini kuweni enyi waja wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ndugu” (al-Bukhaariy, Muslim na Abu Daawuud)

Hakika kuingia Ramadhaan ni fursa yenye baraka kwa kusafisha nafsi na nyoyo na kujumuisha maneno kwenye kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa  Waislamu wote kuelekea kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) hali ya kuwa watiifu kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), wakielekeza ibada yake huku wakijiweka mbali na yenye kumuudhi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Asiyoyapenda.

Namuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atufikishe sote kwenye mwezi wa Ramadhaan na Atusaidie juu ya kufunga na kusimama, na Atengeneze mambo yetu, na Aunganishe nyoyo zetu, na Atuongoze njia zilizo sawa, na Atutoe kwenye kiza na kutuingiza kwenye nuru, na Atufanye miongoni mwa waja Wake wenye taqwa na vipenzi Vyake waliokurubishwa ambao hawana hofu wala hawahuzuniki.

 

Chanzo:  http://al-badr.net/detail/R8U25Lf9Gbrk

Imefasiriwa na: Alhidaaya.com

 

Share