01-Swalaah - Kuwajibika Na Fadhila Zake: Maana Ya Swalah Na Kuwajibika Kwake

Swalaah – Kuwajibika Na Fadhila Zake

 

01- Kuwajibika Na Fadhila Zake: Maana Ya Swalaah Na Kuwajibika Kwake

 

Alhidaaya.com

 

 

Maana Ya Swalaah Kilugha:

           

 

Ni du'aa kama Anavyosema  Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا وَصَلِّ عَلَيْهِمْ ۖ إِنَّ صَلَاتَكَ سَكَنٌ لَّهُمْ ۗ وَاللَّـهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ﴿١٠٣﴾

Chukua (ee Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika mali zao Swadaqah, uwatakase na ziwazidishie kwazo na waombee du’aa (na maghfirah). Hakika du’aa yako ni utulivu kwao. Allaah ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote. [At-Tawbah: 103]

 

 Hadiyth ifuatayo inathibitisha pia maana hiyo:
 

عن أبي هريرة -رضي الله عنه- قال: قال رسول الله -صلى الله عليه وسلم: ((إذا دعي أحدكم فليجب فإن كان صائمًا فليصلِّ و إن كان مفطرًا فليطعم)) أخرجه مسلم         

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Akialikwa mmoja wenu aitike (mwaliko), ikiwa amefunga  aombe du'aa (kwa waliomualika), akiwa hakufunga basi ale (chakula))) [Muslim] 

 

Yaani: Awaombee du'aa ya maghfirah, baraka na kheri)

 

Swalaah kutoka kwa Allaah ni Himdi na kutoka kwa Malaika ni du'aa kama Anavyosema:

 

إِنَّ اللَّـهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ ۚ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا ﴿٥٦﴾

56. Hakika Allaah na Malaika Wake wanamswalia Nabiy. Enyi walioamini mswalieni na msalimieni kwa mamkizi ya amani na kwa tasliymaa [Al-Ahzaab: 56]

 

Abu 'Alyah amesema: Swalaah ya Allaah ni kumsifu mja kwa Malaika Wake na Swalaah ya Malaika ni du'aa.

 

Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) amesema: "Wanawaswalia" maana wanawabarikia"  

 

Vile vile Swalaah kutoka kwa Allaah ni maghfirah au Baraka. Swalaah kwa maana ya maghfirah nikutokana na kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ ﴿١٥٧﴾

Hao zitakuwa juu yao Barakah kutoka kwa Rabb wao na rahmah, na hao ndio wenye kuongoka. [Al-Baqarah: 157]

 

Na kama ilivyosimuliwa kutoka kwa Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa alisema:

اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى آل أَبِي أَوْفَى

‘Allahumma Swalli ‘alaa Aali Abi Awfiy’ Akimaanisha ‘Ee Allaah wasamehe jamaa wa Abu Awfiy’.  

 

Hivyo hapa Swalaah ina maana ya maghfirah.
 

 

Maana Swalaah Kishariy'ah

 

Ni kumuabudu Allaah kwa kauli na vitendo maalumu  vinavyoanza na Takbiyrah (Allaahu Akbar) na kumalizika na Tasliym (kutoa salaam).

 

Na imeitwa Swalaah kwa sababu inahusiana na du'aa katika kumuabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) tunaposimama, tunaporukuu, tunaposujudu na tunapokaa, hivyo Swalaah nzima ni du'aa.

 

 

Hukumu Ya Swalaah:

 

Swalaah ni fardhi kwa kila Muislamu mwenye akili timamu, aliyebaleghe kutokana na dalili kutoka katika Qur-aan:

 

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَۚ وَذَٰلِكَ دِينُ الْقَيِّمَةِ ﴿٥﴾

Na hawakuamrishwa isipokuwa wamwabudu Allaah wenye kumtakasia Dini, wenye kujiengua na upotofu kuelemea Dini ya haki na wasimamishe Swalaah na watoe Zakaah; na hiyo ndiyo Dini iliyosimama imara. [Al-Bayyinah: 5]

إِنَّ الصَّلَاةَ كَانَتْ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ كِتَابًا مَّوْقُوتًا ﴿١٠٣﴾

hakika Swalaah kwa Waumini ni fardhi iliyowekwa nyakati maalumu [An-Nisaa: 103]

 
 

Ama katika Sunnah ni kauli yake Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipomtuma Mu'aadh Bin Jabal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kupeleka risala Yemen kwa kumwambia: ((…na wafundishe kwamba Allaah Amewafaridhisha Swalaah tano kila siku…)) [Al-Bukhaariy Na Muslim]

 

Vile vile,

 

  عبدالله بن عمر قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم (( بُنِـيَ  الإِسْلاَمُ علـى خَمْسٍ: شَهادَةِ أنْ لا إِلٰهَ إلا الله وأنَّ مُـحَمَّداً رَسُولُ الله وإِقامِ الصَّلاَةِ وإِيتاءِ الزَّكاةِ وَحَجِّ البَـيْتِ وَصَوْمِ رَمَضَانَ((  البخاري

Kutoka kwa 'Abdullaah ibn 'Umar ambaye amesema: Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Uislamu umejengeka kwa matano; Kushuhudia (na kukiri kwa moyo)  kwamba hakuna muabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Rasuli wa Allaah na kuswali (Swalaah tano), kutoa Zakaah, kuhiji katika Nyumba (Makkah) na kufunga (mwezi wa) Ramadhwaan)) [Al-Bukhaariy]

 

Kuna Aayah na Hadiyth nyingi zinazothibitisha kuwajibika kwa Swalaah. Ama mwanamke mwenye hedhi na aliye katika nifaas hawawajibiki kuswali kutokana na kauli ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  

 

  أليس إذا حاضت المرأة لم تصل ولم تصم ؟  -متفق       

((Kwani sio kweli kwamba mwanamke anapokuwa katika hedhi haswali wala hafungi?)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

 

Share