03-Wewe Pekee Tunakuabudu: Fadhila Za Du’aa

 

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

Wewe Pekee Tunakuabudu Na Wewe Pekee Tunakuomba Msaada.

 

03-Fadhila Za Du’aa

 

 

 

Fadhila za du’aa ni nyingi mno, zifuatazo ni baadhi ya fadhila zake:

 

 

1- Du’aa Ni ‘Ibaadah:

 

Juu ya kuwa ‘ibaadah zetu hazimfai wala kumnufaisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) chochote, lakini Yeye (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anatuhimiza tumkabili kumuomba:

 

عَنِ النُّعْمَانِ بْنِ بَشِيرٍ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) فِي قَوْلِهِ ((وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ)) قَالَ: ((الدُّعَاءُ هُوَ الْعِبَادَةُ)) وَقَرَأَ ((وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ)) إِلَى قَوْلِهِ: ((دَاخِرِينَ))

Amesimulia Nu’maan bin Bashiyr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika kauli yake [Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa] ((Na Rabb wenu Amesema: “Niombeni, Nitakuitikieni. ) Amesema: ((Du’aa ni ‘ibaadah)) kisha akasoma: ((Na Rabb wenu Amesema: “Niombeni, Nitakuitikieni. )) mpaka kauli Yake: ((daakhiriyn)) [Abu Daawuwd, At-Tirmidhiy, Ibn Maajah, Ahmad – Hadiyth Hasan Swahiyh]

 

 

 

2- Du’aa Ni ‘Amali Tukufu Kabisa:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) عَنْ النَّبِيِّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ: ((لَيْسَ شَيْءٌ أَكْرَمَ عَلَى اللَّهِ تَعَالَى مِنْ الدُّعَاءِ))  

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakuna kitu kitukufu mbele ya Allaah kama du’aa))  [At-Tirmidhiy, Ibn Maajah, Ahmad, na amesema At-Tirmidhiy: Hasan Ghariyb na ameisahihisha Ibn Hibbaan, Al-Haakim na ameipa muwafaka Adh-Dhahaabiy na ameipa daraja ya Hasan Al-Albaaniy katika Swahiyh Adab Al-Mufrad] 

 

 

 

3- Du’aa Inadhihirisha Tawhiyd ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

Mja anapomkabili Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa kumuomba du’aa, huwa anamkabili kwa aina zote za Tawhiyd; kwani huwa ameamini kwamba Yeye Allaah ni Rabb, Mola, Muumbaji, Mtoaji rizki, Mwendeshaji na Msimamizi wa mambo, Mfishaji na Mwenye kuhuisha; nayo ni Tawhiyd Ar-Rubuwbiyyah. Na kwamba Yeye Pekee Ndiye Anayestahiki kuabudiwa kwa haki na kuombwa (Tawhiyd Al-Uluwhiyyah), na kwamba Yeye Ndiye Mwenye Majina Mazuri kabisa na Sifa Zake (Tawhiyd Al-Asmaa wasw-Swifaat).

 

 

 

4- Kuomba Du’aa Ni Kujikurubisha Na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kama Anavyosema:

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ

Na watakapokuuliza waja Wangu kuhusu Mimi, basi Mimi ni Niko karibu (kwa ujuzi);  [Al-Baqarah: 186]

 

 

 

5- Kuomba Du’aa Ni Sifa mojawapo ya ‘Ibaadur-Rahmaan’ (Waja wa Mwingi wa Rahmah)   

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ametaja baadhi ya sifa ambazo Amezihusisha na waja Wake aliowaita ‘Ibaadur-Rahmaan katika Suwratul-Furqaan.  Miongoni mwa sifa hizo ni kuomba du’aa mbili zifuatazo:

وَالَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَا اصْرِفْ عَنَّا عَذَابَ جَهَنَّمَ ۖ إِنَّ عَذَابَهَا كَانَ غَرَامًا ﴿٦٥﴾

Na wale wanaosema: “Rabb wetu! Tuepushe adhabu ya Jahannam. Hakika adhabu yake ni yenye kugandamana daima; isiyomwacha mtu.” [Al-Furqaan: 65]

 

وَالَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَا هَبْ لَنَا مِنْ أَزْوَاجِنَا وَذُرِّيَّاتِنَا قُرَّةَ أَعْيُنٍ وَاجْعَلْنَا لِلْمُتَّقِينَ إِمَامًا ﴿٧٤﴾

Na wale wanaosema: “Rabb wetu! Tutunukie katika wake zetu na dhuria wetu viburudisho vya macho yetu, na Tujaalie kuwa waongozi kwa wenye taqwa.  [Al-Furqaan: 74]

 

 

 

6- Kuomba Du’aa Ni Miongoni Mwa Sifa Za Watu Wa Jannah:

 

 

Waumini watakapokuwa Jannah hawatakuwa na la kuwashughulisha kama wanavyoshughulika duniani, bali ni starehe tupu na maombi yao na kauli zao zitakuwa ni kumtakasa, kumtukuza na kumhimidi Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kama Anavyosema:

 

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ يَهْدِيهِمْ رَبُّهُم بِإِيمَانِهِمْ ۖتَجْرِي مِن تَحْتِهِمُ الْأَنْهَارُ فِي جَنَّاتِ النَّعِيمِ﴿٩﴾

Hakika wale walioamini na wakatenda mema, Rabb wao Atawaongoza kwa iymaan zao. Zitapita chini yao mito katika Jannaat za neema.

 

 

دَعْوَاهُمْ فِيهَا سُبْحَانَكَ اللَّـهُمَّ وَتَحِيَّتُهُمْ فِيهَا سَلَامٌ ۚ وَآخِرُ دَعْوَاهُمْ أَنِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ﴿١٠﴾

Wito wao humo ni: “Utakasifu ni Wako ee Allaah.” Na maamkizi yao humo ni “Salaamun!” Na wito wao wa mwisho ni “AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah) Rabb wa walimwengu.” [Yuwnus: 9 -10]

 

 

 

7- Du’aa Ni Sababu Ya Kufunguliwa Milango Ya Rahmah Na Sababu Ya Kuondolewa Na Balaa Kabla Ya Kuteremka:

 

عَنْ ابْنِ عُمَرَ (رضي الله عنه)  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((مَنْ فُتِحَ لَهُ مِنْكُمْ بَابُ الدُّعَاءِ فُتِحَتْ لَهُ أَبْوَابُ الرَّحْمَةِ وَمَا سُئِلَ اللَّهُ شَيْئًا يَعْنِي أَحَبَّ إِلَيْهِ مِنْ أَنْ يُسْأَلَ الْعَافِيَةَ)) وَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((إِنَّ الدُّعَاءَ يَنْفَعُ مِمَّا نَزَلَ وَمِمَّا لَمْ يَنْزِلْ فَعَلَيْكُمْ عِبَادَ اللَّهِ بِالدُّعَاءِ))  

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayefunguliwa mmoja wenu mlango wa du’aa, amefunguliwa mlango wa Rahmah, na Akipendacho Allaah Zaidi kuombwa ni al-‘aafiyah (afya, siha, amani, hifadhi n.k))  Na akasema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Hakika du’aa inanufaisha (misiba) inayoteremka na isiyoteremka, hivyo basi juu yenu waja wa Allaah kwa kuomba du’aa)) [At-Tirmidhiy na ameipa daraja ya Hasan Shaykh Al-Albaaniy katika Swahiyh Al-Jaami’]

 

8- Du’aa Inaweza Kubadilisha Qadar (Majaaliwa):

 

Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

عَنْ سَلْمَانَ (رضي الله عنه)  قَالَ:  قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ):  ((لاَ يَرُدُّ الْقَضَاءَ إِلاَّ الدُّعَاءُ ولاَ يَزِيدُ فِي الْعُمْرِ إِلاَّ الْبِرُّ))  

Kutoka kwa Salmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hairudishi Qadhwaa ila du’aa na haizidishi umri ila wema)) [At-Tirmidhiy]

 

Kwa hiyo du’aa inabadilisha yaliyoandikwa katika Sahifa za Malaika wawili; wa kulia na kushoto kama vile ilivyothibiti katika kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

يَمْحُو اللَّـهُ مَا يَشَاءُ وَيُثْبِتُ ۖ وَعِندَهُ أُمُّ الْكِتَابِ﴿٣٩﴾

Allaah Anafuta yale Ayatakayo na Anathibitisha (Ayatakayo), na Kwake kiko Mama wa Kitabu. [Ar-Ra’d: 39]

 

Kwa maana mtu akifanya jema, basi jema hilo linafuta dhambi kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَأَقِمِ الصَّلَاةَ طَرَفَيِ النَّهَارِ وَزُلَفًا مِّنَ اللَّيْلِ ۚ إِنَّ الْحَسَنَاتِ يُذْهِبْنَ السَّيِّئَاتِ ۚ ذَٰلِكَ ذِكْرَىٰ لِلذَّاكِرِينَ﴿١١٤﴾

Na simamisha Swalaah katika ncha mbili za mchana na sehemu ya kwanza ya usiku; hakika mema yanaondosha maovu. Hivyo ni ukumbusho kwa wanaokumbuka. [Huwd: 114]

 

Au mtu akitubia na akaomba maghfirah basi maovu yake hubadilishwa kwa mema yake kama ilivyothibiti katika kauli za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَالَّذِينَ لَا يَدْعُونَ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ وَلَا يَقْتُلُونَ النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّـهُ إِلَّا بِالْحَقِّ وَلَا يَزْنُونَ ۚ وَمَن يَفْعَلْ ذَٰلِكَ يَلْقَ أَثَامًا ﴿٦٨﴾

Na wale ambao hawaombi pamoja na Allaah mwabudiwa mwengine na wala hawaui nafsi ambayo Allaah Ameiharamisha isipokuwa kwa haki, na wala hawazini. Na atakayefanya hivyo atakutana na adhabu.

 

يُضَاعَفْ لَهُ الْعَذَابُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَيَخْلُدْ فِيهِ مُهَانًا ﴿٦٩﴾

Ataongezewa adhabu maradufu Siku ya Qiyaamah, na mwenye kudumu humo akiwa amedhalilika.

 

 

إِلَّا مَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ عَمَلًا صَالِحًا فَأُولَـٰئِكَ يُبَدِّلُ اللَّـهُ سَيِّئَاتِهِمْ حَسَنَاتٍ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٧٠﴾

Isipokuwa yule aliyetubu na akaamini na akatenda ‘amali njema; basi hao Allaah Atawabadilishia maovu yao kuwa mema. Na Allaah daima ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu.

 

وَمَن تَابَ وَعَمِلَ صَالِحًا فَإِنَّهُ يَتُوبُ إِلَى اللَّـهِ مَتَابًا ﴿٧١﴾

Na atakayetubu na akatenda mema, basi hakika yeye anatubia kwa Allaah tawbah ya kweli. [Al-Furqaan: 68-71]

 

Na katika kuhusiana na du’aa, mfano mtu amejiombea du’aa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amghufurie madhambi yake na kwa kutubia kwake, basi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) humghufuria madhambi yake. Au alimtendea wema fulani nduguye Muumini kisha huyu ndugu akamuombea du’aa njema kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) amghufurie dhambi zake au amjaalie kheri fulani. Basi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akaamrisha Malaika wayafute maovu na kuthibitisha mema. Lakini Allaah ('Azza wa Jalla) ni Mjuzi wa yote hayo kabla ya hapo, kwa kuwa imeshaandikwa katika Lawhum-Mahfuwdhw (Ubao Uliohifadhiwa) kabla ya kuumbwa mbingu na ardhi na viliomo ndani yake pindi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alipoiamrisha kalamu iandike Qadhwaa na Qadar. Na hivyo basi yaliyoandikwa humo katika Lawhun-Mahfuwdhw hayafutiki kamwe, kwa sababu hiyo ni Ilmu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Kujua Kwake; kwamba mja atafanya wema fulani, siku kadhaa kisha Yeye Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atamuamrisha Malaika afute na athibitishe katika Sahifa za Malaika wawili.  Na hii ndio ‘Aqiydah Sahihi kuamini kuwa Allaah Ameandika katika Lawhun Mahfuwdhw yote yaliyotokea na yatakayotokea mpaka Siku ya Qiyaamah.

 

 

 

9- Kuomba Du’aa Ni Kuepushwa Na Moto  

 

Waumini wenye taqwa watakapoepushwa na Moto huko Aakhirah, watakabiliana na wenzao na kuulizana sababu za kuingizwa kwao Jannah, na kuomba du’aa ni mojawapo wa sababu hizo; Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

وَأَقْبَلَ بَعْضُهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ يَتَسَاءَلُونَ ﴿٢٥﴾

Na watakabiliana baadhi yao kwa wengineo wakiulizana.

 

قَالُوا إِنَّا كُنَّا قَبْلُ فِي أَهْلِنَا مُشْفِقِينَ ﴿٢٦﴾

Watasema: “Hakika sisi tulikuwa kabla kwenye ahli zetu wenye kuogopa

 

 

فَمَنَّ اللَّـهُ عَلَيْنَا وَوَقَانَا عَذَابَ السَّمُومِ ﴿٢٧﴾

Basi Allaah Akatufadhilisha, na Akatuokoa na adhabu ya moto unaobabua.

 

 

إِنَّا كُنَّا مِن قَبْلُ نَدْعُوهُ ۖ إِنَّهُ هُوَ الْبَرُّ الرَّحِيمُ ﴿٢٨﴾

Hakika sisi tulikuwa kabla Tunamuomba Yeye Pekee, hakika yeye Ndiye Mwingi huruma na fadhila, Mwenye kurehemu.” [Atw-Twuwr: 25- 28]

 

 

Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alipokuwa akisoma Aayah hizi, akiomba du’aa:

"اللَّهُمَّ مُنَّ عَلَيْنَا وَقِنَا عَذَاب السَّمُوم إِنَّك أَنْتَ الْبَرّ الرَّحِيم"

‘Ee Allaah, Tufanyie fadhila, na Tuepushe na adhabu Moto unaobabua, hakika Wewe ni Al-Barrur-Rahiym (Mwingi huruma na fadhila - Mwenye kurehemu).” [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

 

 

10- Kuomba Du’aa Ni Kufuata Sunnah Za Manabiy, Na Nyendo Za Salaf.  

 

Kuhusu Manabiy, Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwamba kuomba du’aa ilikuwa ni shani yao. Manabiy walipokosea walirudi kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kuomba maghfirah na msamaha. Iliwasibu Manabiy balaa, maudhi, madhara na shari za kila aina kutoka kaumu zao baada ya kuwalingania Ujumbe wa Allaah. Walipotaka nusura, walitumia du’aa kuwa ni ufumbuzi, utatuzi wa mashakili yao wapate faraja.

Mfano kuhusu Nuhw (‘Alayhis-salaam) aliposhindwa kabisa baada na kaumu yake:

كَذَّبَتْ قَبْلَهُمْ قَوْمُ نُوحٍ فَكَذَّبُوا عَبْدَنَا وَقَالُوا مَجْنُونٌ وَازْدُجِرَ ﴿٩﴾

Walikadhibisha kabla yao kaumu ya Nuwh, wakamkadhibisha mja Wetu, wakasema: “Majnuni.” Na akakaripiwa.

فَدَعَا رَبَّهُ أَنِّي مَغْلُوبٌ فَانتَصِرْ ﴿١٠﴾

Basi akamwita Rabb wake kwamba: “Hakika mimi nimeshindwa nguvu basi Nusuru.” [Al-Qamar: 9-10]

 

 

Mfano wa Nabiy Zakariyyah alipotamani mwana ili amrithi katika Unabiy:

 

 وَزَكَرِيَّا إِذْ نَادَىٰ رَبَّهُ رَبِّ لَا تَذَرْنِي فَرْدًا وَأَنتَ خَيْرُ الْوَارِثِينَ ﴿٨٩﴾

Na Zakariyyaa alipomwita Rabb wake: “Rabb wangu! Usiniache pekee; Nawe Ndiye Mbora wa wenye kurithi.”

 

فَاسْتَجَبْنَا لَهُ وَوَهَبْنَا لَهُ يَحْيَىٰ وَأَصْلَحْنَا لَهُ زَوْجَهُ ۚ إِنَّهُمْ كَانُوا يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَيَدْعُونَنَا رَغَبًا وَرَهَبًا ۖ وَكَانُوا لَنَا خَاشِعِينَ ﴿٩٠﴾

Basi Tukamuitikia na Tukamtunukia Yahyaa, na Tukamtengenezea mke wake. Hakika wao walikuwa wakikimbilia katika mambo ya kheri, na wakituomba kwa raghba na khofu, na walikuwa wenye kutunyenyekea. [Al-Anbiyaa: 89-90]

 

Na mifano mingineyo mbali mbali ya du’aa za Manabiy katika katika Qur-aan. [Rejea mlango wa Du’aa katika Qur-aan]

 

Ilikuwa pia ni nyendo za Salafus-Swaalih ambao wakimuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa unyenyekevu nyakati za usiku:

 

إِنَّمَا يُؤْمِنُ بِآيَاتِنَا الَّذِينَ إِذَا ذُكِّرُوا بِهَا خَرُّوا سُجَّدًا وَسَبَّحُوا بِحَمْدِ رَبِّهِمْ وَهُمْ لَا يَسْتَكْبِرُونَ ۩﴿١٥﴾

Hakika wanaamini Aayaat Zetu wale wanapokumbushwa nazo huporomoka kusujudu, na wakasabbih kwa Himidi za Rabb wao, nao hawatakabari.

 

تَتَجَافَىٰ جُنُوبُهُمْ عَنِ الْمَضَاجِعِ يَدْعُونَ رَبَّهُمْ خَوْفًا وَطَمَعًا وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ ﴿١٦﴾

Mbavu zao zinatengana na vitanda, wanamuomba Rabb wao kwa khofu na matumaini, na katika yale Tuliyowaruzuku wanatoa. [As-Sajdah: 15-16]

 

 

 

11- Kuomba Du’aa Ni Amali Mojawapo Itendwayo Na Malaika Kuwaombea Waumin:

 

الَّذِينَ يَحْمِلُونَ الْعَرْشَ وَمَنْ حَوْلَهُ يُسَبِّحُونَ بِحَمْدِ رَبِّهِمْ وَيُؤْمِنُونَ بِهِ وَيَسْتَغْفِرُونَ لِلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا وَسِعْتَ كُلَّ شَيْءٍ رَّحْمَةً وَعِلْمًا فَاغْفِرْ لِلَّذِينَ تَابُوا وَاتَّبَعُوا سَبِيلَكَ وَقِهِمْ عَذَابَ الْجَحِيمِ﴿٧﴾

 (Malaika) Ambao wanabeba ‘Arsh na walio pembezoni mwake, wanasabbih kwa Himidi za Rabb wao, na wanamwamini; na wanawaombea maghfirah wale walioamini: “Rabb wetu! Umekienea kila kitu kwa rahmah na ujuzi, basi waghufurie wale waliotubu, na wakafuata njia Yako, na wakinge na adhabu ya moto uwakao vikali mno.

 

رَبَّنَا وَأَدْخِلْهُمْ جَنَّاتِ عَدْنٍ الَّتِي وَعَدتَّهُمْ وَمَن صَلَحَ مِنْ آبَائِهِمْ وَأَزْوَاجِهِمْ وَذُرِّيَّاتِهِمْ ۚ إِنَّكَ أَنتَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ﴿٨﴾

 “Rabb wetu! Waingize Jannaat za kudumu milele ambazo Umewaahidi, pamoja na waliotengenea miongoni mwa baba zao, na wake zao, na dhuria wao.  Hakika Wewe Ndiye Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote.

 

وَقِهِمُ السَّيِّئَاتِ ۚ وَمَن تَقِ السَّيِّئَاتِ يَوْمَئِذٍ فَقَدْ رَحِمْتَهُ ۚ وَذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ﴿٩﴾

 “Na wakinge maovu, kwani Unayemkinga na maovu Siku hiyo, basi kwa yakini Umemrehemu. Na huko ndiko kufuzu adhimu. [Ghaafir: 7-9]

 

 

12- Kuomba Du’aa Ni Dalili Ya Wenye Akili Wanaothibitisha Tawhiyd

 

Wenye akili hutafakari uumbaji wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) wa mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake. Hutafakari pia jinsi Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anavyoendesha mambo yote ya ulimwengu kwa ajili ya walimwengu.  Hapo hutambua utukufu na uwezo wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), kisha huomba du’aa. Basi hao Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amewasifu kuwa ni dalili ya ‘wenye akili’:

 

إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لَآيَاتٍ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ ﴿١٩٠﴾ 

Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi, na mabadiliko ya mfuatano wa usiku na mchana; bila shaka ni Aayaat (ishara, zingatio) kwa wenye akili.

 

الَّذِينَ يَذْكُرُونَ اللَّـهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِهِمْ وَيَتَفَكَّرُونَ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَـٰذَا بَاطِلًا سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النَّارِ ﴿١٩١﴾ 

Ambao wanamdhukuru Allaah kwa kusimama  na kwa kukaa na kwa kulala ubavuni mwao na wanatafakari katika kuumbwa mbingu na ardhi (wakisema): “Rabb wetu, Hukuumba haya bure, Subhaanak! (Utakasifu ni Wako) tukinge na adhabu ya moto.”

 

 

رَبَّنَا إِنَّكَ مَن تُدْخِلِ النَّارَ فَقَدْ أَخْزَيْتَهُ ۖ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ ﴿١٩٢﴾

 “Rabb wetu, hakika Umuingizaye motoni, kwa yakini Umemhizi. Na madhalimu hawana yeyote mwenye kuwanusuru.”

 

 

رَّبَّنَا إِنَّنَا سَمِعْنَا مُنَادِيًا يُنَادِي لِلْإِيمَانِ أَنْ آمِنُوا بِرَبِّكُمْ فَآمَنَّا ۚ رَبَّنَا فَاغْفِرْ لَنَا ذُنُوبَنَا وَكَفِّرْ عَنَّا سَيِّئَاتِنَا وَتَوَفَّنَا مَعَ الْأَبْرَارِ ﴿١٩٣﴾

 “Rabb wetu, hakika sisi tumemsikia mwitaji anaita kwenye iymaan kwamba ‘mwaminini Rabb wenu’ basi tukaamini.  Rabb wetu, Tughufurie madhambi yetu na Tufutie makosa yetu na Tufishe pamoja na Waumini wema.”

 

 رَبَّنَا وَآتِنَا مَا وَعَدتَّنَا عَلَىٰ رُسُلِكَ وَلَا تُخْزِنَا يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ إِنَّكَ لَا تُخْلِفُ الْمِيعَادَ ﴿١٩٤﴾

 “Rabb wetu na Tupe Uliyotuahidi kupitia Rusuli Wako, wala Usituhizi Siku ya Qiyaamah; hakika Wewe Huendi kinyume na miadi.” [Aal-‘Imraan: 190-194]

 

 

Fadhila zao Waumini hao wenye kuomba du’aa hizo, ni kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amewatakabalia du’aa zao, na Amewaghufuria maovu yao, na Amewaahidi mengi mazuri pamoja na kuwaingiza katika Jannah Yake yenye neema  [Aal-‘Imraan: 195-199]

 

 

 

Share