Kibarua Cha Kufanyia Kazi Sehemu Za Ma'asi

 

SWALI

Assalaama-alaykum,

Nnaomba kuuliza suala langu ambalo linahusika na uajiri. Mimi nnafanya kazi kama ni mjenzi au kibarua na mara nyigi hupangiwa tu kazi nikaambiwa nenda pahali fulani kuna kazi fulani. Sasa suali langu ni kuwa je! Iwapo nitapangiwa kufanya kazi kama vile kujenga Hoteli ambayo itakuja kupelekea watu kumuasi M.Mungu au kujenga Baa ambayo watu watakuja kunywa ulevi au Night club, Je! itanibidi niende kwa vile natafuta rizki? Na vile mimi sitashiriki kuyatenda hayo au haitonifaa kabisa kuingiza nguvu zangu katika majengo hayo?

Wabillahi tawfik.   

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Ni muhimu tufahamu ya kwamba haifai kwa Muislamu kusaidia katika ujenzi wa sehemu ambazo zitaleta uadui, uchafu na maasiya katika ardhi. Allaah anatuambia:

“Na saidianeni katika wema na uchamngu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Na mcheni Allaah. Hakika Allaah ni Mkali wa kuadhibu” (5: 2).

Inavyotakiwa ni umueleze muajiri wako kuhusu hilo jambo kuwa kwa mujibu wa Dini yako hufai kufanya hivyo. Na waajiri wengine ni wenye kuelewa na anaweza kukupeleka sehemu nyingine. Na hii kwako itakuwa umefanya Da‘wah. Ikiwa hakukubali utaacha nayo na utatafuta kibaruwa sehemu nyengine na kwa kuwa umeacha kwa ajili ya Allah kwenda katika haramu Allah Atakutolea njia nyengine ya kupata riziki yako ya halali. Allaah Anasema:

 

“Na anayemcha Allaah, Humtengezea njia ya kutokea. Na Humruzuku kwa jiha asiyotazamia. Na anayemtegemea Allaah  Yeye Humtosha. Hakika Allaah  Anatimiza amri Yake. Allaah  Kajaalia kila kitu na kipimo chake” (65: 2 – 3).

Na Allah Anajua zaidi

 

 

Share