05-Wewe Pekee Tunakuabudu: Adabu Za Kuomba Du'aa

 

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

Wewe Pekee Tunakuabudu Na Wewe Pekee Tunakuomba Msaada

 

05-Adabu Za Kuomba Du'aa

 

 

 Zifatazo ni adabu za kuomba du’aa na dalili zake:

 

 

1- Kutia Wudhuu  

 

Kutoka kwa Abu Muwsaa (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba, wakati Abu ‘Aamir (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliporushiwa mshale katika shingo yake alimuendea akamuomba amchopoe mshale. Akamchopoa kisha akamuomba amuendee Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili amuombee. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akachukua wudhuu, kisha akanyanyua mikono yake hadi zikaonekana kwapa zake, kisha akaomba:

((اللَّهُمَّ اغْفِرْ لِعُبَيْدٍ أَبِي عَامِرٍ))

((Ee Allaah, Mghufurie ‘Ubayd Abiy ‘Aamir)) [Al-Bukhaariy (6383), Muslim (2498), Ibn Hibbaan katika Swahiyh yake (7198)]

 

 

 

2- Kuelekea Qiblah

 

Imethibitika mara kadhaa kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  alikuwa akielekea Qiblah alipoomba du’aa; mfano alipoomba du’aa wakati wa Hajj; alipokuwa baina ya Swafaa na Marwah, baada ya kurusha vijiwe katika Jamaraat, katika Mash’aril-Haraam, au alipoomba dhidi ya makafiri katika vita vya Badr n.k.

 

 

 

3- Kuanza Kwa Kumtukuza Allaah Na Kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

 

 

عن فَضَالَةَ بْنَ عُبَيْدٍ (رضي الله عنه) يَقُولُ: سَمِعَ النَّبِيُّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) رَجُلاً يَدْعُو فِي صَلاَتِهِ فَلَمْ يُصَلِّ عَلَى النَّبِيِّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) فَقَالَ النَّبِيُّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ):  ((عَجِلَ هَذَا))  ثُمَّ دَعَاهُ فَقَالَ لَهُ أَوْ لِغَيْرِهِ: ((إِذَا صَلَّى أَحَدُكُمْ فَلْيَبْدَأْ بِتَحْمِيدِ اللَّهِ وَالثَّنَاءِ عَلَيْهِ ثُمَّ لْيُصَلِّ عَلَى النَّبِيِّ ثُمَّ لْيَدْعُ بَعْدُ بِمَا شَاءَ))  

Kutoka kwa Fadhwaalah bin ‘Ubayd (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimsikia mtu akiomba katika du’aa yake bila ya kumswalia yeye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Akasema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Ameharakisha huyu)) kisha akamwita na kumwambia au kumwambia mwingine: ((Anapoomba mmoja wenu basi aanze kwa Kumhimidi Allaah, na kumtukuza kisha amswalie Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) halafu aombe anachotaka)) [Abu Daawuwd, At-Tirmidhiy, Ahmad]

 

Tunapoanza kuswali, tunaanza kusoma Suwratul-Faatihah ambayo ndani yake mna du’aa. Bila ya Suwrah hii tukufu Swalaah huwa haisihi. Tunaisoma mara kumi na saba kwa siku. Katika Suwrah hiyo, tunaanza kwanza kwa kumhimidi, kumsifu na kumtukuza Allaah Naye hutujibu hapo hapo, kisha tunaendelea kumuomba Atuongoze katika njia iliyonyooka. Imesimuliwa katika Hadiythul-Qudsiy:

 

 قال رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم): ((قَالَ اللَّهُ تَعَالَى: قَسَمْتُ الصَّلاَةَ بَيْنِي وَبَيْنَ عَبْدِي نِصْفَيْنِ, وَلِعَبْدِي مَا سَأَلَ. فَإِذَا قَالَ الْعَبْدُ: الْحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ,  قَالَ اللَّهُ تَعَالَى: حَمِدَنِي عَبْدِي. وَإِذَا قَالَ: الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ, قَالَ اللَّهُ تَعَالَى: أَثْنَى عَلَيَّ عَبْدِي. وَإِذَا قَالَ: مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ, قَالَ: مَجَّدَنِي عَبْدِي, فَإِذَا قَالَ: إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ, قَالَ: هَذَا بَيْنِي وَبَيْنَ عَبْدِي وَلِعَبْدِي مَا سَأَلَ. فَإِذَا قَالَ: اهْدِنَا الصِّرَاطَ الْمُسْتَقِيمَ صِرَاطَ الَّذِينَ أَنْعَمْتَ عَلَيْهِمْ غَيْرِ الْمَغْضُوبِ عَلَيْهِمْ ولاَ الضَّالِّينَ قَالَ: هَذَا لِعَبْدِي وَلِعَبْدِي مَا سَأَل))   

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Ta’aala Amesema:  Nimegawa Swalaah baina Yangu na mja Wangu sehemu mbili na mja Wangu atapata alichokiomba. Basi mja anaposema:  “Himidi zote Anastahiki Allaah Rabb wa walimwengu.”, Allaah Ta’aalaa Husema: “Mja Wangu amenisifu”. Mja akisema: " Mwingi wa Rahmah,  Mwenye kurehemu”, Allaah Husema: “Mja Wangu amenitukuza”. Mja akisema: "Mfalme wa siku ya malipo”, Allaah Husema: “Mja Wangu Ameniadhimisha". Mja akisema: "Wewe Pekee tunakuabudu na Wewe Pekee tunakuomba msaada”, [Husema]: "Hii ni baina Yangu na Mja Wangu, na Mja wangu atapata aliyoyaomba". Mja akisema: "Tuongoze njia iliyonyooka. Njia ya wale Uliowaneemesha, sio ya walioghadhibikiwa wala waliopotea.”, [Husema] Yote haya ni ya Mja Wangu na Mja Wangu atapata aliyoyaomba)) [Muslim, Abu Daawuwd., At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy]

 

 

 

4- Kuinua Mikono

 

Hadiyth nyingi zimethibitisha kuwa Nabiy  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  alipoomba du’aa alinyanyua mikono yake;, mfano alipoomba mvua alinyanyua mikono yake mpaka  kwapa zake zikaonekana, au alipoeleeka Qiblah na kuomba dhidi ya washirikina katika vita vya Badr mpaka joho lake likamuanguka kutoka mabegani mwake (Ar-Rahiyq Al-Makhtuwm). Pia alipokuwa akiomba du’aa katika ‘ibaadah za Hijjah mfano baina ya Swafaa na Marwah, au kila alipomaliza kurusha vijiwe katika Jamaraat na katika hali mbali mbali zilizothibiti katika Siyrah. Dalili nyingine ni Hadiyth ifuatayo:

 

عنْ سَلْمَانَ (رضي الله عنه) قَالَ : قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((إِنَّ رَبَّكُمْ تَبَارَكَ وَتَعَالَى حَيِيٌّ كَرِيمٌ يَسْتَحْيِي مِنْ عَبْدِهِ إِذَا رَفَعَ يَدَيْهِ إِلَيْهِ أَنْ يَرُدَّهُمَا صِفْرًا )) 

Kutoka kwa Salmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika Rabb wenu Tabaaraka wa Ta’aalaa Yuhai na Mkarimu Anamstahi a mja Wake anapoinua mikono yake [kumuomba] Airudishe sifuri)) [bila ya kumjibu] [Abu Daawuwd na  ameipa daraja ya Swahiyh Shaykh Al-Albaaniy]   

 

Tanbihi: Haikuthibiti Katika Sunnah kunyanyua mikono kuomba du’aa baada ya Swalaah.

 

 

5- Kukiri Madhambi Na Kuomba Maghfirah:

 

Mfano wa Nabiy Yuwnus (‘alayhis-salaam) alipofanya kosa akamezwa na nyangumi alipomuomba Rabb wake kwa kukiri makosa yake kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَذَا النُّونِ إِذ ذَّهَبَ مُغَاضِبًا فَظَنَّ أَن لَّن نَّقْدِرَ عَلَيْهِ فَنَادَىٰ فِي الظُّلُمَاتِ أَن لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنتُ مِنَ الظَّالِمِينَ ﴿٨٧﴾

Na Dhan-Nuwn (Yuwnus) alipoondoka akiwa ameghadhibika, akadhani kwamba Hatutamdhikisha; akaita katika kiza kwamba: “Hapana Muabudiwa wa haki isipokuwa Wewe, Subhaanak! Utakasifu ni Wako, hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu.”

 

فَاسْتَجَبْنَا لَهُ وَنَجَّيْنَاهُ مِنَ الْغَمِّ ۚ وَكَذَٰلِكَ نُنجِي الْمُؤْمِنِينَ ﴿٨٨﴾

Basi Tukamuitikia na Tukamuokoa kutokana na ghamu. Na hivyo ndivyo Tuwaokowavyo Waumini. [Al-Anbiyaa: 87-88]

 

Du’aa nyenginezo za kuomba maghfirah:   

 

 ‘Sayyidul-Istighfaar’ ni du’aa kuu ya kuomba maghfirah.

 

 عن شَدَّادُ بْنُ أَوْسٍ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) عَنْ النَّبِيِّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((سَيِّدُ الإِسْتِغْفَارِ أَنْ تَقُولَ: اللَّهُمَّ أَنْتَ رَبِّي لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ خَلَقْتَنِي وَأَنَا عَبْدُكَ وَأَنَا عَلَى عَهْدِكَ وَوَعْدِكَ مَا اسْتَطَعْتُ أَعُوذُ بِكَ مِنْ شَرِّ مَا صَنَعْتُ أَبُوءُ لَكَ بِنِعْمَتِكَ عَلَيَّ وَأَبُوءُ لَكَ بِذَنْبِي فَاغْفِرْ لِي فَإِنَّهُ لاَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلاَّ أَنْتَ)) قَالَ:  ((وَمَنْ قَالَهَا مِنْ النَّهَارِ مُوقِنًا بِهَا فَمَاتَ مِنْ يَوْمِهِ قَبْلَ أَنْ يُمْسِيَ فَهُوَ مِنْ أَهْلِ الْجَنَّةِ وَمَنْ قَالَهَا مِنْ اللَّيْلِ وَهُوَ مُوقِنٌ بِهَا فَمَاتَ قَبْلَ أَنْ يُصْبِحَ فَهُوَ مِنْ أَهْلِ الْجَنَّةِ))

 

Kutoka kwa Shaddaad bin Aws (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Sayyidul Istighfaar ni useme: “Ee Allaah, Wewe ni Rabb wangu, hapana ilahi (mungu apasaye kuabudiwa kwa haki) ila Wewe, umeniumba mimi na mimi ni mja Wako, nami niko juu ya  ahadi Yako, na agano Lako, kiasi cha uwezo wangu, najikinga Kwako kutokana  na shari ya nilichokifanya, nakiri  Kwako kwa kunineemesha, na nakiri kwa madhambi yangu, basi nakuomba unighufurie kwani hakuna mwingine wa kughufuria madhambi ila Wewe Akasema: ((Atakayesema mchana akiwa na yakini nayo, akafariki siku hiyo kabla kuingia jioni basi atakuwa mtu wa Jannah, na atakayesema usiku naye akiwa na yakini nayo akafariki kabla hajafika asubuhi basi yeye ni mtu wa Jannah))  [Al-Bukhaariy, Tirmidhy, An-Nasaaiy]

 

Pia:

 

عَنْ أَبِي بَكْرٍ الصِّدِّيقِ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) أَنَّهُ قَالَ لِرَسُولِ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ:) "عَلِّمْنِي دُعَاءً أَدْعُو بِهِ فِي صَلاَتِي"  قَالَ: ((قُلْ اللَّهُمَّ إِنِّي ظَلَمْتُ نَفْسِي ظُلْمًا كَثِيرًا وَلاَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلاَّ أَنْتَ فَاغْفِرْ لِي مَغْفِرَةً مِنْ عِنْدِكَ وَارْحَمْنِي إِنَّك أَنْتَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ))

Kutoka kwa Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Alimwambia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) “Nifunze du’aa niiombe katika Swalaah yangu.” Akasema: ((Sema, Ee Allaah hakika mimi nimejidhulumu nafsi yangu dhulma nyingi, na haghufurii madhambi ila Wewe, basi Nighufurie maghfira kutoka Kwako, na Unirehemu. Hakika Wewe ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu . [Al-Bukhaariy (8/168),  Muslim (4/2078) ]

 

 

 

6- Kukiri Neema Za Allaah

 

Kukumbuka neema za Allaah (Subhaanhu wa Ta’aalaa) kisha kuzikiri kwa moyo, ulimi na vitendo. Kufanya hivyo ni kujirudishia manufaa kwani kila mja anapomshukuru Rabb wake (’Azza wa Jalla) Humzidishia neema hizo. Anasema Allaah (Subhaanauu wa Ta’aalaa):

 

وَإِذْ تَأَذَّنَ رَبُّكُمْ لَئِن شَكَرْتُمْ لَأَزِيدَنَّكُمْ

Na pindi Alipotangaza Rabb wenu: “Ikiwa mtashukuru, bila shaka Nitakuzidishieni (neema Zangu); [Ibraahiym: 7]

 

 

 

7- Kuomba Kwa Unyenyekevu, Khofu, Matumaini.

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

وَادْعُوهُ خَوْفًا وَطَمَعًا ۚ إِنَّ رَحْمَتَ اللَّـهِ قَرِيبٌ مِّنَ الْمُحْسِنِينَ ﴿٥٦﴾

na muombeni kwa khofu na matumaini. Hakika rahmah ya Allaah iko karibu na wafanyao ihsaan. [Al-A’raaf: 56]

 

 

 

8- Kuomba Kwa Sauti Ndogo

 

Haipendekezi kuomba du’aa kwa sauti kubwa, kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ni Mwenye Kusikia ya dhahiri na ya siri. Pia inazuia kufanya usumbufu na ghasia kwa wengine. Kuomba kwa siri pia kujiweka mbali na riyaa. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

وَاذْكُر رَّبَّكَ فِي نَفْسِكَ تَضَرُّعًا وَخِيفَةً وَدُونَ الْجَهْرِ مِنَ الْقَوْلِ بِالْغُدُوِّ وَالْآصَالِ وَلَا تَكُن مِّنَ الْغَافِلِينَ﴿٢٠٥﴾

Na mdhukuru Rabb wako katika nafsi yako kwa unyenyekevu na kwa khofu na si kwa jahara katika kauli asubuhi na jioni; na wala usiwe miongoni mwa walioghafilika. [Al-A’raaf: 205]

 

 

Mafunzo kutoka Nabiy Zakariyyah (‘Alayhis-salaam) alipoomba kama ilivyotajwa katika Suwrat Maryam ambayo imeanza kwa:

كهيعص ﴿١﴾

Kaaf Haa Yaa ‘Ayyn Swaad. 

 

 

ذِكْرُ رَحْمَتِ رَبِّكَ عَبْدَهُ زَكَرِيَّا ﴿٢﴾

 (Huu ni) Ukumbusho wa rahmah ya Rabb wako kwa mja Wake Zakariyyaa.

 

 

إِذْ نَادَىٰ رَبَّهُ نِدَاءً خَفِيًّا ﴿٣﴾

Alipomwita Rabb wake mwito wa siri. [Maryam: 1-3]

 

 

 

Na dalili katika Hadiyth:

 

عَنْ أَبِي مُوسَى الأَشْعَرِيِّ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) قَالَ: كُنَّا مَعَ رَسُولِ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) فَكُنَّا إِذَا أَشْرَفْنَا عَلَى وَادٍ هَلَّلْنَا وَكَبَّرْنَا. ارْتَفَعَتْ أَصْوَاتُنَا فَقَالَ النَّبِيُّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم)َ: ((يَا أَيُّهَا النَّاسُ ارْبَعُوا عَلَى أَنْفُسِكُمْ فَإِنَّكُمْ لاَ تَدْعُونَ أَصَمَّ ولاَ غَائِبًا إِنَّهُ مَعَكُمْ ، إِنَّهُ سَمِيعٌ قَرِيبٌ تَبَارَكَ اسْمُهُ وَتَعَالَى جَدُّهُ))

 

Amesimulia Abu Muwsaa Al-Ash’ariyy (رضي الله عنه): Tulikuwa pamoja na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na tukawa kila tukipanda bonde, tunafanya tahliyl (Laa Ilaaha Illa-Allaah), na tunaleta takbiyr (Allaahu Akbar). Zikapanda sauti zetu, na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Enyi watu, zihurumieni nafsi zenu, kwani hamumwombi kiziwi wala asiyekuwepo, hakika Yeye Yupo nanyi (kwa Ujuzi Wake), hakika Yeye Ni Mwenye Kusikia yote, Yupo Karibu, Limebarikika Jina Lake na Umetukuka Ujalali Wake.” [Al-Bukhaariy]

 

 

 

9- Kuomba Mara Tatu

 

Desturi iliyothibiti katika Sunnah kwenye du’aa mbali mbali na Adhkhaar ni kuomba mara tatu, na dalili mojawapo ni katika riwaya ndefu inayosema:

 

  “...وَكَانَ إِذَا دَعَا دَعَا ثَلاَثًا وَإِذَا سَأَلَ سَأَلَ ثَلاَثًا ثُمَّ قَالَ: ((اللَّهُمَّ عَلَيْكَ بِقُرَيْشٍ)) ثَلاَثَ مَرَّاتٍ...

“...na alikuwa anapoomba anaomba mara tatu, akiuliza anauliza mara tatu kisha akaomba: ((Ee Allaah, juu Yako Maquraysh)) mara tatu ...)) [Muslim]

 

 

 

10- Aanze Mtu Kujiombea Nafsi Yake Kwanza:

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amemuamrisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aanze kujiombea maghfirah.

 

وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ مُتَقَلَّبَكُمْ وَمَثْوَاكُمْ﴿١٩﴾

na omba maghfirah kwa dhambi zako na kwa ajili ya Waumini wa kiume na Waumini wa kike. Na Allaah Anajua harakati zenu huku na kule na pahala penu pa kupumzikia. [Muhammad: 19]

 

Na katika Hadiyth:

 

عَنْ أُبَيِّ بْنِ كَعْبٍ (رضي الله عنه)   أَنَّ "رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ كَانَ إِذَا ذَكَرَ أَحَدًا فَدَعَا لَهُ بَدَأَ بِنَفْسِهِ"

Kutoka kwa Ubayy bin Ka’b (Radhwiya Allaahu) kwamba “Alipotajwa mtu kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akimuombea kwa kuanza  kujiombea mwenyewe kwanza” At-Tirmidhiy ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Tirmidhiy [3385] na taz Swahiiyh Al-Jaami’ [4723]

 

Dalili kutoka kwa Manabii:

 

Nabiy Nuwh (‘Alayhis-salaam):

 

رَّبِّ اغْفِرْ لِي وَلِوَالِدَيَّ وَلِمَن دَخَلَ بَيْتِيَ مُؤْمِنًا وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ وَلَا تَزِدِ الظَّالِمِينَ إِلَّا تَبَارًا﴿٢٨﴾

 “Rabb wangu! Nighufurie, na wazazi wangu wawili, na kila aliyeingia nyumbani mwangu mwenye kuamini, na Waumini wa kiume na Waumini wa kike, na wala Usiwazidishie madhalimu isipokuwa kuteketea kabisa. [Nuwh: 28]

 

 

Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis-salaam):

رَبِّ اجْعَلْنِي مُقِيمَ الصَّلَاةِ وَمِن ذُرِّيَّتِي ۚ رَبَّنَا وَتَقَبَّلْ دُعَاءِ﴿٤٠﴾

 “Rabb wangu! Nijaalie niwe mwenye kusimamisha Swalaah na dhuria wangu. Rabb wetu! Nitakabalie du’aa yangu.”

رَبَّنَا اغْفِرْ لِي وَلِوَالِدَيَّ وَلِلْمُؤْمِنِينَ يَوْمَ يَقُومُ الْحِسَابُ ﴿٤١﴾

 “Rabb wetu! Nighufurie na wazazi wangu wawili na Waumini Siku itakayosimama hesabu.” [Ibraahiym: 40-41]

 

Nabiy Muwsaa (‘Alayhis-salaam):

قَالَ رَبِّ اغْفِرْ لِي وَلِأَخِي وَأَدْخِلْنَا فِي رَحْمَتِكَ ۖ وَأَنتَ أَرْحَمُ الرَّاحِمِينَ﴿١٥١﴾

(Muwsaa) Akasema: “Rabb wangu! Nighufurie na kaka yangu, na Utuingize katika rahmah Yako. Nawe ni Mbora zaidi wa kurehemu kuliko wengine wote wenye kurehemu.” [Al-A’raaf: 151]

 

 

Dalili kutoka Salafus-Swaalih (Wema waliotangulia)

 

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ﴿١٠﴾

Na wale waliokuja baada yao wanasema: “Rabb wetu! Tughufurie na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa iymaan na wala Usijaalie katika nyoyo zetu mafundo ya chuki kwa wale walioamini; Rabb wetu! Hakika Wewe ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu. [Al-Hashr:10]

 

 

 

11- Kuomba Jambo Likiwa Na Kheri 

 

Mfano mtu akiwa anaomba kupatiwa kazi aombe ile yenye kheri naye, au mwanamke akiomba kupatiwa mume, aombe mume wa kheri naye n.k. kwani mtu hawezi kujua lipi lenye kheri au shari naye. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

وَعَسَىٰ أَن تَكْرَهُوا شَيْئًا وَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ وَعَسَىٰ أَن تُحِبُّوا شَيْئًا وَهُوَ شَرٌّ لَّكُمْ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿٢١٦﴾

Na asaa mkachukia jambo na hali lenyewe ni kheri kwenu. Na asaa mkapenda jambo na hali lenyewe ni la shari kwenu. Na Allaah Anajua na nyinyi hamjui. [Al-Baqarah: 216]

 

 

 

12- Kusema "Aamiyn"

 

Anapomaliza mja du’aa yake, inapasa aseme ‘Aamiyn’ kwa maana: ‘Ee Rabb Nitakabalie’.  Kama vile tunavyomalizia Suwratul-Faatihah baada ya kuomba du’aa. Na kwa hivyo, imepokelewa kutoka kwa  ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

 ( إِنَّ الْيَهُودَ قَوْمٌ حُسَّدٌ ، وَهُمْ لَا يَحْسُدُونَا عَلَى شَيْءٍ كَمَا يَحْسُدُونَا عَلَى السَّلَامِ ، وَعَلَى آمِينَ  

 ((Hakika Mayahudi ni watu mahasid na hakuna jambo wanalotuhusudu kama kutuhusudu katika maamkizi na katika Aamiyn)) [Ibn Khuzaymah (574) na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Asw-Swahiyhah (691)]

 

 

 

 

 

Share