015-Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake أسماء الله الحسنى وصفاته: AL-QUDDUWS

 

أسماء الله الحسنى وصفاته

Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake

 

Alhidaaya.com

 

 

الْقُدُّوس

AL-QUDDUWS

 

 

 

Al-Qudduws: Mtakatifu Ametakasika Na Sifa Zote Hasi (Pungufu)

 

 

Qudduws linatokana na ‘Qaddasa’ ambayo ina mbili:

 

Kwanza: Kutwaharika, safi, kutakasika na kuwa mbali na najisi, aibu, na upungufu. Imekuja katika Qur-aan pale Malaika waliposema:

قَالُوا أَتَجْعَلُ فِيهَا مَن يُفْسِدُ فِيهَا وَيَسْفِكُ الدِّمَاءَ وَنَحْنُ نُسَبِّحُ بِحَمْدِكَ وَنُقَدِّسُ لَكَ ۖ

Wakasema: “Utaweka humo atakayefanya ufisadi humo na kumwaga damu, na hali sisi tunakusabbih kwa Himidi Zako na tunakutukuza kwa Utakatifu Wako?” [Al-Baqarah: 30]

Az-Zajjaaj amesema maana ya نُقَدِّسُ لَكَ ni: “Tunatwaharisha nafsi zetu Kwako.”

 

Na ndio maana Masjid Al-Aqswaa ya Palestina ikaitwa Baytul-Maqdis ‘Nyumba iliyotakasika’ au sehemu ambayo mtu anajitakasa kutokana na dhambi. Na pia Palestina ikaitwa "Ardhw Al-Muqaddas" (ardhi iliyotakasika).

 

Na katika Qur-aan ametajwa Ruwh Al-Qudus kuwa ni Jibriyl (‘Alayhis-salaam) anayeteremsha maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala):

قُلْ نَزَّلَهُ رُوحُ الْقُدُسِ مِن رَّبِّكَ بِالْحَقِّ لِيُثَبِّتَ الَّذِينَ آمَنُوا وَهُدًى وَبُشْرَىٰ لِلْمُسْلِمِينَ ﴿١٠٢﴾

Sema: Ameiteremsha Ruwhul-Qudus (Jibriyl) kutoka kwa Rabb wako kwa haki ili iwathibitishe wale walioamini na ni mwongozo na bishara kwa Waislamu. [An-Nahl 16:102]

 

Maana ya pili: Iliyobarikiwa, na ndani yake limetoka neno Muqaddasah (iliyobarikiwa) [Al-Lisaan (5/3549), An-Nihaayah (5/23), Ibn Jariyr (1/457), Daqaiq At-Tafsiyr ya Ibn Taymiyyah (1/310)]

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ametaja ardhi iliyobarikiwa katika kauli Yake:

سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَىٰ بِعَبْدِهِ لَيْلًا مِّنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَى الْمَسْجِدِ الْأَقْصَى الَّذِي بَارَكْنَا حَوْلَهُ  

Utakasifu ni wa Ambaye Amemsafirisha usiku mja Wake kutoka Al-Masjid Al-Haraam mpaka Al-Masjid Al-Aqswaa ambao Tumevibariki vilivyoko pembezoni mwake;  [Al-Israa: 1]

 

Jina Lake hili tukufu la Al-Qudduws limetajwa katika Qur-aan mara mbili:

هُوَ اللَّـهُ الَّذِي لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْمَلِكُ الْقُدُّوسُ  

Yeye Ndiye Allaah Ambaye hakuna Muabudiwa wa haki ila Yeye, Mfalme, Mtakatifu Ametakasika na sifa zote hasi… [Al-Hashr 59:23]

 

Na pia:

يُسَبِّحُ لِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ الْمَلِكِ الْقُدُّوسِ الْعَزِيزِ الْحَكِيمِ ﴿١﴾

Vinamsabbih Allaah Pekee vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi, Mfalme, Ametakasika na sifa zote hasi, Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote. [Al-Jumu’ah 62:1]

 

 

Imaam Ibn Al-Qayyim amesema kuhusu maana ya Al-Qudduws: “Aliyesalimika na kila shari, upungufu na aibu kama walivyosema Wafasiri (wa Qur-aan) kwamba Yeye Ametakasika na kila aibu ambayo inapingana na Utukufu Wake.” [Kitaab Asmaa Al-Husnaa, uk.103]

 

Al-Bayhaqiy amesema: “Al-Qudduws ni Ambaye Ametakasika na kila aibu inayomtia upungufu kama kuwa na watoto na kuwa na washirika, na Sifa hii (Al-Qudduws) inamstahiki dhati Yake:  [Al-I’tiqaad ya Al-Bayhqiy (Uk. 54), An-Nihaayah ya Ibn Kathiyr (4/23), Sharh Asmaa Al-Husnaa ya Ar-Raaziy (Uk. 186)]

 

Ibn Kathiyr amesema kuhusu maana ya Al-Qudduws: “Aliyeepukika na kila upungufu, na mwenye kusifika na sifa za ukamilifu." [Tafsiyr Ibn Kathiyr (4/363)]

 

 

Al-Qudduws: Mwenye kuepushwa na kila kinachopinga ukamilifu Wake, katika dhati Yake, katika Majina na Sifa Zake, katika matendo Yake, katika Utawala Wake, Yeye (Tabaaraka wa Ta’aalaa) Amejitenga na kila chenye kwenda kinyume na ukamilifu Wake.

 

Al-Qudduws: Yeye Mu’adhwam [Imethibiti kutoka kwa Mujaahid] yaani ni Mkubwa na Mwenye taadhima, na kila utakatifu, utwahara na ukubwa. [Al-Haq Al-Waadhwih (81-82) na Fat-hu Ar-Rahiym (19-20)].  

 

Al-Qudduws: Ni Al-Mubaarak, Ambaye neema Zake zimekithiri na kuenea kote, na baraka Zake ardhini na mbingu za juu, wakati wote. Jina Lake limebarikiwa, na Sifa Zake zimebarikiwa, na matendo yote yamebarikiwa, na dhati Yake tukufu imebarikiwa.

 

 

Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah: Al-Qudduws:

 

Kuthibitisha iymaan ya kimatendo ya sifa hii tukufu ni kumfanya Muumini kumuadhimisha na kumtukuza Rabb wake. Na inampasa Muumini kujitakasa kutokana na uchafu wa ushirikina na dhulma na maovu yote, na alazimiane na utwahara wa kihisia na kimaana katika kila wakati na katika hilo.

 

Aitakase nafsi yake na matamanio, na mambo ya utata, na moyo wake kutokana na kughafilika, na kiwiliwili chake kutokana na kwenda kinyume na maamrisho, na matamanio yake kwa anayoyaona, na hilo ni kwa kutekeleza maamrisho Yake (Ta’aalaa) na kukatazika na makatazo Yake, na kufuata taratibu na adabu zake. Akifanya hayo moyo wake utang’aa na kumcha Allaah, na hilo litaonekana katika dhahiri yake, na atawaambukiza wengine, na hivyo familia yake itatwaharika kwa twahara yake, na watoto wake, kisha kwa kiasi cha twahara yake watatwaharika wengine.

 

Na yafuatayo ni miongoni mwa ya kujitakasa na kujipatia khayr:

 

1. Jitakase kwa Tawhiyd. Yeye Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni Muabudiwa wa haki Pekee, Hana mshirika wala mke wala mwana.

Anasema:

وَقَالُوا اتَّخَذَ اللَّـهُ وَلَدًا ۗ سُبْحَانَهُ ۖ بَل لَّهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ كُلٌّ لَّهُ قَانِتُونَ ﴿١١٦﴾

Na wakasema: “Allaah Amejichukulia mwana.” Subhaanah! Utakasifu ni Wake! Bali ni Vyake vilivyomo mbinguni na ardhini, vyote vinamtii [Al-Baqarah 2:116]

 

Hata Majini wamemtakasa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) waliposema:

وَأَنَّهُ تَعَالَىٰ جَدُّ رَبِّنَا مَا اتَّخَذَ صَاحِبَةً وَلَا وَلَدًا ﴿٣﴾

“Na kwamba hakika umetukuka kabisa Ujalali wa Rabb wetu, Hakujifanyia mke wala mwana.” [Al-Jinn 72: 3]

 

Na kutokumshirikisha na lolote kwani shirki ni dhambi kubwa mno kama alivyosema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipoulizwa:

عَنْ اِبْنِ مَسْعُودٍ ‏ رضى الله عنه ‏ قَالَ سَأَلْتُ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم: أَيُّ اَلذَّنْبِ أَعْظَمُ؟ قَالَ: ((أَنْ تَجْعَلَ لِلَّهِ نِدًّا, وَهُوَ خَلَقَكَ))‏  

Imepokelewa kutoka kwa Ibn Mas-‘uwd (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: “Nilimuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): Je, dhambi ipi kubwa mno?” Akasema: ((Kumfanyia Allaah mlinganishi (mshirika) na hali Yeye Amekuumba)) [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

Soma vitabu vya Tawhiyd na jifunze aina za Tawhiyd za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ili ujue yepi yenye kumshirikisha ujiepushe nayo.  

 

2. Jitakase na kwa kusoma Qur-aan kwa wingi kwa sababu Qur-aan inasafisha maradhi ya moyo yaliyotajwa katika Qur-aan na Sunnah ambayo ni shirki, kufru, unafiki, uhasidi, chuki, uchoyo n.k. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءَتْكُم مَّوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَشِفَاءٌ لِّمَا فِي الصُّدُورِ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ ﴿٥٧﴾

Enyi watu! Kwa yakini yamekujieni mawaidha kutoka kwa Rabb wenu, na shifaa ya yale yaliyomo vifuani, na mwongozo na rahmah kwa Waumini [Yuwnus 10: 57]

 

Hivyo basi, takasa moyo wako uwe na ikhlaasw katika ‘amali zako, kwa sababu hakuna kitakachokufaa Siku ya Qiyaamah isipokuwa kufika kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa)  na moyo msafi.  

Anasema Aliyetukuka:

يَوْمَ لَا يَنفَعُ مَالٌ وَلَا بَنُونَ ﴿٨٨﴾

“Siku hayatofaa mali wa watoto.

 

إِلَّا مَنْ أَتَى اللَّـهَ بِقَلْبٍ سَلِيمٍ ﴿٨٩﴾

“Isipokuwa yule atakayemfikia Allaah na moyo uliosalimika." [Ash-Shu’araa 26: 88-89]

 

Na Hadiyth ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه)  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه و آله وسلم): ((إِنَّ اللَّهَ لاَ يَنْظُرُ إِلى أجْسَامِكُمْ وَلاَ إِلَى صُوَرِكُمْ وَلَكِنْ يَنْظُرُ إِلَى قُلُوبِكُمْ)) رواه مسلم

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwammba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika Allaah Hatazami viwiliwili vyenu wala sura zenu, lakini Anatazama nyoyo zenu)). [Muslim]

 

 

Hali kadhaalika Qur-aan nzima ina barakah. Soma kwa wingi upate kubarikiwa na Allaah (Ta'aalaa)  Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ إِلَيْكَ مُبَارَكٌ لِّيَدَّبَّرُوا آيَاتِهِ وَلِيَتَذَكَّرَ أُولُو الْأَلْبَابِ ﴿٢٩﴾

Kitabu Tumekiteremsha kwako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) chenye Baraka, ili wapate kuzingatia kwa makini Aayaat zake, na ili wapate kukumbuka wenye akili. [Swaad 38: 29]

 

3. Jitakase kwa kujifunza ‘Aqiydah sahihi kwa sababu ‘Aqiydah sahihi itakuepusha kuingia katika makundi potofu. Na itakubakisha katika utakaso wa Dini ambao ndio mwenendo wa Manabii wote pamoja na wema waliotangulia. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Taa’alaa):

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَۚ وَذَٰلِكَ دِينُ الْقَيِّمَةِ ﴿٥﴾

Na hawakuamrishwa isipokuwa wamwabudu Allaah wenye kumtakasia Dini, wenye kujiengua na upotofu kuelemea Dini ya haki. [Al-Bayyinah 98: 5].

 

4. Jitakase kwa kusimamisha Swalaah tano kwa kuwa Swalaah inamwepusha mtu na machafu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

وَأَقِمِ الصَّلَاةَ ۖ إِنَّ الصَّلَاةَ تَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ ۗ  

…na simamisha Swalaah, hakika Swalaah inazuia machafu na munkari. [Al-‘Ankabuwt 29: 45]

 

Na Hadiyth ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((أَرَأَيْتُمْ لَوْ أَنَّ نَهْرًا بِبَابِ أَحَدِكُمْ يَغْتَسِلُ مِنْهُ كُلَّ يَوْمٍ خَمْسَ مَرَّاتٍ هَلْ يَبْقَى مِنْ دَرَنِهِ شَيْءٌ؟)) قَالُوا: لَا يَبْقَى مِنْ دَرَنِهِ شَيْءٌ. قَالَ: ((فَذَلِكَ مَثَلُ الصَّلَوَاتِ الْخَمْسِ يَمْحُو اللَّهُ بِهِنَّ الْخَطَايَا)) البخاري ومسلم

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mnaonaje ingelikuwa kuna mto mbele ya nyumba ya mmoja wenu kisha akawa anaoga humo kila siku mara tano, je atabakiwa na uchafu?)) Wakasema: "Habakiwi na uchafu". Akasema: ((Hivyo ni mfano wa Swalaah ambazo Allaah hufuta madhambi kwayo)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

5. Jitakase kwa Zakaah ambayo maana yake kutakasa. Na pia kutoa swadaqah na kutoa mali kwa ajili ya Allaah upate kujitakasa kama pale Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Alipomwambia Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا  

Chukua (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) katika mali zao Swadaqah, uwatwaharishe na uwatakase kwazo. [At-Tawbah 9: 103]

 

Na unapotoa mali yako kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni sababu mojawapo nyengine ya kupata baraka katika mali yako kwa sababu Yeye Ameahidi kukuongozea maradufu kama ilivyothibiti katika Aayah kadhaa na Ahaadiyth za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

6. Jitakase na dhulma ambayo Yeye Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ameiharamisha. Amesema katika Hadiyth Qudsiy:

يا عِبادي إنِّي حَرَّمْتُ الظُلْمَ على نَفْسِي وَجعَلْتُهُ بَيْنَكُمْ مُحَرَّماً فلا تَظَالَمُوا.

Enyi waja Wangu, Nimeikataza nafsi Yangu dhulma na Nimeiharamisha kwenu (hiyo dhulma), kwa hivyo msidhulumiane.” [Muslim]

 

Na Anasema Allaah Aliyetukuka:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَظْلِمُ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ ۖ وَإِن تَكُ حَسَنَةً يُضَاعِفْهَا وَيُؤْتِ مِن لَّدُنْهُ أَجْرًا عَظِيمًا ﴿٤٠﴾

Hakika Allaah Hadhulumu hata uzito au chembe (au sisimizi). Na ikiwa ni ‘amali njema Huizidisha na Hutoa kutoka Kwake ujira adhimu. [An-Nisaa 4:40]

 

7. Mtukuze Al-Qudduws na muombe. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha adhkaar za kumtukuza Al-Qudduws kama ifuatavyo:

Katika kurukuu na kusujudu kwenye Swalaah:

سُبـّوحٌ قُـدّْوس، رَبُّ الملائِكَـةِ وَالـرُّوح

Subbuwhun Qudduwsun Rabbul-Malaaikati war-Ruwh

Mwingi wa kutakaswa, Mtakatifu, Rabb wa Malaika na Jibriyl [Hadiyth ya Aaishah (Radhwiya Allaahu ’anhaa) - Muslim (1/353), Abuu Daawuwd (1/230)]

 

Pia du’aa ya mwisho kabisa baada ya kutoa salaam katika Swalaah ya Witr ni:

سُـبْحانَ المَلِكِ القُدّوسِ

Subhaanal-Malikil-Qudduws

 

unaisoma mara tatu, kisha ya tatu yake unaivuta kwa sauti na huku ukisema:

 ربِّ الملائكةِ والرّوح

Rabbil-Malaaikati war-Ruwh

Utakasifu ni wa Mfalme, Mtakatifu. Ee Rabb wa Malaika na wa Jibriyl  [Hadiyth ya ‘Abdur-Rahmaan bin Abzay (Radhwiya Allaahu ‘anhu) - An-Nasaaiy (3/244), Ad-Daaraqutwniy na wengineo].

 

 

 

Share