14-Wewe Pekee Tunakuabudu: Tawassul Zinazokubalika: Kutawassal Kwa Majina Ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)

 

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

Wewe Pekee Tunakuabudu Na Wewe Pekee Tunakuomba Msaada

 

Tawassul Zinazokubalika

 

14-Kutawassal Kwa Majina Ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)

 

 

 

 

Kutawassal kwa Majina Mazuri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kama Anavyotuamrisha Mwenyewe:

 

وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا ۖ وَذَرُوا الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي أَسْمَائِهِ ۚ سَيُجْزَوْنَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ﴿١٨٠﴾

Na Allaah Ana Majina Mazuri kabisa, basi muombeni kwayo. Na waacheni wale wanamili katika kukadhibisha Majina Yake, watalipwa yale waliyokuwa wakiyatenda. [Al-A’raaf: 180]

 

Na kama alivyoomba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika du’aa inayotaja:

 

  أَسْأَلُكَ بِكُلِّ اسْمٍ هُوَ لَكَ سَمَّيْتَ بِهِ نَفْسَكَ، أَوْ عَلَّمْتَهُ أَحَدًا مِنْ خَلْقِكَ، أَوْ أَنْزَلْتَهُ فِي كِتَابِكَ، أَوْ اسْتَأْثَرْتَ بِهِ فِي عِلْمِ الْغَيْبِ عِنْدَكَ،

As-aluka bikullismin huwa Laka, sammayta bihi Nafsaka aw Anzaltahu fiy Kitaabika, aw ‘Allamtahu ahadan min Khalqika, awis-staa-tharta bihi fiy ‘ilmil-ghaybi  ‘In-daka,

 

Nakuomba kwa kila Jina ambalo ni Lako Ulilojiita Kwako Mwenyewe au Uliloliteremsha katika Kitabu Chako, au Ulilomfundisha yeyote yule kati ya viumbe Vyako, au Ulilolihifadhi Wewe mwenyewe (na kujihusisha kulijua) katika ’ilmu ya ghayb Kwako. [Ameipokea Ahmad (1/391) [452], Al-Haakim (1/509) na ameisahihisha Al-Albaaniy katika As-Silsilah Asw-Swahiyhah (199) na Al-Kalim Atw-Twayyib (124)]

 

Na pia anaweza mtu kusema: “Yaa Dhal-Jalaali wal-Ikraami” (Ee Mwenye Ujalali na ukarimu) kama alivyopokea Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

  ((‏‏ألِظُّوا بِيَا ذَا الْجَلالِ وَالإكْرَام ))

((Dumisheni kwa wingi: Yaa-Dhal-Jalaali wal-Ikraami)) [Swahiyh Sunan At-Tirmidhiy (2797)[

 

Na miongoni mwa Majina Yake (‘Azza wa Jalla) ni: “Ar-Rahmaan-Ar-Rahiym” (Mwingi wa rahmah, Mwenye kurehemu). Anaweza kuanza mtu du’aa yake kwa kusema: 

 

Allaahumma inniy as-aluka biannaka Antar-Rahmaanu-Rahiym” (Ee Allaah, hakika mimi nakuomba kwa kuwa Wewe ni Mwenye rahmah, Mwenye kurehemu)

 

Nitakabalie haja yangu kadhaa.”

 

Au kusema:

Yaa Arhamar-Raahimiyn”

(Ee Mbora zaidi wa kurehemu kuliko wengine wote wenye kurehemu)

 

kama walivyoomba baadhi ya Manabiy wakatabaliwa du’aa zao:

 

وَأَيُّوبَ إِذْ نَادَىٰ رَبَّهُ أَنِّي مَسَّنِيَ الضُّرُّ وَأَنتَ أَرْحَمُ الرَّاحِمِينَ ﴿٨٣﴾

Na Ayyuwb alipomwita Rabb wake: “Hakika mimi imenigusa dhara, Nawe Ndiye Mbora zaidi wa kurehemu kuliko wengine wote wenye kurehemu”.

 

 

فَاسْتَجَبْنَا لَهُ فَكَشَفْنَا مَا بِهِ مِن ضُرٍّ ۖ وَآتَيْنَاهُ أَهْلَهُ وَمِثْلَهُم مَّعَهُمْ رَحْمَةً مِّنْ عِندِنَا وَذِكْرَىٰ لِلْعَابِدِينَ ﴿٨٤﴾

Tukamuitikia basi Tukamuondoshea dhara aliyokuwa nayo, na Tukampa ahli zake na mfano wao pamoja nao; ni rahmah kutoka Kwetu na ni ukumbusho kwa wanaoabudu (Allaah). [Al-Anbiyaa: 83-84]

 

 

Pia utumie Sifa za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kumuomba jambo makhsusi ulitakalo mfano:

Yaa Razzaqu, niruzuku kadhaa wa kadhaa.”

 

Yaa Ghafuwuru, nighufurie madhambi yangu.”

 

Yaa ‘Afuwwu, nisamehe.” Kama vile du’aa ya usiku wa Laylatul-Qadr:

 

اللَّهُمَّ إِنَّكَ عَفُوٌّ تُحِبُّ الْعَفْوَ فَاعْفُ عَنِّي

Allaahumma Innaka ‘Afuwwun Tuhibbul-‘afwa fa’fu ‘anniy

Ee Allaah, hakika Wewe Mwingi wa kusamehe Unapenda kusamehe basi nisamehe [At-Tirmidhiy, Ahmad, Ibn Maajah, Swahiyh At-Tirmidhiy (3/170)]

 

Yaa Tawwaabu, nipokelee tawbah yangu.”

 

Yaa Hafiydhwu, nihifadhi kutokana na adui yangu, au kadhaa wa kadhaa.”

 

Yaa Wahhaabu, nitunukie (mke au mume mwema, au mwana…)

 

Yaa Fattaahu, nifungulie jambo langu kadhaa, au nihukumie jambo langu kadhaa.”

 

Yaa Shakuwru, nipokelee shukurani zangu Kwako…

 

Yaa Hamiydu, ee Mwenye kustahiki kuhimidiwa…

 

Yaa Shaafi’u, niponyeshe maradhi yangu.”

 

Yaa Qadiyru, niwezeshee jambo langu kadhaa.”

 

 

Na Sifa Zake nyinginezo utumie katika ile hali makhsusi inayohusiana na Sifa hiyo.

 

Pia unaweza kumwita kwa Sifa ambazo hakuna awezaye kuzimiliki mfano du’aa zifuatazo za Sunnah:

يَا مُقَلِّبَ الْقُلُوبِ ثَبِّتْ قَلْبِي عَلَى دِينِك

Yaa muqallibal quluwbi, thabbit qalbiy ‘alaa Diynika

Ee Mwenye kupindua nyoyo, Thibitisha moyo wangu katika Dini Yako. [At-Tirmidhiy, Ibn Maajah, Ahmad, Al-Haakim  na Swahiyh Al-Jaami’ 7987]

 

 

 اللَّهُمَّ مُصَرِّفَ الْقُلُوبِ صَرِّفْ قُلُوبَنَا عَلَى طَاعَتِك

Allaahumma Muswarrifal quluwbi, swarrif quluwbanaa ‘alaa twaa’atika

Ee Allaah, Mwenye kugeuza nyoyo, zigeuzi nyoyo zetu katika utiifu Wako  [Muslim]

 

Na pia unaweza kutumia Sifa kama zifuatazo:

 

Yaa Faarijal-hammi, nifarijie dhiki yangu kadhaa.”

 

Yaa Kaashifal-ghammi, niondoshee huzuni, au balaa, au janga kadhaa wa kadhaa.”

 

Yaa Qadhwiyal-hajaat, nikidhie, nitimizie haja zangu kadhaa wa kadhaa.”

 

Kisha unaweza kumalizia du’aa kwa kumwita Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

Yaa Kariymu, Ya Samiy’u, Yaa Qariybu, Ya Mujiybu

 (Ee Mkarimu, Ee Mwenye kusikia yote daima, Ee Uliye karibu kwa Ujuzi Wako, Ee Mwenye kuitikia)  Niitikie du’aa yangu kadhaa”.  

 

Na kadhaalika katika Majina na Sifa Zake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

 

 

 

 

Share