16-Wewe Pekee Tunakuabudu: Tawassul Zinazokubalika: Kutawassal Kwa Du'aa Ya Nabiy Yuwnus

 

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

Wewe Pekee Tunakuabudu Na Wewe Pekee Tunakuomba Msaada

 

Tawassul Zinazokubalika

 

16-Kutawassal Kwa Du'aa Ya Nabiy Yuwnus ('Alayhis-Salaam)

 

 

 

 

Du'aa ya Nabiy Yuwnus ('Alayhis-Salaam) ni sababu mojawapo kubwa ya kuitikiwa du’aa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Nabiy Yuwnus ('Alayhis-Salaam) baada ya kuwalingania watu wake katika Tawhiyd wakakanusha, aliwakimbia bila ya kupata idhini ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) hivyo akamkosea Rabb Wake. Baada ya kutupwa baharini kutoka katika jahazi aliyoipanda kwa ajili ya kukimbia mbali, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akamuamrisha nyangumi ammeze bila ya kumla nyama yake au kumvunja mifupa yake. Akabakia tumboni mwa nyangumi kwa masiku kadhaa, akawa anaomba du’aa hiyo ya kujirudi kwa Rabb Wake.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

وَذَا النُّونِ إِذ ذَّهَبَ مُغَاضِبًا فَظَنَّ أَن لَّن نَّقْدِرَ عَلَيْهِ فَنَادَىٰ فِي الظُّلُمَاتِ أَن لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنتُ مِنَ الظَّالِمِينَ ﴿٨٧﴾

Na Dhan-Nuwn (Yuwnus) alipoondoka akiwa ameghadhibika, akadhani kwamba Hatutamdhikisha; akaita katika kiza kwamba: “Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe, Subhaanak! (Utakasifu ni Wako), hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu.” [Al-Anbiyaa: 87]

 

Basi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akamtakabalia:

فَاسْتَجَبْنَا لَهُ وَنَجَّيْنَاهُ مِنَ الْغَمِّ ۚ وَكَذَٰلِكَ نُنجِي الْمُؤْمِنِينَ ﴿٨٨﴾

Basi Tukamuitikia na Tukamuokoa kutokana na ghamu. Na hivyo ndivyo Tuwaokowavyo Waumini. [Al-Anbiyaa: 88]

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akathibitisha kwamba du’aa hiyo aliyoiomba Nabiy Yuwnus ('Alayhis-Salaam) ni du’aa inayosababisha kutakabaliwa du’aa:

 

عَنْ سَعْدٍ بن أبي وقاص (رضي الله عنه)  قَالَ:  قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم)َ: ((دَعْوَةُ ذِي النُّونِ إِذْ دَعَا وَهُوَ فِي بَطْنِ الْحُوتِ: "لاَ إِلَهَ إلاَّ أَنْتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنْتُ مِنْ الظَّالِمِينَ" فَإِنَّهُ لَمْ يَدْعُ بِهَا رَجُلٌ مُسْلِمٌ فِي شَيْءٍ قَطُّ إِلاَّ اسْتَجَابَ اللَّهُ لَهُ))

Kutoka kwa Sa’d bin Abi Waqqaasw (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Du’aa ya Dhan-Nuwn (Nabiy Yuwnus 'Alayhis Salaam) alipoomba alipokuwa katika tumbo la nyangumi:

 

لاَ إِلَهَ إلاَّ أَنْتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنْتُ مِنْ الظَّالِمِينَ

“Laa ilaaha illa Anta Subhaanaka inniy kuntu minadhw-dhwaalimiyn”

 

basi hakika hakuna Muislamu aombaye kwayo kitu chochote kile ila Allaah Atamuitikia)) [Swahiyh At-Tirmidhiy (3505), Swahiyh Al-Jaami’ (3383), Takhriyj Al-Mishkaat Al-Maswaabiyh(2232), As-Silsilah Asw-Swahiyhah (1744)]

 

Bila ya shaka du’aa ya Nabiy Yuwnus ('Alayhis-Salaam) inastahiki kuwa ni wasiylah ya kutakabaliwa du’aa kwa sababu du’aa hiyo imegawanyika katika sehemu tatu:

 

 

1. Kumpwekesha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 لاَ إِلَهَ إلاَّ أَنْتَ

Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe.

 

Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema: “(Nabiy Yuwnus ‘Alayhis-Salaam) Amekiri Tawhiyd ya Uluwhiyyah ambayo inahusiana na aina mojawapo ya du’aa (Du’aa ya ‘ibaadah) kwa sababu ‘Ilaah’ Ndiye Mwenye kustahiki kuombwa aina zote mbili za du’aa; du’aa ya ‘ibaadah na du’aa ya mas-alah (jambo). Naye Ndiye Allaah Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye.” [Kuulizwa kwake Shaykh kuhusu du’aa ya Dhan-Nuwn]

 

 

2. Kumsabbih (kumtakasa) Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa): Kwa maana kumtakasa Allaah ('Azza wa Jalla) kutokana na kila kasoro.

سُبْحَانَكَ

Subhaana! (Utakasifu ni Wako).

 

 

3. Mja kukiri madhambi:

إِنِّي كُنْتُ مِنْ الظَّالِمِينَ

 Hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu.

 

Akasema tena Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah: “Kuhusu kauli yake: “Hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu” Inahusiana na kukiri kwake dhambi, na hivyo ni kuomba maghfirah.”

 

Na Istighfaar (kuomba maghfirah) kuna faida tele kwa dalili kadhaa.

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)

اسْتَغْفِرُوا رَبَّكُمْ إِنَّهُ كَانَ غَفَّارًا﴿١٠﴾

 “Ombeni maghfirah kwa Rabb wenu; hakika Yeye ni Mwingi mno wa kughufuria.

 

يُرْسِلِ السَّمَاءَ عَلَيْكُم مِّدْرَارًا﴿١١﴾

 “Atakutumieni mvua tele ya kuendelea.”

 

 

وَيُمْدِدْكُم بِأَمْوَالٍ وَبَنِينَ وَيَجْعَل لَّكُمْ جَنَّاتٍ وَيَجْعَل لَّكُمْ أَنْهَارًا﴿١٢﴾

 “Na Atakuongezeeni mali na wana, na Atakupeni mabustani na Atakupeni mito.” [Nuwh: 10-12]

 

 

 

 

Share