Kuswali Kwenye Msikiti Wenye Kaburi: Nini Hukmu Yake?

Hukmu Ya Kuswali Kwenye Msikiti Wenye Kaburi

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Kama inavyofahamika kuwa haifai kuswali kwa kuelekea kaburi kama ilivyothibiti kutoka kwa Nabii, swali langu ni kwamba, nifanyaje ikiwa nimeenda katika kijiji mathalani nikakuta kuna msikiti mmoja tu na mbele yake kuna kaburi?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Kwanza, ifahamike kuwa hairuhusiwi kujenga Misikiti kwenye kaburi, wala hairuhusiwi kuswali ndani ya Msikiti wenye kaburi ndani yake.

 

Katika kauli ya mwisho aliyoitoa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kabla ya kurudishwa roho yake iliyotwaharika kwa Rabb wake Aliyeiumba, alisema;

"Allaah Awaangamize Mayahudi na Manaswara, wameyageuza makaburi ya Manabii wao kuwa mahali pa ‘ibaadah, pasibaki na dini mbili katika bara la Arabuni".

[Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Na akasema tena (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

“Ghadhabu ya Allaah imezidi kwa wale wanaogeuza makaburi ya Manabii wao na wachaji Allaah wao kuwa mahala pa ‘ibaadah. Ee Rabb wangu!  Usijaalie kaburi langu likawa mahali pa ‘ibaadah (Misikiti)”. [Muslim]

 

Na akasema:

"Msiswali kuyaelekea makaburi wala msikae juu yake.” [Muslim]

 

Na akasema:

"Allaah Amewalaani Mayahudi na Manaswara wamegeuza makaburi ya Manabii wao kuwa Misikiti". [Imepokelewa na Maimaam wa Hadiyth wenye Sunnan]

 

Hii inadhihirisha wazi kuwa kujenga Misikiti kwenye makaburi ni katika madhambi makubwa.

 

Vilevile ‘Ulamaa wanasema, ikiwa Msikiti ulijengwa juu ya kaburi, basi hukmu ni kuuvunja huo Msikiti na kaburi likabaki lilipo. Na ikiwa kaburi limeingizwa ndani ya Msikiti, basi kaburi lifukuliwe na kilichoko ndani kihamishwe kupelekwa kwenye makaburi wanapozikiwa watu.

 

Ama kuhusu kuswali kwenye Msikiti ambao mbele yake kuna kaburi, tumeliona hilo haliruhusiwi isipokuwa kwa sharti ambalo Wanachuoni wametaja la kuwepo ukuta mrefu ambao unazuia kuliona hilo kaburi na ukuta wenyewe uwe baina ya Msikiti na kaburi na usiwe ni ule ukuta wa Msikiti.

 

Kukitekelezeka sharti hilo, basi ‘Ulamaa wanasema kuwa inaruhusika kuswali ndani ya Msikiti huo.

 

Ama kukiwa hakuna kizuizi cha ukuta mrefu baina ya Msikiti na kaburi, basi haifai kuswali ndani ya Msikiti huo.

 

 

Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) amesema: Imesimuliwa kwamba Abu Marthad Al-Ghanawi amesema: Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Usikae katika makaburi, au kuswali kuyaelekea makaburi.)) [Muslim].

 

Hii inamaanisha kwamba ni haraam kuswali kuyaelekea maeneo ya makaburi au mbele ya makaburi au mbele ya kaburi moja.

 

 

Sababu ya kuwa kwa nini hairuhusiwi kuswali kuyaelekea maeneo ya makaburi ni sababu ile ile [inayojibu] ni kwa nini hairuhusiwi kuswali kuyaelekea makaburi. Itakavyokuwa kwamba mtu anaelekea mbele ya kaburi au eneo la kaburi katika namna ambayo inaweza kusemwa kwamba anaswali kuyaelekea makaburi, basi hili linakuja chini ya kizuizi, na iwapo inaangukia chini ya makatazo basi hairuhusiki, kwa sababu Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Msiswali…))

 

Kizuizi kwa hapa ni katika kuswali, hivyo iwapo mtu ataswali kuelekea kaburi, basi anaunganisha utiifu na uasi, na wala hairuhusiwi kujiweka karibu na Allaah katika namna hiyo.

 

Angalizo: Iwapo kuna ukuta baina yako na eneo la kaburi, basi kanuni kuu [inaeleza] ni kwamba inaruhusika kuswali katika namna hii na wala haikatazwi. Vivyo hivyo, iwapo kuna mtaa au mwendo mkubwa ambao unamaanisha kwamba huwezi kunasibishwa kuswali kuyaelekea makaburi, basi hili linaruhusiwa.

Na Allaah Anajua zaidi  

[Al-Mughniy 1/403; Ash-Sharh Al-Mumti’ cha Ibn ‘Uthaymiyn, 2/232.]

 

 

Swali lilojibiwa na Al-Lajnah Ad-Daaimah:

 

SWALI:

 

Je, ikiwa hali ya huo Msikiti hapo kijijini hauna kizuizi baina yake na kaburi, aswali nyumbani?

 

Jopo la Al-Lajnah Ad-Daaimah ikiongozwa na Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah) inasema haifai kuswali peke yake nyumbani, bali akusanye ndugu zake na watafute eneo waswalie humo kwa pamoja, japo eneo la wazi.

 

Kadhaalika, afanye bidii kuanzisha Msikiti ambao ndani yake watasimamisha shariy’ah ya Allaah ya Swalaah tano kila siku kwa utaratibu sahihi wa shariy’ah ya Kiislamu, na kujiweka mbali nay ale Allaah Aliyoyakataza.

Na swalaah na salaam ziwe juu ya Nabiy wetu Muhammad, familia yake, na Maswahaba zake.

[Al-Lajnatud Daaimah Lil Buhuwth Al-‘Ilmiyyah wal Iftaa, mj. 1, uk. 52]

 

Tunakhitimisha kwa kumshauri ndugu huyo, ajitahidi kwa uwezo wake kujenga japo kibanda kidogo cha makuti kwa kadiri uwezo wao unavyowaruhusu wakifanye Msikiti ili waweze kutekeleza ‘ibaadah zao hapo mbali na sehemu zilizokatazwa kishariy’ah.

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Awasahilishie jambo hilo na Awatakalie ‘amali zao na juhudi zao.

 

Na Allaah ni Mjuzi zaidi

 

 

 

Share