143-Aayah Na Mafunzo: Ummah Bora Na Adilifu Ni Ummah Wa Kiislamu

Aayah Na Mafunzo

Al-Baqarah

Ummah Bora Na Adilifu Ni Ummah Wa Kiislamu  

 

 

وَكَذَٰلِكَ جَعَلْنَاكُمْ أُمَّةً وَسَطًا لِّتَكُونُوا شُهَدَاءَ عَلَى النَّاسِ وَيَكُونَ الرَّسُولُ عَلَيْكُمْ شَهِيدًا ۗ وَمَا جَعَلْنَا الْقِبْلَةَ الَّتِي كُنتَ عَلَيْهَا إِلَّا لِنَعْلَمَ مَن يَتَّبِعُ الرَّسُولَ مِمَّن يَنقَلِبُ عَلَىٰ عَقِبَيْهِ ۚ وَإِن كَانَتْ لَكَبِيرَةً إِلَّا عَلَى الَّذِينَ هَدَى اللَّـهُ ۗ وَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيُضِيعَ إِيمَانَكُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ بِالنَّاسِ لَرَءُوفٌ رَّحِيمٌ ﴿١٤٣﴾

143. Na ndivyo hivyo Tumekufanyeni ummah bora na adilifu ili muwe mashahidi juu ya watu na awe Rasuli shahidi juu yenu. Na Hatukukifanya Qiblah ambacho ulikuwa ukikielekea (Baytul-Maqdis) isipokuwa Tupate kumpambanulisha yule anayemfuata Rasuli miongoni mwa mwenye kugeuka akarudi nyuma. Na hakika ilikuwa ni jambo gumu isipokuwa kwa wale ambao Allaah Amewaongoza. Na Allaah Hakuwa Mwenye kupoteza iymaan yenu (Swalaah), hakika Allaah kwa watu, bila shaka ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu.

 

 

Mafunzo:

 

Masjid hiyo waliyoswali Swahaba wakageuza Qiblah chao kuelekeza Al-Ka’bah wakiwa ndani ya Swalaah, ndio inayojulikana kama Masjd Al-Qiblatayni (Msikiti wa Qiblah mbili) Yaani; kuelekea kwao ndani ya Swalaah moja, kwanza Baytul-Maqdis (Palestina) kisha kuelekea kwao Al-Ka’bah baada ya kuteremshwa Aayah hii ya 143 Al-Baqarah.

 

Kuhusu kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى): Na ndivyo hivyo Tumekufanyeni ummah bora na adilifu ili muwe mashahidi juu ya watu na awe Rasuli shahidi juu yenu”, Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (رضي الله عنه) amehadithia kwamba: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Ataitwa Nuwh Siku ya Qiyaamah ataulizwa: Je, umebalighisha ujumbe? Atasema: Naam. Wataitwa watu wake wataulizwa: Je, alikufikishieni ujumbe? Watasema: Hakutujia mwonyaji wala hakuna aliyetumwa kwetu. Ataulizwa Nuwh: Nani mwenye kukushuhudia hayo? Atasema: Muhammad na Ummah wake.  Akasema: Hiyo ndio maana kauli Yake: “Na ndivyo hivyo Tumekufanyeni ummah bora na adilifu ili muwe mashahidi juu ya watu na awe Rasuli shahidi juu yenu.” Akasema: “Waswatwaa, maana yake ni uadilifu basi mtatoa ushahidi (kuhusu Nuwh) kubalighisha ujumbe na kisha nitakuwa shahidi wenu.”  [Ahmad (3/32) na Al-Bukhaariy pia kama hivyo (4487)]

 

 

Share