079-Sababu Ya Kuteremshwa Sema: “Yeyote Aliyekuwa Adui Wa Jibriyl...

Aayah Na Mafunzo

Al-Baqarah

Sababu Ya Kuteremshwa Sema: “Yeyote aliyekuwa adui wa Jibriyl

Imekusanywa na Alhidaaya.com

 

 

قُلْ مَن كَانَ عَدُوًّا لِّجِبْرِيلَ فَإِنَّهُ نَزَّلَهُ عَلَىٰ قَلْبِكَ بِإِذْنِ اللَّـهِ مُصَدِّقًا لِّمَا بَيْنَ يَدَيْهِ وَهُدًى وَبُشْرَىٰ لِلْمُؤْمِنِينَ ﴿٩٧﴾

97. Sema: “Yeyote aliyekuwa adui wa Jibriyl, basi hakika yeye ameiteremsha Qur-aan katika moyo wako (ee Nabiy صلى الله عليه وآله وسلم) kwa idhini ya Allaah inayosadikisha yaliyo kabla yake, na mwongozo na bishara kwa Waumini.

 

مَن كَانَ عَدُوًّا لِّلَّـهِ وَمَلَائِكَتِهِ وَرُسُلِهِ وَجِبْرِيلَ وَمِيكَالَ فَإِنَّ اللَّـهَ عَدُوٌّ لِّلْكَافِرِينَ ﴿٩٨﴾

98. Yeyote aliyekuwa adui wa Allaah na Malaika Wake, na Rusuli Wake, na Jibriyl, na Miykaala, basi hakika Allaah ni adui kwa makafiri.

 

Mafunzo:

 

Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremka hali ya kuwa ni jawabu kwa Mayahudi miongoni mwa wana wa Israaiyl, pale walipodai kuwa Jibriyl (عليه السلام) ni adui yao. [Imaam Ahmad katika Musnad yake kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما)].

Kadhaalika kama alivyohadithia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) kwamba: Kundi miongoni mwa Mayahudi lilihudhuria kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) wakasema: Yaa Abaa Al-Qaasim! Tuelezeee kuhusu tunayokuuliza kwani hayajui isipokuwa Nabiy. Akasema: “Niulizeni mnayotaka lakini niwekeeni ahadi kwa Allaah (kama ahadi) aliyofungamana Ya’quwb kwa wanawe, kuwa nikikuhadithieni jambo mkalijua, mtanifuata katika Uislamu.” Wakasema: Umelipata hilo (tumekubali). Akasema: “Niulizeni mtakacho.” Wakasema: Tuelezee mambo manne tutakayokuuliza; Tueleze ni chakula gani alichojiharamishia Ya’quwb kabla ya kuteremshwa Tawraat? Na tueleze vipi yanakuwa maji (manii) ya mwanamme na mwanamke, na vipi anakuwa (mtoto) wa kiume anayetokana na maji hayo? Na tueleze vipi anakuwa usingizini huyu Nabiy ambaye hajui kusoma? Na nani anakuwa kipenzi chake katika Malaika? Akasema: “Je, mnanipa ahadi kwa Allaah kuwa nikikuelezeni mtanifuata?” Ibn ‘Abbaas akasema: Mayahudi wakampa ahadi. Akasema: “Nakuapieni kwa Ambaye Ameteremsha Tawraat kwa Muwsaa (عليه السلام) hivi mnajua kuwa Ya’quwb aliugua maradhi makali, yakakaa muda mrefu maradhi yake, akaweka nadhiri kwa Allaah kuwa, endapo atapona maradhi yake, atajiharamishia vinywaji avipendavyo sana na vyakula avipendavyo sana na kilikuwa chakula akipendacho zaidi nyama ya ngamia na kinywaji akipendacho zaidi ni maziwa yake?” Wakasema: Allaahumma na’am! Akasema: “Yaa Allaah Washuhudie!  Na nakuapieni kwa Allaah Ambaye hapana muabudiwa wa haki ila Yeye, na Ambaye Amteremsha Tawraat kwa Muwsaa (عليه السلام), hivi mnajua kuwa maji ya mwanamme ni meupe mazito, na maji ya mwanamke ni ya njano mepesi, basi moja ya maji hayo yakiwa juu ya mengine anakuwa jinsia yake huyo mtoto na kufanana naye kwa idhini ya Allaah.  Na endapo yakiwa maji ya mwanaume juu ya maji ya mwanamke, anakuwa (mtoto) wa kiume, na yakiwa maji ya mwanamke juu ya mwanamme, anakuwa wa kike kwa idhini ya (Allaah سبحانه وتعالى)?” Wakasema: Allaahumaa na’am! Akasema: “Yaa Allaah Washuhudie! Na nakuapieni kwa Allaah Ambaye Ameteremsha Tawraat kwa Muwsaa, hivi mnajua kuwa huyu Nabiy asiyejua kusoma (kuwa) yanalala macho yake wala haulali moyo wake?” Wakasema: Allaahumma na’am! Akasema: “Yaa Allaah Shuhudia!” Wakasema: Basi sasa wewe tuelezee ni nani kipenzi chako katika Malaika? Hapo ndio tutakuwa na wewe au tutafarikiana. Akasema: “Hakika kipenzi changu ni Jibriyl na wala Allaah Hakutuma Nabiy yeyote ila anakuwa kipenzi chake.” Wakasema: Hapo ndio tunafarikiana! Lau angekuwa kipenzi chako mwengine katika Malaika tungekufuata na tungekusadikisha. Akasema: “Kipi kinachokuzuieni kumsadikisha?” Wakasema: Hakika yeye ni adui yetu. Ibn ‘Abbaas akasema: Hapo ndipo Alipoteremsha Allaah Ta’aala: Sema: “Yeyote aliyekuwa adui wa Jibriyl, basi hakika yeye ameiteremsha Qur-aan katika moyo wako...”  mpaka kauli ya Allaah [Aayah (2: 101)]  “...Kitabu cha Allaah nyuma ya migongo yao kana kwamba hawajui.” na hapo wakastahiki ghadhabu juu ya ghadhabu (2: 90) Suwrah Al-Baqarah) [Musnad Ahmad (2384). Ni Hadiyth Swahiyh kwa mkusanyiko wa njia zake na imenukuliwa Ijmaa’ juu usahihi wake].

 

 

 

Share