077-Aayah Na Mafunzo: Watu Watatu Allaah Hatowasemesha Siku Ya Qiyaamah

Aayah Na Mafunzo

Aal-‘Imraan

Watu Watatu Allaah Hatowasemesha Siku Ya Qiyaamah  

 

 

 

إِنَّ الَّذِينَ يَشْتَرُونَ بِعَهْدِ اللَّـهِ وَأَيْمَانِهِمْ ثَمَنًا قَلِيلًا أُولَـٰئِكَ لَا خَلَاقَ لَهُمْ فِي الْآخِرَةِ وَلَا يُكَلِّمُهُمُ اللَّـهُ وَلَا يَنظُرُ إِلَيْهِمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَلَا يُزَكِّيهِمْ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٧٧﴾

77. Hakika wale wanaobadilisha ahadi ya Allaah na viapo vyao kwa thamani ndogo; hao hawana sehemu yoyote katika Aakhirah na wala Allaah Hatowasemesha na wala Hatowatazama Siku Ya Qiyaamah na wala Hatowatakasa na watapata adhabu iumizayo.

 

Mafunzo:

 

Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Watu wa aina tatu Allaah Hatowasemesha Siku ya Qiyaamah, wala Hatowatazama;  Mtu wa kwanza mwenye kuapa juu ya bidhaa yake kuwa amekwishapewa thamani kubwa zaidi ya hiyo aliyopewa hali yakuwa ni muongo, na mtu wa pili  mwenye kuapa kiapo cha uongo baada ya Alasiri ili apate kuichukua mali ya Muislamu kupitia kiapo hicho, na mtu wa tatu mwenye kubakhilia (kuzuilia) mabaki ya maji. Allaah Atasema Siku ya Qiyaamah: Leo hii Ninakunyima fadhila Zangu kama ulivyozuilia mabaki ya kile ambacho haukukitengeneza kwa mikono yako.” [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

 

Sababun- Nuzuwl: Aayah hii imeteremka kama alivyohadithia ’Abdullaah bin Mas’uwd(رضي الله عنه)  kwamba: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alisema: ”Yeyote atakayeapa kiapo ili achukue mali ya Muislamu (bila ya haki) atakutana na Allaah Akiwa Amemghadhibikia.” Hapo Allaah Akateremsha kusadikisha kauli hii: Hakika wale wanaobadilisha ahadi ya Allaah na viapo vyao kwa thamani ndogo; hao hawana sehemu yoyote katika Aakhirah...” mpaka mwisho wa Aayah (3: 77). Akasema: Kisha akaingia Al-Ash’ath bin Qays akasema: Je, ’Abdur-Rahmaan anakuhadithieni nini? Tukasema: Kadhaa wa kadhaa. Akasema: Aayah hii imeteremshiwa kuhusu mimi; nilikuwa na kisima katika ardhi ya bin-’ammi yangu (lakini alikanusha kuwa similiki). Kisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akaniambia: ”Ima ulete ushahidi au yeye (bin-’ammi yako) atatoa kiapo (kuthibitisha madai yake).” Nikasema:  Nina hakika atatoa kiapo (cha uongo) ee Rasuli wa Allaah. Kisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: ”Atakayeapa kwa ajili ya kuchukua ardhi ya Muislamu (bila haki) hali ya kuwa ni muongo katika kiapo chake, atakutana na Allaah Akiwa Amemghadhibikia.” [Al-Bukhaariy].

 

Na pia imeteremka kwa mtu mmoja ambaye  aliisimamisha bidhaa yake sokoni  kisha  akaapa juu hiyo bidhaa kuwa amekwishapewa thamani kubwa kwenye hiyo bidhaa zaidi ya hiyo anayotaka kupewa,  hali ya kuwa hajapewa thamani hiyo, na aliapa kiapo hicho  ili amshawishi  mmoja katika Waislamu ainunue hiyo bidhaa, hapo ikateremka hii Aayah [Amehadithia Ibn Abi Awfaa (رضي الله عنه) ameipokea Al-Bukhaariy].

 

Share