103-Aayah Na Mafunzo: Allaah Anaridhia Mshikamane Kwa Kamba Yake Msifarikiane

Aayah Na Mafunzo

Aal-‘Imraan

Allaah Anaridhia Mshikamane Kwa Kamba Yake Msifarikiane

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا ۚ وَاذْكُرُوا نِعْمَتَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ إِذْ كُنتُمْ أَعْدَاءً فَأَلَّفَ بَيْنَ قُلُوبِكُمْ فَأَصْبَحْتُم بِنِعْمَتِهِ إِخْوَانًا وَكُنتُمْ عَلَىٰ شَفَا حُفْرَةٍ مِّنَ النَّارِ فَأَنقَذَكُم مِّنْهَا ۗ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمْ آيَاتِهِ لَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ ﴿١٠٣﴾ 

103. Na shikamaneni kwa kamba ya Allaah nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Allaah juu yenu, pale mlipokuwa maadui (kati yenu); kisha Akaunganisha nyoyo zenu, mkawa kwa neema Yake ndugu; na mlikuwa ukingoni mwa shimo la moto Akakuokoeni humo. Hivyo ndivyo Allaah Anavyokubainishieni Aayaat Zake mpate kuongoka.

 

 

Mafunzo:

 

Maana Ya Kushikamana Na Kamba Ya Allaah Bila Kufarikiana.

 

Kushikamana na kamba ya Allaah bila ya kufarikiana   imekusudiwa kubakia katika Swiraatw Al-Mustaqiym [Rejea Al-Faatihah (1:6)] 

 

Na pia Kauli ya Allaah (عزّ وجلّ):

 

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ ﴿١٥٣﴾

Na kwamba hii njia Yangu iliyonyooka, basi ifuateni. Na wala msifuate njia nyinginezo zitakufarikisheni na njia Yake. Hivyo ndivyo Alivyokuusieni (Allaah) kwayo mpate kuwa na taqwa [Al-An’aam (6:153)]

 

Pia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ametahadharisho mno kuhusu kuthibitika katika Swiraatw Al-Mustaqiym ambayo inamaanisha kutokutoka nje na mafunzo ya Qur-aan na Sunnah. Miongoni mwa maonyo yake ni Hadiyth ifuatayo:

 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Najiyh Al-‘Irbaadhw bin Saariyah (رضي الله عنه) amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alitupa mawaidha mazito (yenye maana kubwa), nyoyo zikaogopa na macho yakabubujikwa machozi. Tukasema: Ee Rasuli wa Allaah! Yanaonekana kama kwamba mawaidha ya kutuaga, basi tuusie.  Akasema: “Nakuusieni kuwa na taqwa ya Allaah na kusikiliza na kutii japokuwa mtaongozwa na mtumwa Mhabashi. Hakika atakayeishi umri mrefu miongoni mwenu ataona ikhtilaaf nyingi. Kwa hiyo, shikamaneni na Sunnah zangu na mwenendo wa Makhalifa waongofu, yashikilieni kwa magego [mambo yao]. Na tahadharini na mambo yenye kuzushwa, kwani kila uzushi ni upotovu.” [Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy, na amesema: Hadiyth Hasan Swahiyh].

   

Na pia,

 

Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah Anawaridhia mambo matatu na Anachukia kwenu mambo matatu; Anawaridhia mumwabudu Yeye, wala msimshirikishe kwa chochote, na mshikamane nyote na kamba ya Allaah wala msifarikiane. Na anachukia kwenu uvumi, kuuliza sana na   kupoteza mali.” [Muslim, na katika riwayaah: “Na muwanasihi wenye kuwatawalia mambo yenu.” Swahiyh Adab Al-Mufrad (343)].

 

  

 

 

 

Share