180-Aayah Na Mafunzo: Tahadharisho La Kutokutoa Zakaah

Aayah Na Mafunzo

Aal-‘Imraan

Tahadharisho La Kutokutoa Zakaah

Alhidaaya.com

 

 

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَلَا يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ يَبْخَلُونَ بِمَا آتَاهُمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ هُوَ خَيْرًا لَّهُم ۖ بَلْ هُوَ شَرٌّ لَّهُمْ ۖ سَيُطَوَّقُونَ مَا بَخِلُوا بِهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ وَلِلَّـهِ مِيرَاثُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۗ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ ﴿١٨٠﴾

Wala wasidhani kabisa wale wanaofanya ubakhili kwa yale Aliyowapa Allaah katika fadhila Zake kwamba hayo ni kheri kwao, bali ni shari kwao. Watafungwa kongwa yale waliyoyafanyia ubakhili Siku ya Qiyaamah. Na ni Wake Allaah Pekee urithi wa mbingu na ardhi. Na Allaah kwa myatendayo ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. [Aal-'Imraan: 180]

 

 

Mafunzo:

 

 

Tahadharisho la kutokutoa Zakaah: Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Yeyote yule ambaye Allaah Amemruzuku mali kisha asiitolee Zakaah yake, basi (Siku ya Qiyaamah) mali yake itakuwa kama nyoka dume kipara aliye na madoti mawili juu ya macho yake. Atamvingirita shingoni na kumuuma mashavu yake huku akisema: Mimi mali yako! Mimi hazina yako!” [Al-Bukhaariy]

 

Na Anasema pia Allaah (سبحانه وتعالى):

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ كَثِيرًا مِّنَ الْأَحْبَارِ وَالرُّهْبَانِ لَيَأْكُلُونَ أَمْوَالَ النَّاسِ بِالْبَاطِلِ وَيَصُدُّونَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ ۗ وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلَا يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ﴿٣٤﴾

Enyi walioamini! Hakika wengi katika Wanazuoni Marabai wa dini (zao) na Wamonaki wanakula mali za watu kwa batili, na wanazuia njia ya Allaah. Na wale wanaorundika dhahabu na fedha na wala hawazitoi katika njia ya Allaah, basi wabashirie adhabu iumizayo. 

 

 

 

يَوْمَ يُحْمَىٰ عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَىٰ بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنُوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ ۖ هَـٰذَا مَا كَنَزْتُمْ لِأَنفُسِكُمْ فَذُوقُوا مَا كُنتُمْ تَكْنِزُونَ﴿٣٥﴾

Siku zitakapopashwa katika Jahannam, na kwazo vikachomwa moto vipaji vyao, na mbavu zao, na migongo yao (wakiambiwa): Haya ndiyo mliyoyarundika kwa ajili ya nafsi zenu. Basi onjeni yale mliyokuwa mkiyarundika. [At-Tawbah: 34-35]

 

 

Share