043-Aayah Na Mafunzo: Kisa Cha ‘Aishah Kuwa Ni Sababu Ya Kuteremshwa Hukmu Ya Tayammum Na Uharamisho Wa Pombe Na Kikomo Chake

 

Aayah Na Mafunzo

An-Nisaa

Kisa Cha Kidani Cha ‘Aishah (رضي الله عنها)

Ni Sababu Ya Kuteremshwa Hukmu Ya Tayammum

Hatua Za Uharamisho Wa Pombe Na Kikomo Chake

 

Alhidaaya.com

 

 

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَقْرَبُوا الصَّلَاةَ وَأَنتُمْ سُكَارَىٰ حَتَّىٰ تَعْلَمُوا مَا تَقُولُونَ وَلَا جُنُبًا إِلَّا عَابِرِي سَبِيلٍ حَتَّىٰ تَغْتَسِلُوا ۚ وَإِن كُنتُم مَّرْضَىٰ أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ أَوْ جَاءَ أَحَدٌ مِّنكُم مِّنَ الْغَائِطِ أَوْ لَامَسْتُمُ النِّسَاءَ فَلَمْ تَجِدُوا مَاءً فَتَيَمَّمُوا صَعِيدًا طَيِّبًا فَامْسَحُوا بِوُجُوهِكُمْ وَأَيْدِيكُمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَفُوًّا غَفُورًا ﴿٤٣﴾

Enyi walioamini! Msikaribie Swalaah na hali mmelewa mpaka mjue mnayoyasema, na wala mkiwa mna janaba isipokuwa mmo safarini mpaka muoge josho. Na mkiwa wagonjwa au safarini au mmoja wenu ametoka msalani au mmewagusa wanawake kisha hamkupata maji, basi ikusudieni ardhi safi ya mchanga (mtayammam), mpake nyuso zenu na mikono yenu. Hakika Allaah daima Ni Mwingi wa Kusamehe, Mwingi wa Kughufuria. [An-Nisaa: 43]

 

Mafunzo:

 

Tayammum ni katika mambo matatu tuliyofadhilishwa nayo Ummah wetu wa Kiislamu kwa dalili:  

 

Hudhayfah bin Al-Yamaani (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Tumefadhilishwa juu ya watu matatu; Swafu zetu (katika Swalaah) zimefafanishwa kama swafu za Malaika. Na tumejaaliwa ardhi yote kuwa Masjid, na mchanga wake kwetu ni twahara inapokosekana maji.” [Muslim].

 

Sababu ya kuteremshwa hukmu ya tayammum

 

Mama wa ‘Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها)  amehadithia: “Tulikwenda katika moja ya safari tukafika Al-Baydaa au Dhaatul-Jaysh ambako kidani changu kilivunjika (na kikapotea). Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akawa anakitafuta, kisha pia watu wengineo wakainuka kukitafuta. Hapakuweko na maji sehemu hiyo, basi watu wakamwendea Abuu Bakr Asw-Swiddiyq na kusema: Huoni alivyofanya ‘Aaishah? Kamfanya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) pamoja na watu wakae sehemu ambayo hakuna maji! Abuu Bakr akaja wakati Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa amelaa akiwa amelaza kichwa chake mapajani mwangu. Akaniambia: Umemzuia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na watu sehemu ambako hakuna maji na wala hawana (akiba ya) maji. Basi akanigombesha na akasema Aliyomjaalia (Allaah) kusema kuhusu mimi na akanipiga ubavuni kwa mkono wake. Hakuna kilichonizuia kusogea (kutokana na maumivu) isipokuwa kwa vile Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alilala mapajani mwangu. Hapo Allaah Akateremsha Aayah ya tayammum, basi wakatayammam. ‘Usayd bin Al-Hudhwayr akasema: Ee ahli ya Abuu Bakr! Hii si baraka ya kwanza kwenu. Kisha akaendeshwa ngamia ambaye nilikuwa nimempanda na tukakipata kidani chini yake.” [Al-Bukhaariy].

 

Hatua Za Uharamisho Wa Pombe Na Kikomo Chake:

 

Hatua ya kwanza kuhusu pombe imetahadharishwa katika Suwratul-Baqarah (2:219):

 

يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ ۖ قُلْ فِيهِمَا إِثْمٌ كَبِيرٌ وَمَنَافِعُ لِلنَّاسِ وَإِثْمُهُمَا أَكْبَرُ مِن نَّفْعِهِمَا ۗ

Wanakuuliza kuhusu pombe na kamari. Sema: Katika viwili hivyo mna dhambi kubwa na (baadhi ya) manufaa kwa watu. Na dhambi yake viwili hivyo ni kubwa kuliko manufaa yake. [Al-Baqarah (2:219)]

 

Kisha hatua ya pili ilikuwa ni kukatazwa pombe katika nyakati za Swalaah kwa sababu Swahaba walikosea kusoma Qur-aan katika Swalaah kutokana na kulewa. Allaah (سبحانه وتعالى) Akateremsha Aayah katika Suwrah An-Nisaa (4:43):  

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَقْرَبُوا الصَّلَاةَ وَأَنتُمْ سُكَارَىٰ حَتَّىٰ تَعْلَمُوا مَا تَقُولُونَ  

Enyi walioamini! Msikaribie Swalaah na hali mmelewa mpaka mjue mnayoyasema [An-Nisaa (4:43)]

 

Baada ya hapo ikafutwa hukmu hiyo na ikabakia pombe kuwa ni haraam nyakati zote kwa kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّمَا الْخَمْرُ وَالْمَيْسِرُ وَالْأَنصَابُ وَالْأَزْلَامُ رِجْسٌ مِّنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ فَاجْتَنِبُوهُ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٩٠﴾

Enyi walioamini! Hakika pombe na kamari na masanamu na kutazamia kwa mishale ya kupigia ramli, ni najisi na chukizo kutokana na kazi ya shaytwaan. Basi jiepusheni navyo mpate kufaulu. [Al-Maaidah (5:90)]

 

Baada ya kuteremshwa Aayah hii ya Suwrah Al-Maaidah (5:90), hapo hapo Swahaba wakaacha moja kwa moja kulewa ikawa ndio kikomo cha kunywa pombe.

 

 

Bonyeza kiungo kifuatacho upate faida nyenginezo kuhusu matahadharisho ya pombe, uharamisho wake, laana na adhabu zake.

 

04-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Al-Huduwd (Adhabu): Mlango Wa Adhabu Ya Mnywaji Pombe Na Kubainisha Kileo (Ni Nini)

 

 

 

 

Share