092-Aayah Na Mafunzo: Haramisho La Kuua Bila Haki Na Adhabu Zake

Aayah Na Mafunzo

An-Nisaa

Haramisho La Kuua Bila Haki Na Adhabu Zake

 

Alhidaaya.com

 

 

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ أَن يَقْتُلَ مُؤْمِنًا إِلَّا خَطَأً ۚ وَمَن قَتَلَ مُؤْمِنًا خَطَأً فَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مُّؤْمِنَةٍ وَدِيَةٌ مُّسَلَّمَةٌ إِلَىٰ أَهْلِهِ إِلَّا أَن يَصَّدَّقُوا ۚ فَإِن كَانَ مِن قَوْمٍ عَدُوٍّ لَّكُمْ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مُّؤْمِنَةٍ ۖ وَإِن كَانَ مِن قَوْمٍ بَيْنَكُمْ وَبَيْنَهُم مِّيثَاقٌ فَدِيَةٌ مُّسَلَّمَةٌ إِلَىٰ أَهْلِهِ وَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مُّؤْمِنَةٍ ۖ فَمَن لَّمْ يَجِدْ فَصِيَامُ شَهْرَيْنِ مُتَتَابِعَيْنِ تَوْبَةً مِّنَ اللَّـهِ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ عَلِيمًا حَكِيمًا ﴿٩٢﴾

Na haiwi kwa Muumin amuue Muumin ila kwa kukosea tu. Na atakayemuua Muumin kwa kukosea basi aachilie huru mtumwa Muumin na atoe diya kwa kuifikisha kwa ahli zake, isipokuwa kama wenyewe watasamehe. Na akiwa ni jamaa wa maadui zenu naye ni Muumin, basi (aliyeua) aachilie huru mtumwa Muumin. Na akiwa ni miongoni mwa watu ambao kuna mkataba baina yenu na baina yao, basi wapewe diya watu wake na aachiliwe huru mtumwa Muumin. Asiyepata, afunge Swiyaam miezi miwili mfululizo kuwa ni tawbah kwa Allaah. Na Allaah daima Ni Mjuzi wa yote, Mwenye Hikmah wa yote.

 

وَمَن يَقْتُلْ مُؤْمِنًا مُّتَعَمِّدًا فَجَزَاؤُهُ جَهَنَّمُ خَالِدًا فِيهَا وَغَضِبَ اللَّـهُ عَلَيْهِ وَلَعَنَهُ وَأَعَدَّ لَهُ عَذَابًا عَظِيمًا ﴿٩٣﴾

Na atakayemuua Muumini kwa kusudi, basi jazaa yake ni Jahannam, atadumu humo, na Allaah Atamghadhibikia, Atamlaani na Atamuandalia adhabu kuu. [An-Nisaa: 92-93]

 

 

Mafunzo:

 

Dalili nyingi katika Qur-aan na Sunnah zimeharamisha kuua mtu bila ya haki. Miongoni mwa Ahaadiyth ni:

 

‘Abdullaah bin ‘Amru (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Kutokomea dunia ni kwepesi zaidi kuliko kuua Muislamu.” [Swahiyh An-Nasaaiy (3998)].

 

“Wangeshirikiana watu wa mbinguni na ardhini kumwaga damu ya Muumini, Allaah Angewaingiza motoni.” [Amehadithia Al-Baraa bin ‘Aazib (رضي الله عنه) ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Targhiyb].

 

“Muumini hatoacha kuwa katika Dini yake madamu hajagusa damu ya haramu.” (hajamwaga damu). [Al-Bukhaariy].

 

Na pia kuhusu madhambi saba yanayoangamiza bonyeza kiungo kifuatacho:

 

108-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Madhambi Saba Yanayoangamiza

 

 

 

 

 

Share