Masarufu Ya Wazazi

 

SWALI:

asalam aleykum,mume wangu amejenga nyumba mbili al-hamdulilah tunamshukuru m/mungu kwa kutupa uwezo, na kodi inapokewa na wazazi wake,sisi hatuziulizi kodi wala hatujuwi kodi ni ngapi,mimi  kila mwezi ninampelekea mamangu pesa kidogo hatupeleki kwa wazazi wake mume kwa sababu wanapokea kodi za nyumba tulozijenga, ni sawa mimi kumpelekea mamangu pesa kila mwezi na hatupeleki kwa wazazi wake? JAZAKUMULLAHU KHEIR

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 Shukrani dada yetu kwa swali lako hilo zuri la mas-ala ya kijamii. Tunawaombea kwa Allaah Aliyetukuka muzidi kuwafanyia wema wazazi wenu kwani katika kufanya hivyo munakuwa ni wenye kukamilika katika Dini yenu.

Hakika ni kuwa sisi Waislamu tumeamriwa na Allaah Aliyetukuka pamoja na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tuwe ni wenye kuwafanyia wema wazazi wetu na haswa mama. Allaah Aliyetukuka Anatuambia: “Na Mola wako Amehukumu kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu na Ameagiza kuwafanyia wema mkubwa wazazi” (17: 23).

Pia, “Na Tumemuusia mwanadamu kuwafanyia ihsani wazazi wake – mama yake ameichukua mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu…” (31: 14).

Insha Allaah, Allaah Aliyetukuka Atawatilia baraka kubwa kwa kuwajengea nyumba wazazi wa mume ambao kwayo hupata kodi na riziki ya kuendesha maisha yao. Hiyo ni moja katika ihsani lakini ikiwa yapo yaziada ambao mwaweza kuwanyia itakuwa kheri zaidi kwenu nyinyi kwa kuijaliza mizani yenu ya amali njema. Musifikirie hata kwa mara moja kuwa kwa kuwa mumewajengea nyumba basi hamna jukumu tena kwao.

Pia katika kuwajengea nyumba huenda mkawa mmewapa kama tunu, hivyo, hilo haliwazuii nyingi kuwapatia pesa nyingine za kuwasaidia ikiwa mna uwezo huo wala msichoke kuwasaidia. Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Awazidishie moyo huo wa kuwaangalia wazazi wenu pamoja na kuwafanyia ihsani iliyo njema na kubwa zaidi.

Wewe kumpelekea mamako pesa za kumsaidia ni katika ihsani na wema na endelea mwenendo huo huo wala usiache mpaka iwe huna cha kumpelekea. Ikiwa utapata kidogo mpelekee kulingana na uwezo wako na ikiwa utapata katika mapato yako kingi basi pia muongezee kulingana na uwezo wako.

Kwa hiyo, wewe endelea kumpelekea mamako pesa ambazo zitamsaidia na ikiwa pia mnaweza kuwapelekea wazazi wa mume wako pia itakuwa ni ziada njema kwenye amali zenu ambazo mtazikuta Kesho Akhera.

Tunawaombea tawfiki katika hilo na Allaah Awabariki hapa duniani na Kesho Akhera. Awapatie yaliyo mema hapa duniani na mema Kesho Akhera na Atuepushe sote na adhabu ya Moto wa Jahanamu.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share