157-Aayah Na Mafunzo: Nabiy ‘Iysaa Amenyanyuliwa Mbinguni Na Atateremka Kabla Qiyaamah

 

Aayah Na Mafunzo

An-Nisaa

  Nabiy ‘Iysaa Amenyanyuliwa Mbinguni Na Atateremka Kabla Qiyaamah

 

Alhidaaya.com

 

 

 Kauli Zake Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 وَقَوْلِهِمْ إِنَّا قَتَلْنَا الْمَسِيحَ عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ رَسُولَ اللَّـهِ وَمَا قَتَلُوهُ وَمَا صَلَبُوهُ وَلَـٰكِن شُبِّهَ لَهُمْ ۚ وَإِنَّ الَّذِينَ اخْتَلَفُوا فِيهِ لَفِي شَكٍّ مِّنْهُ ۚ مَا لَهُم بِهِ مِنْ عِلْمٍ إِلَّا اتِّبَاعَ الظَّنِّ ۚ وَمَا قَتَلُوهُ يَقِينًا ﴿١٥٧﴾

Na kusema kwao (kwa kujifaharisha): Hakika sisi tumemuua Al-Masiyh ‘Iysaa mwana wa Maryam, Rasuli wa Allaah. Na hawakumuua wala hawakumsulubu lakini walishabihishiwa tu. Na hakika wale waliokhitilafiana katika hayo, kwa hakika wamo katika shaka nayo. Hawana ujuzi nalo kabisa isipokuwa kufuata dhana tu. Na kwa yakini hawakumuua. 

 

بَل رَّفَعَهُ اللَّـهُ إِلَيْهِ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ عَزِيزًا حَكِيمًا ﴿١٥٨﴾

Bali Allaah Alimnyanyua Kwake. Na Allaah daima Ni Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote.  

 

 

وَإِن مِّنْ أَهْلِ الْكِتَابِ إِلَّا لَيُؤْمِنَنَّ بِهِ قَبْلَ مَوْتِهِ ۖ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكُونُ عَلَيْهِمْ شَهِيدًا ﴿١٥٩﴾

Na hakuna yeyote katika Watu wa Kitabu ila atamwamini kabla ya kufa kwake. Na Siku ya Qiyaamah atakuwa shahidi juu yao.

[An-Nisaa (4:157-159)]

 

Mafunzo:

 

Hizi ni Aayah dalili zinazothibitisha kwamba Nabiy ‘Iysaa (عليه السلام) hakufishwa bali amenyanyuliwa na Allaah mbinguni.

 

Pia ni dalili bayana kwa wanaokanusha kuteremka kwa Nabiy ‘Iysaa (عليه السلام) zama za mwisho kukaribia Qiyaamah kama ni dalili mojawapo kubwa ya kutokea Qiyaamah. Nabiy ‘Iysaa ('Alayhis-Salaam) atateremka kutoka mbinguni kuja duniani kama ni miongoni mwa alama kubwa za Qiyaamah. Na pia kuna Ahaadiyth nyingi nyingine za Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) zimethibiti baadhi yake ni:

 

((وَالَّذِي نَفْسِي بِيَدِهِ لَيُوشِكَنَّ أَنْ يَنْزِلَ فِيكُمْ ابْنُ مَرْيَمَ حَكَمًا مُقْسِطًا)) 

((Naapa kwa Yule Ambaye nafsi yangu iko Mikononi Mwake, hivi karibuni atateremka kwenu mwana wa Maryam ('Iysaa) akiwa ni kiongozi muadilifu)). [Al-Bukhaariy, Muslim].

 

Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Naapa kwa Yule Ambaye nafsi yangu iko Mikononi Mwake, hivi karibuni atateremka kwenu mwana wa Maryam ('Iysaa) akiwa ni kiongozi muadilifu na atavunja misalaba, na kuua nguruwe, na ataondosha jizyah (ushuru kutoka kwa wasio Waislamu ambao wamo katika himaya ya serikali ya Waislamu). Kisha kutakuwa na mali nyingi hadi itafikia kuwa hakuna mtu wa kupokea sadaka. Wakati huu sijda moja itakuwa ni bora kwao kuliko maisha haya na yote yaliyomo (katika dunia).” Kisha Abuu Huraryah akasema: Someni mkipenda:

 

وَإِن مِّنْ أَهْلِ الْكِتَابِ إِلَّا لَيُؤْمِنَنَّ بِهِ قَبْلَ مَوْتِهِ ۖ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكُونُ عَلَيْهِمْ شَهِيدًا ﴿١٥٩﴾

Na hakuna yeyote katika Watu wa Kitabu ila atamwamini kabla ya kufa kwake. Na Siku ya Qiyaamah atakuwa shahidi juu yao.  (4: 159)   [Al-Bukhaariy]

 

 

Na pia:

 

Na pia: Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mtakuwaje atakapoteremka Al-Masiyh, mwana wa Maryam (‘Iysaa) akiwa Imaam wenu miongoni mwenu wenyewe?” [Al-Bukhaariy].

 

Na pia amesema Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): “Manabii ni bin-‘ammi, mama zao tofauti, lakini Dini yao moja. Mimi ndiye mwenye haki zaidi kwa ‘Iysaa mwana wa Maryam kuliko yeyote mwengine, kwani hakukuwa na Nabiy baina yake na mimi. Atateremka na mtakapomuona mtamtambua. Ni mtu aliyeumbika vizuri, (rangi ya ngozi yake) baina nyekundu na nyeupe. Atateremka akiwa amevaa nguo mbili ndefu, rangi ya njano isiyokoza. Kichwa chake kitakuwa kina michirizi ya matone ya maji, japokuwa umande haukugusa. Atavunja misalaba, ataua nguruwe, ataondosha jizyah na atawaita watu katika Uislamu. Wakati huu, Allaah Ataangamiza dini zote isipokuwa Uislamu na Allaah Atamuangamiza Masiyh-Dajjaal. Usalama utajaa ardhini, hadi kwamba simba watachanganyika na ngamia, chui na ng'ombe, fisi na kondoo, watoto watacheza na nyoka na hawatowadhuru. ‘Iysaa atabakia muda wa miaka arubaini kisha atafariki, na Waislamu watamswalia Swalaah ya janaazah.” [Abuu Daawuwd, Ahmad na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Al-Jaami’ (2182)]

 

Maelezo zaidi rejea kiungo kifuatacho:

 

055-Nabiy ‘Iysaa ('Alayhis-Salaam) Hakufa Na Atakuwa Katika Alama Za Qiyaamah

 

 

 

 

Share