077-Asbaabun-Nuzuwul: Hakika wale wanaobadilisha ahadi ya Allaah

 أسْبابُ النُّزُول

Asbaabun-Nuzuwl

Sababu Za Kuteremshwa (Baadhi Ya Aayaat Za Qur-aan)

Imekusanywa na: Alhidaaya.com

 

 

Aal-‘Imraan 077-Hakika wale wanaobadilisha ahadi ya Allaah

 

 

إِنَّ الَّذِينَ يَشْتَرُونَ بِعَهْدِ اللَّـهِ وَأَيْمَانِهِمْ ثَمَنًا قَلِيلًا أُولَـٰئِكَ لَا خَلَاقَ لَهُمْ فِي الْآخِرَةِ وَلَا يُكَلِّمُهُمُ اللَّـهُ وَلَا يَنظُرُ إِلَيْهِمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَلَا يُزَكِّيهِمْ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٧٧﴾

77. Hakika wale wanaobadilisha ahadi ya Allaah na viapo vyao kwa thamani ndogo; hao hawana sehemu yoyote katika Aakhirah na wala Allaah Hatowasemesha na wala Hatowatazama Siku Ya Qiyaamah na wala Hatowatakasa na watapata adhabu iumizayo.

 

Sababun-Nuzuwl:

 

Aayah hii imeteremka kama alivyohadithia ’Abdullaah bin Mas’uwd(رضي الله عنه) kwamba: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alisema: ”Yeyote atakayeapa kiapo ili achukue mali ya Muislamu (bila ya haki) atakutana na Allaah Akiwa Amemghadhibikia.” Hapo Allaah Akateremsha kusadikisha kauli hii: Hakika wale wanaobadilisha ahadi ya Allaah na viapo vyao kwa thamani ndogo; hao hawana sehemu yoyote katika Aakhirah...” mpaka mwisho wa Aayah (3: 77). Akasema: Kisha akaingia Al-Ash’ath bin Qays akasema: Je, ’Abdur-Rahmaan anakuhadithieni nini? Tukasema: Kadhaa wa kadhaa. Akasema: Aayah hii imeteremshiwa kuhusu mimi; nilikuwa na kisima katika ardhi ya bin ’ammi yangu (lakini alikanusha kuwa similiki). Kisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akaniambia: ”Ima ulete ushahidi au yeye (bin ’ammi yako) atatoa kiapo (kuthibitisha madai yake).” Nikasema: Nina hakika atatoa kiapo (cha uongo) ee Rasuli wa Allaah. Kisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: ”Atakayeapa kwa ajili ya kuchukua ardhi ya Muislamu (bila haki) hali ya kuwa ni muongo katika kiapo chake, atakutana na Allaah Akiwa Amemghadhibikia.” [Al-Bukhaariy].

 

Na pia imeteremka kwa mtu mmoja ambaye aliisimamisha bidhaa yake sokoni  kisha akaapa juu hiyo bidhaa kuwa amekwishapewa thamani kubwa kwenye hiyo bidhaa zaidi ya hiyo anayotaka kupewa,  hali ya kuwa hajapewa thamani hiyo, na aliapa kiapo hicho ili amshawishi mmoja katika Waislamu ainunue hiyo bidhaa, hapo ikateremka hii Aayah [Amehadithia Ibn Abi Awfaa (رضي الله عنه) ameipokea Al-Bukhaariy].

 

Share