188-Asbaabun-Nuzuwul: Usiwadhanie Kabisa Wale Wanaofurahia Kwa Waliyopewa

أسْبابُ النُّزُول

Asbaabun-Nuzuwl

Sababu Za Kuteremshwa (Baadhi Ya Aayaat Za Qur-aan)

Imekusanywa na: Alhidaaya.com

 

 

Aal-‘Imraan   188-Usiwadhanie kabisa wale wanaofurahia kwa waliyopewa

 

لَا تَحْسَبَنَّ الَّذِينَ يَفْرَحُونَ بِمَا أَتَوا وَّيُحِبُّونَ أَن يُحْمَدُوا بِمَا لَمْ يَفْعَلُوا فَلَا تَحْسَبَنَّهُم بِمَفَازَةٍ مِّنَ الْعَذَابِ ۖ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿١٨٨﴾ 

188. Usiwadhanie kabisa wale wanaofurahia kwa waliyopewa na wanapenda wasifiwe kwa wasiyoyatenda. Usiwadhanie kabisa kuwa watasalimika na adhabu. Nao watapata adhabu iumizayo.

 

 

Sababun-Nuzuwl:

 

Aayah hii imeteremka kuhusu wanafiki  kama alivyohadithia Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (رضي الله عنه) kwamba: “Katika zama za Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), pale alipokuwa anatoka Nabiy  (صلى الله عليه وآله وسلم) kwenda vitani, wanafiki walimkhalifu na kubakia nyuma wasiende vitani, na wakifurahi kwa kubakia kwao nyuma kinyume na (alivyofanya) Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم). Kisha pale alipokuwa anarudi Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) walitoa nyudhuru kwake na wakiapa na wakipenda wasifiwe kwa hayo waliyoyafanya, hapo ikateremka (hii Aayah…)” [Amehadithia Abuu Sai’yd (رضي الله عنه), ameipokea Al-Bukhaariy na Muslim].

 

Pia, Marwaan alimwambia mlinzi wake, Rafiy’ aende kwa Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) kumwambia: “Ingekuwa kila mtu miongoni mwetu anafurahia kwa aliyoyafanya na kupenda kusifiwa kwa ambayo hakuyatenda, basi ataadhibiwa na sisi tutaadhibiwa.” Ibn ‘Abbaas akasema: Mna nini na Aayah hii? Hakika Aayah hii imeteremshwa kuhusu Ahlul-Kitaab. kisha akasoma Aayah (3: 187): “Na pindi Allaah Alipochukua fungamano la wale waliopewa Kitabu (Allaah Akawaambia): Bila shaka mtakibainisha kwa watu na wala hamtokificha…” (3: 187 Suwrah hii Aal-Imraan) kisha Ibn ‘Abbaas akasoma: “Usiwadhanie kabisa wale wanaofurahia kwa waliyopewa na wanapenda wasifiwe kwa wasiyoyatenda…” kisha akasema: “Waliulizwa jambo (waliokuwa na ujuzi nalo) na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) lakini walimficha ujuzi wake hilo jambo na wakamuambia kinyume cha uhalisia wa hilo jambo, kisha wakaondoka wakifurahia kuwa wamemuongopea wakataka wasifiwe kwa hayo waliyoyaficha.” [Muslim].

 

 

Share