060-Asbaabun-Nuzuwul: Je, huoni wale wanaodai kwamba wao wameamini yaliyoteremshwa kwako...

أسْبابُ النُّزُول

Asbaabun-Nuzuwl

Sababu Za Kuteremshwa (Baadhi Ya Aayaat Za Qur-aan)

Imekusanywa na: Alhidaaya.com

 

 

An-Nisaa 060-Je, huoni wale wanaodai kwamba wao wameamini yaliyoteremshwa kwako

 

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ يَزْعُمُونَ أَنَّهُمْ آمَنُوا بِمَا أُنزِلَ إِلَيْكَ وَمَا أُنزِلَ مِن قَبْلِكَ يُرِيدُونَ أَن يَتَحَاكَمُوا إِلَى الطَّاغُوتِ وَقَدْ أُمِرُوا أَن يَكْفُرُوا بِهِ وَيُرِيدُ الشَّيْطَانُ أَن يُضِلَّهُمْ ضَلَالًا بَعِيدًا ﴿٦٠﴾

60. Je, huoni wale wanaodai kwamba wao wameamini yaliyoteremshwa kwako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) na yale yaliyoteremshwa kabla yako; wanataka wahukumiane kwa twaghuti (ubatilifu) na hali wameamrishwa wakanushe hiyo. Na shaytwaan anataka awapoteze upotofu wa mbali.

 

Sababun-Nuzuwl:

 

Aayah hii pamoja na mbili zinazofuatia (4: 60-62) zimeteremka kama alivyohadithia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) kuwa alikuwa Abuu Barzat Al-Aslamiyy ni Kuhani akitoa hukumu kuhusu magomvi yanayotokea baina ya Mayahudi. Siku moja baadhi ya watu katika washirikina walileta magomvi kwake, kisha Allaah Akateremsha Aayah hii: “Je, huoni wale wanaodai kwamba wao wameamini yaliyoteremshwa kwako…”  [Abuu Haatim Atw-Twabaraaniy, Ibn Hajar Al-‘Asqalaaniy (4/19) amesema isnaad yake ni nzuri].

 

Sababun-Nuzuwl nyingine pia ya Aayah hii ni kwamba waligombana mtu kutoka Answaar na Myahudi kisha Myahudi akasema: “Twende kwa Muhammad akatuhukumu.” Na yule Answaar akasema: “Twende kwa Ka’ab Al-Ashraf.” Imesemwa pia kuwa miongoni mwa wanafiki walliokuwa wakijidai kuwa ni Waislamu, lakini huku wakitafuta hukmu za kijaahiliyyah. [Tafsiyr Ibn Kathiyr].

 

Pia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) amesema: “Abuu Barzah Al-Aslamiy alikuwa mtabiri na akihukumu magomvi ya Mayahudi. Baadhi ya Waislamu walipomwendea kutaka awahukumu, Allaah (سبحانه وتعالى) Akateremsha: “Je, huoni wale wanaodai kwamba wao wameamini yaliyoteremshwa kwako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) na yale yaliyoteremshwa kabla yako… mpaka: “Wa-Allaahi hatukutaka ila mazuri na mapatano.” (4: 60-62) [Atw-Twabaraaniy].

 

 

Share