006-Asbaabun-Nuzuwl: Al-Maaidah Aayah 006: يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا قُمْتُمْ إِلَى الصَّلَاةِ فَاغْسِلُوا وُجُوهَكُمْ وَأَيْدِيَكُمْ

أسْبابُ النُّزُول

Asbaabun-Nuzuwl

Sababu Za Kuteremshwa (Baadhi Ya Aayaat Za Qur-aan)

Imekusanywa na: Alhidaaya.com

 

 

Al-Maaidah    006-Sababu ya kuteremshwa hukmu ya tayammum:

 

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا قُمْتُمْ إِلَى الصَّلَاةِ فَاغْسِلُوا وُجُوهَكُمْ وَأَيْدِيَكُمْ إِلَى الْمَرَافِقِ وَامْسَحُوا بِرُءُوسِكُمْ وَأَرْجُلَكُمْ إِلَى الْكَعْبَيْنِ ۚ وَإِن كُنتُمْ جُنُبًا فَاطَّهَّرُوا ۚ وَإِن كُنتُم مَّرْضَىٰ أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ أَوْ جَاءَ أَحَدٌ مِّنكُم مِّنَ الْغَائِطِ أَوْ لَامَسْتُمُ النِّسَاءَ فَلَمْ تَجِدُوا مَاءً فَتَيَمَّمُوا صَعِيدًا طَيِّبًا فَامْسَحُوا بِوُجُوهِكُمْ وَأَيْدِيكُم مِّنْهُ ۚ مَا يُرِيدُ اللَّـهُ لِيَجْعَلَ عَلَيْكُم مِّنْ حَرَجٍ وَلَـٰكِن يُرِيدُ لِيُطَهِّرَكُمْ وَلِيُتِمَّ نِعْمَتَهُ عَلَيْكُمْ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴿٦﴾

Enyi walioamini!  Mnaposimama kwa ajili ya Swalaah, osheni nyuso zenu na mikono yenu mpaka kwenye visugudi, na panguseni (kwa kupaka maji) vichwa vyenu na (osheni) miguu yenu hadi vifundoni. Na mkiwa na janaba basi jitwaharisheni. Na mkiwa wagonjwa au mko safarini au mmoja wenu ametoka msalani, au mmewagusa wanawake, kisha hamkupata maji, basi ikusudieni ardhi safi ya mchanga (mtayammam), panguseni kwayo nyuso zenu na mikono yenu. Allaah Hataki kukufanyieni magumu, lakini Anataka kukutwaharisheni na Akutimizieni Neema Yake juu yenu ili mpate kushukuru.

 

Sababun-Nuzuwl

 

Sababu Ya Kuteremshwa Hukmu Ya Tayammum (Kuikusudia Ardhi Safi Ya Mchanga Kwa Ajili Ya Wudhuu):

 

Mama wa ‘Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) amehadithia: “Tulikwenda katika moja ya safari tukafika Al-Baydaa au Dhaatul-Jaysh ambako kidani changu kilivunjika (na kikapotea). Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akawa anakitafuta, kisha pia watu wengineo wakainuka kukitafuta. Hapakuweko na maji sehemu hiyo, basi watu wakamwendea Abuu Bakr Asw-Swiddiyq na kusema: Huoni alivyofanya ‘Aaishah? Kamfanya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) pamoja na watu wakae sehemu ambayo hakuna maji! Abuu Bakr akaja wakati Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa amelaa akiwa amelaza kichwa chake mapajani mwangu. Akaniambia: Umemzuia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na watu sehemu ambako hakuna maji na wala hawana (akiba ya) maji. Basi akanigombesha na akasema Aliyomjaalia (Allaah) kusema kuhusu mimi na akanipiga ubavuni kwa mkono wake. Hakuna kilichonizuia kusogea (kutokana na maumivu) isipokuwa kwa vile Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alilala mapajani mwangu. Hapo Allaah Akateremsha Aayah ya tayammum (kutia Wudhuu kwa mchanga), basi wakatayammam. ‘Usayd bin Al-Hudhwayr akasema: Ee ahli ya Abuu Bakr! Hii si baraka ya kwanza kwenu. Kisha akaendeshwa ngamia ambaye nilikuwa nimempanda na tukakipata kidani kilichokuwa (kimejificha) chini yake.” [Al-Bukhaariy]

 

 

Share