Skip navigation.
Home kabah

Maana Ya Ibada

Yuusuf Abdur-Rahmaan Mgaza


 

MAANA HALISI YA IBAADA

 

Lengo kubwa na la msingi katika Dini ni kujua watu Muumba wao na wakamuabudu ipasavyo Yeye peke Yake pasi na kumshirikisha na kitu chochote.


Kwa hakika uislamu umeweka Ibaada nyingi tu,na ukaziweka bayana namna ya kumuabudu Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'ala) pamoja na kumtwii kama vile Swalah, Dua, Dhikri, Swaumu, Hijja, Zakaah, Shahada, Kuamrishana mema na kukatazana mabaya, na Kulinganiana katika Dini ya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'ala), Kupigana jihadi katika kuitetea Dini ya Mwenyezi Mungu, na kusoma Qur-aan, na mengineyo miongoni mwa mambo ya Ibaada ambazo zitamfanya mtu awe karibu mno na Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'ala).


Ama hakika maana halisi ya Ibaada ni kila jambo zuri atakalolifanya mwanaadamu na Mwenyezi Mungu Akawa radhi nalo (Akaliridhia), au ni kuacha mwanaadamu makatazo ya Mwenyezi Mungu(Subhaanahu wa Ta'ala) na kusalimika na shari Zake.


Uislamu umeziweka bayana na kuzipambanua Ibaada, na pia ukaziwekea mipaka yake, hakuna ruhusa kwa mtu wa aina yeyote ile kuweka Ibaada yake kinyume na Ibaada  ambazo Ameziweka Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'ala) ili Mwanaadamu asije akapetuka mipaka kwa Ibaada yake hiyo aliyo iweka na kukosa Thawabu na malipo kutoka mbele za Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'ala).


Na ni sharti katika kufanya Ibaada kutia Nia ya kweli na kukusudia kwa Ibaada hiyo Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'ala) pekee, ili isije ikaingia katika Riyaa na unafiki, kwani Riyaa na unafiki ni zinaporomosha malipo kutoka mbele za muumba wetu.

 

 

FAIDA ZA IBAADA

 

Ibaada katika Uislamu ina faida nyingi za kijamii na za kinafsi (kiroho) na kiafya kwa mwanaadamu, kwani zinamfanya mtu aweze kuepukana na Kibri na Hadaa.

 

1.      Mtu anaporukuu na kusujudu katika Swalah nafsi yake inahisi unyenyekevu mbele ya Mola wake.

2.      Vilevile kujitwaharisha kwa ajili ya Swalah kunaleta Afya na mandhari mazuri.

3.      Kufunga Swaumu kunamfanya mtu ahisi machungu na tabu za umasikini, na kunaleta afya katika mwili.

4.      Na Swala za jamaa zinatufundisha kujuana kati ya Waislamu na kuzoeana na kusaidiana wenyewe kwa wenyewe.

5.      Na Zakaah pamoja na Sadaka nyinginezo za kimali zinachangia katika kuondoa matatizo mbalimbali ya jamii kiuchumi.

6.      Hijja inatufundisha Subra na uvumilivu kwa kukutana na watu mbalimbali na kujuana nao na kusaidiana katika mambo ambayo yatawanufaisha Waislamu wengine na Uislamu kwa ujumla.

7.      Na katika Du'aa (Maombi) Mwanaadamu anahisi haja yake kubwa kwa Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'ala) na kuitakasha Nafsi yake kutokana na kibri na hadaa, pia huwaombea wazazi wake na Waislamu wengine kheri, kwa hapo hatakua na majivuno na kujiona, na anajifunza kupenda kheri katika kila jambo, na watu wote na hujengeka katika Tabia nzuri.

 

Hivyo basi Ibaada zote kwa hakika zinamlea mtu na kumfundisha Tabia nzuri na uhusiano mwema wenye kusalimika na maovu, na pia zinachangia katika kuzitengeneza na kuziendeleza jamii.

 

Dini yetu tukufu ya Kiislamu imetukataza kuacha kufanya kazi za kuyajenga maisha yetu ya Duniani na kujishughulisha na Ibaada za kuijenga Akhera tu, bali pia na kuijenga Dunia, kwani hizo kazi za kuijenga Dunia pia huitakidiwa kuwa ni Ibaada tosha ikiwa zitaendeshwa kwa kufuata misingi na mafundisho sahihi ya Dini yetu, Mwenyezi Mungu Ameliweka wazi hilo pale Aliposema;

[Na utafute kwa yale aliyokupa Mwenyezi Mungu makazi mazuri ya akhera, wala usisahau sehemu yako ya Dunia, na ufanye wema kama Mwenyezi Mungu alivyokufanyia, wala usitafute kufanya ufisadi katika nchi, bila shaka Mwenyezi Mungu Hawapendi mafisadi] (28: 77).

Ewe Mola wetu Tupe katika Dunia wema na Tupe pia katika akhera wema, na Utukinge na adhabu ya moto, na Utujaalie kuwa ni katika waja wako walio wema.

 

Aamiyn.