Wakati Wa Mwisho Wa Swalaah Ya Ishaa

 

SWALI:

Asalam Aleykum

Je sala ya Isha mwisho wake wa kuisali ni saa ngapi 

 


 

JIBU: 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaana wa Ta'aala) Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Qiyaamah.

Nyakati za Swalah mwanzo wake na mwisho wake zimetajawa katika Hadiyth ifuatayo: 

عن عبد الله بن عمرو أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال (( وقت الظهر إذا زالت الشمس وكان ظل الرجل كطوله ما لم يحضر العصر ووقت العصر ما لم تصفر الشمس ووقت صلاة المغرب ما لم يغب الشفق ووقت صلاة العشاء إلى نصف الليل الأوسط ووقت صلاة الصبح من طلوع الفجر ما لم تطلع الشمس فإذا طلعت الشمس فأمسك عن الصلاة فإنها تطلع بين قرني شيطان))  مسلم  

Imetoka kwa 'Abdullah bin 'Amru (Radhiya Allahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amesema: ((Wakati wa Adhuhuri unabakia mpaka jua linapopita kilele chake, na kivuli cha mtu kinakuwa ni  sawa na urefu wa mtu  na madamu wakati wa Alasiri bado haukufika. Na wakati wa Alasiri unaendelea kubakia madamu jua halikugeuka kuwa manjano. Na wakati wa Magharibi unabakia madamu rangi nyekundu ingalipo, na wakati wa 'Ishaa unabakia mpaka katikati ya usiku. Na wakati wa Alfajiri unaanza baada ya kupambazuka hadi kabla ya jua kuchomoza, acheni kuswali wakati huo kwani jua huchomoza baina ya pembe mbili za shaytwaani)) [Muslim]

 Swalah ya 'Ishaa inapaswa kuswaliwa kabla ya kufika katikati ya usiku au thuluthi ya usiku (kwa mapokezi mengine). Na hairuhusiwi kuichelewesha hadi wakati huo kwa sababu Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((وَقْتُ العِشاء إلى نصف الليل))   رواه مسلم

((Wakati wa 'Ishaa ni hadi katikati ya usiku)) [Muslim]

Kuiswali katikati ya usiku ni kulingana na urefu wa nyakati za usiku, kwa sababu katika baadhi ya nchi siku za baridi usiku huwa mrefu na siku za joto usiku huwa mfupi.  Mfano ikiwa usiku una masaa kumi, basi haifai kuichelewesha hadi mwisho wa masaa matano baada ya kuadhiniwa.

Ni bora zaidi kuiswali katika thuluthi ya mwanzo ya usiku. Mtu akiiswali mwanzo wa wakati ya 'Ishaa yaani baada ya kuadhiniwa, hakuna ubaya kufanya hivyo, lakini ni inapendekezeka zaidi kuichelewesha kwa sababu Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akipendekeza kucheleweshwa Swalah ya 'Ishaa kama ilivyo katika dalili ifuatayo:

عن أبي هريرة رضي الله عنه قال : قال رسول الله صلى الله عليه وعلى آله وسلم : (( لولا أن أشق على أمتي لأمرتهم أن يؤخروا العشاء إلى ثلث الليل ، أو نصفه))    رواه الترمذي

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allahu 'anhu) ambaye amesema: Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Lau kama nisingelikuwa nachelea mashaka kwa Ummah wangu, ningeliwaamrisha waicheleweshe (Swalah ya) 'Ishaa hadi thuluthi ya usiku au nusu yake)) [At-Tirmidhiy]

Hata hivyo ufahamu wa Maulamaa pamoja na hadiyth hizo, umekhitilafiana kuhusu mwisho wa Swalah ya 'Ishaa katika kauli tatu:

Kauli ya kwanza:

Mwisho wake ni hadi theluthi ya usiku: Nayo ni rai ya Imaam Ash-Shaafi'iy katika moja ya rai zake (ingawa kwenye kitabu chake 'AL-UMM' anasema ikipita theluthi ya usiku basi Swalah ya 'Ishaa imepita), na pia ni rai ya Imaam Abu Haniyfah, na moja kati ya rai ya madhehebu ya Imaam Maalik. Wameegemea katika rai hii kwa sababu ya hadiyth ya Jibriyl ya kumswalisha Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

Kauli ya pili:

Mwisho wake ni hadi nusu usiku: Nayo ni rai ya Ath-Thawriy, Ibnul-Mubaarak na Is-haaq na Abu Thawr, Imaam Shaafi'iy katika kauli yake nyingine kama tulivyoona juu kwenye kitabu chake cha Al-Umm. Nao wameegemeza msimamo wao huu kwa hadiyth ya 'Abdullah bin 'Amru tuliyoiona nyuma.

Kauli ya tatu:

Hadi inapopambazuka Alfajiri ya kweli: Nayo ni rai ya 'Atwaa na Twaawuus na 'Ikrimah, na Daawuud Adhwaahiriy. Nao wameitolea hadiyth ya Abu Qataadah ya kuonyesha kuwa inaweza Swalah kuswaliwa hadi wakati wa Swalah nyingine endapo mtu amekosa ule wakati wake.

Lakini rai iliyo sahihi kabisa ni kauli ya pili kutokana na Hadiyth iliyo na nguvu kabisa ambayo imeweka wazi mpaka wa mwisho wa Swalah ya 'Ishaa, nayo ni Hadiyth ya 'Abdullah bin 'Amru:

 ((وَقْتُ العِشاء إلى نصف الليل))   رواه مسلم

((Wakati wa 'Ishaa ni hadi katikati ya usiku)) [Muslim]

Hata hivyo, kunawezekana kuzidisha muda huo kidogo hadi usiku wa manane kutokana na hadiyth tuliyoiona nyuma lakini kwa dharura na si kwa khiyari.

Jambo jingine pia la kuongeza ni kuwa haipendezi kulala kabla ya Swalah ya 'Ishaa na kuzungumza baada yake. Kuchukizika huko kulala kabla ya Swalah ya 'Ishaa huenda ni kwa sababu asije mtu akapitiwa na akaikosa hiyo Swalah au akaikosa Jama'ah msikitini. Na ama machukizo ya kupiga soga baada ya Swalah ya 'Ishaa huenda ni kwa sababu ya watu wakakesha kuzungumza na Swalah ya Alfajiri ikawapita au wakajikuta wamezungumza na kufika karibu na Alfajiri wakawa hawajiwezi na kwenda kulala matokeo yake Swalah ikawapita. Pia kuna kuikosa Qiyaamul Layl. Hata hivyo, kama watu watakaa kwa mazungumzo ya dini, hilo halikatazwi maana Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikaa baada ya 'Ishaa yeye na Abu Bakr na 'Umar (Radhiya Allahu 'anhuma) wakijadili masuala ya Waislam.

 Na Allaah Anajua zaidi

 

Share