Kwa Nini Mtu Akipita Mbele Ya Mwenye Kuswali Swalaah Hukatika?

 

SWALI:

Assalaam alaykum, hivi ni kwa nini ukipita mbele ya mtu akiwa anaswali unamkatisha swala kwa sababu zipi?

 


 

JIBU:

AlhamduliLlaah - Himdi Na Sifa Zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Swalah ni fardhi muhimu kabisa na kuiswali inavyopasa ni wajib na amri kutoka kwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akama alivyosema:

((صلوا كما رأيتموني أصلي)) البخاري

 ((Swalini kama mlivyoniona naswali)) [Al-Bukhaariy]

Vile vile kila amri anayotupa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) huwa ni amri kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kama Anavyosema:

((وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا))

((Na anachokupeni Mtume chukueni, na anachokukatazeni jiepusheni nacho)) [Al-Hashr:7]

Wakati mwingine amri tunazopata kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na Mtume Wake (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), ikiwa ni amri ya kutenda jambo au kuliacha huwa tunafahamu sababu zake. Ama mara nyingine huwa hatufahamu sababu zake, lakini tunapaswa tusikilize, tuamini na tutii bila ya kutaka kuchungua sana na kuuliza zaidi na zaidi hadi kufikia mtu kuitia imani yake shaka na mwisho hata akatumbukia katika kufru. Na kufuata amri tunazopewa na Allah au Mtume Wake hata kama hatujui sababu zake ni katika sifa ya Waumini:

((آمَنَ الرَّسُولُ بِمَا أُنزِلَ إِلَيْهِ مِن رَّبِّهِ وَالْمُؤْمِنُونَ كُلٌّ آمَنَ بِاللّهِ وَمَلآئِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ لاَ نُفَرِّقُ بَيْنَ أَحَدٍ مِّن رُّسُلِهِ وَقَالُواْ سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا غُفْرَانَكَ رَبَّنَا وَإِلَيْكَ الْمَصِيرُ))

((Mtume ameamini yaliyoteremshwa kwake kutoka kwa Mola wake, na Waumini vile vile. Wote wamemuamini Allah, na Malaika Wake, na Vitabu Vyake na Mitume Yake. Hatutafautishi baina ya yeyote katika Mitume Yake, na (Waumini) husema: Tumesikia na tumetii. Tunakutaka maghfira Mola  wetu! Na marejeo ni Kwako)) [Al-Baqarah:285]

Vilevile jambo lolote lile likiwa lishaamuliwa na Allah na Mtume Wake japokuwa hatuelewi hekima yake au hatujaridhika nalo, wajibu wetu ni kufuata na kutii ili kuthibitisha utii wetu na imani thabiti kuwa kila kiamrishwacho au kupangwa na Allah na Mtume kwetu sisi, basi huwa ni chenye manufaa na kheri kwetu sisi. Anasema Allah (Subhaanahu wa Ta'ala):

((وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ وَمَن يَعْصِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا))

((Haiwi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke kuwa na khiari katika jambo, Allah na Mtume Wake wanapokata shauri katika jambo lao. Na mwenye kumuasi Allah na Mtume wake basi hakika amepotea upotofu ulio wazi)) [Al-Ahzaab:36]

Bila shaka katika hayo tusiyoyafahamu sababu zake huwa na hikma ndani yake kwani Yeye Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ndiye Mjuzi wa kila kitu. 

Kwa hiyo napotaka kuswali, ni vema kuweka sutra yaani kizuizi kama vile meza ndogo, stuli, kiti, fimbo, mkoba, koti, na kadhalika mbele yako. Na hili ni jambo llililosisitizwa sana na Maulamaa wengine wamesema ni wajibu kutokana na hadiyth zilivyokuja. Ametuamrisha hilo Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Swalah zetu kama alivyokuwa akiswali yeye na kama ilivyokuja katika Hadiyth nyingi, chache zifuatazo:

  كان   صلى الله عليه وسلم  يقفُ قريبًا من السُّتْرة ، فكانَ بينَه وبين الجِدار ثلاثة أذرع  - (البخاري  و أحمد)   
 و بين موضِع سجودِه والجدار ممرّ شاة   
(البخاري و مسلم)

Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisimama karibu na sutrah, baina yake na ukuta ni masafa ya dhiraa tatu.  [Al-Bukhaariy na Ahmad] …na nafasi iliyokuwepo baina ya sehemu anayosujudia na ukuta (kulikuweko) nafasi ya kutosha ya kuweza kupita kondoo. [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

و كان يقول  ((لا تُصَلِّ إلا إلى سُترة ، ولا تدع أحدا يمر بين يديك ، فإنْ أبى فلْتُقاتِله ؛ فإن معه القرين )) ابن خزيمة في صحيحه

Alikuwa akisema: ((Msiswali isipokuwa kuna Sutrah (kizuizi) mbele yenu, na msimuachie mtu kupita mbele yenu, lakini kama mtu akiendelea (kujaribu kupita) basi mzuieni kwani yuko pamoja na shaytwaani)) Ibn Khuzaymah katika sahiyh yake
 


ويقول  (( إذا صلى أحدُكم إلى سترة ؛ فلْيَدْنُ منها ، لا يقطع الشيطان عليه صلاتَه)) أبو داود والبزار و الحاكم و صححه ووافقه الذهبي والنوووي

Alikuwa akisema: ((Mmoja wenu akiswali kuelekea Sutrah, basi awe karibu nayo, ili shaytwaani asiweze kuikata Swalah yake)) [Abu Daawuud, Al-Bazzaar (ukurasa 54 Zawaaid) na Al-Haakim ambaye amekiri kuwa ni Sahiyh na Adh-Dhahabiy na An-Nawawy wameipitisha]

و كان   أحيانا  يتحرى الصلاة عند الإسطوانة التي في مسجده  ( البخاري)

Mara nyingine "Alikuwa anifanya nguzo iliyopo katika msikiti wake kuwa ni kizuizi wakati akiswali'' [Al-Bukhaariy]

Vile vile amekataza mtu asipite mbele ya mwenye kuswali kwani kufanya hivyo ni uovu na Swalah hukatika.

 َعنْ أَبِي جُهَيْمِ بْنِ الْحَارِثِ بْنِ الصِّمَّةِ الأَنْصَارِيِّ رضي الله عنهما قَالَ : قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم : لَوْ يَعْلَمُ الْمَارُّ بَيْنَ يَدَيْ الْمُصَلِّي مَاذَا عَلَيْهِ مِنْ الإِثْمِ ، لَكَانَ أَنْ يَقِفَ أَرْبَعِينَ ، خَيْراً لَهُ مِنْ أَنْ يَمُرَّ بَيْنَ يَدَيْهِ)) البخاري ومسلم

((Kutoka kwa Abu Juhaym bin Al-Haarith bin As-Swummatil-Answaariy (Radhiya Allahu 'anhumaa) ambaye alisema: Kasema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):   ((Angelijua mtu  dhambi za kupita mbele ya mwenye kuswali  basi kusubiri kwake (asipite) arubaini ni kheri kwake kuliko kupita mbele yake)) Kasema Abu-Nassr: sijui kakusudia ni siku arubaini au ni miezi au ni miaka.  [Al-Bukhari na Muslim]

Na pia Swalah hukatika na inapaswa kurejewa ikiwa atapita mbele ya mwenye kuswali mwanamke au punda au mbwa mweusi

عن أبي ذر رضي الله عنه: عن النَّبيِّ صلى الله عليه وسلم قال: تُعادُ الصَّلاَةُ مِنْ مَمَرِّ الحِمَارِ، وَالمرْأةِ، وَالكَلْبِ الأسْوَدِ))  رواه ابن خزيمة في صحيحه

Imetoka kwa Abi Dharr (Radhiya Allahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema:  ((Swalah irudiwe atakapopita mbele punda, na mwanamke, na mbwa mweusi)) [Imepokelewa na Ibn Khuzaiymah katika Sahihi yake]

 Kwa muhtasari ni kuwa mwenye kuswali lau mtu atapita mbele ukiondosha hao waliotajwa katika hadiyth iliyotangulia, Swalah yake haivunjiki lakini itakuwa ni madhambi kwa mwenye kupita kwani atakuwa anafanya kitendo ambacho ni cha kishetani.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share