Skip navigation.
Home kabah

Kufuru Na Aina Zake

 

 

 

(Na Imaam Ibnul-Qayyim)

Imefasiriwa Na Shu’ayb Kifea

 

Dhambi mbaya na yenye hasara kubwa kabisa kuliko dhambi zote ambazo mtu anaweza kumtendeya MwenyeziMungu ni kufuru ambayo ina maana ya ukadhibishaji, ukosefu wa shukurani na ufichaji wa ukweli. Kwa istilahi ya Uislamu, ina maana ya kuukataa ujumbe wa MwenyeziMungu.

         

Zipo kufuru za aina mbili. Mosi,  Kufuru kubwa ambayo inasababisha mtu kuingiya Jahanamu milele. Kufuru hii piya inamfanya mtu atengwe na Umma wa Kiislamu katika maisha haya. Pili, Kufuru ndogo ambayo ina maana ya uwasi katika matendo ya mtu.

Hii nayo yaweza kumpelekeya mtu kuingiya motoni lakini si kwa ukaazi wa milele na wala haihitaji hatuwa yoyote kwa upande wa Umma wa Waislamu.

Katika kufafanuwa tofauti kati ya kufuru hizi mbili, kubwa na ndogo, kuna aya ya 44 ya Sura ya tano ya Qur’an ambayo inabainisha kuwa wale wote wasiohukumu kwa shariya ya MwenyeziMungu ni makafiri.

 Tofauti kati ya aina hizi mbili za kufuru inabainishwa na ufafanuzi uliotolewa na Ibn Abbas na maswahaba kwa ujumla juu ya aya hiyo. Ibn Abbas kasema;

Hii siyo kufru inayomuondoleya mtu utambulisho wake wa kijamii kama Muislamu bali mtu anayefanya kitendo hicho anafanya kufru juu yake Mwenyewe na hayuko Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallama na yule anayemkadhibisha MwenyeziMungu na Siku ya Mwisho.

 Al-Baghawi anasema; Kemeo hili la Allaah linahusiyana na ukataaji wa makusudi wa hukumu ya wazi ya Allaah na si kwa hukumu ambayo pengine mtu haijuwi.

Kwa maneno mengine, kama mtu aijuwa vema hukumu sahihi ya Allaah lakini bado akaamuwa kuhukumu kwa hukumu nyingine huyo ndiye anayehusishwa na kemeo hilo.

Rai sahihi ni kwamba kuhukumu kwa hukumu isiyotokana na kitabu cha  MwenyeziMungu inaweza kuangukiya katika kufuru yoyote kati ya kufru hizi mbili kutegemeyana na na aina ya hukumu na mazingira yake.

Hivyo, kama mtu anaujuwa wajibu wa kuhukumu kwa Kitabu cha Allaah lakini anashindwa kufanya hivyo kwa sababu ya kughafilika, hiyo ni kufru ndogo.

Lakini kama mtu anaamini kuwa si wajibu kumtii Allaah katika kuhukumu jambo lolote ambalo Hukumu Yake iko wazi na kwamba yeye anayo haki ya kuhukumu kinyume na Kitabu cha Allaah, basi hiyo ni kufru kubwa.

 

Kufru kubwa

Kufru kubwa ambayo hupelekeya mtu kutengwa kabisa na jamii ya Waislamu na kuadhibiwa motoni milele, ina sehemu tano;

  1. Kufru ya kukanusha kwa sababu ya kutoamini
  2. Kufru inayotokana na kibri na ukaidi wa kutii hata kama mtu anaukubali Ukweli.
  3. Kufuru ya kufanya hila ya kukwepa Haki
  4. Kufru inayotokana na shaka na
  5. Kufru inayotokana na unafiki.

 

Kufru inayotokana na kukosa imani

Aina hii ya kufru ina maana ya kuamini kuwa Mitume wa MwenyeziMungu wamedanganya  na kwamba MwenyeziMungu hakushusha wahai wahai wowote kumuwongoza mwanadamu.

 

Kufru inayotokana na kibri na ukaidi wa kutii

Mfano wa kufru hii ni ile ya Ibilisi ambaye hakukanusha kuwepo kwa Allaah, wala hakuyakana mamlaka yake bali yeye alikataa kumtii MwenyeziMungu kwa kiburi tu. Vivyo hivyo mtu aliyekubali kuwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni mkweli na kwamba ameleta Haki kutoka kwa Allaah lakini bado asimfuwate.

Aina hii ya kufru ndiyo inayoonekana sana amabapo watu hutakabari na kuwapinga Mitume wa Allaah. Firauni alimpinga Musa si kwa sababu hawakumuamini bali kwa majivuno tu;

"Kisha Tulimtuma Musa na nduguye Harun pamoja na miujiza yetu na dalili zilizo dhahiri kwa Firauni na watu wake wakubwa. Lakini walijivuna, nao walikuwa watu jeuri. Na walisema: “O! Tutawamini watu walio mfano wetu na ambao jamaa zao ni watumwa wetu." (23:47).

Jamii nyingine zikawaambiya hivyo hivyo Mitume wao,

“Hamkuwa nyinyi ila ni watu kama sisi.” (14:10).

“Kina Thamudi walikadhibisha kwa sababu ya upotevu wao” (91:11)

Wayahudi wa Madina nao walimkadhibisha Mtume huku wakiujuwa fika ukweli wake. “Na kilipowafikiya Kitabu kitokacho kwa MwenyeziMungu kisadikishacho yaliyopamoja nao (walikadhibisha) na zamani walikuwa wakiwafunguliya makafiri (habari za Mtume huyo) lakini yalipowafikiya yale waliyokuwa wakiyajuwa, waliyakataa.Basi laana ya MwenyeziMungu iko juu ya makafiri. (2:89)

Kufru ya Ami yake Mtume Abu Talib nayo ilikuwa ya aina hii kwani aliujuwa ukweli na hakuutiliya shaka ujumbe wa Mtume lakini bado hakutamka shahada.

 

Kufuru ya kuukwepa ukweli

Hii ni aina ya kufru ambapo mtu hujitahidi kuuepusha moyo wake kuusikiya Ukweli uliomshukiya Mtume wa Mwisho. Mtu wa namna, katika kuishi kwake hujaribu kuzuwiya moyo na akili yake visiundee ukweli. Haupingi wala hauungi mkono Uislamu.

 

Kufru ya shaka

Hii ni aina ya kufru itokanayo na shaka katika moyo wa mtu juu ya ujumbe ambao MwenyeziMungu au kutiya shaka kama kweli Muhammad ni Mtume wa MwenyeziMungu.

 

Kufru ya unafiki

Kufuru hii ina maana ya kutamka imani juu ya Allaah na Mtume wake kwa ulimi tu lakini moyoni imani haipo.