Utaratibu Sahihi Wa Kufanya Ruqya - 3 - Tiba Enzi Za Ujahili Na Aina Mbili Za Ruqya
(Na Fathi Al-Jundii)
Imefasiriwa na Ummu Ashraf
Tiba Enzi Za Ujahili:
Yafahamika kuwa watu katika zama za ujahiliya walikuwa wakitamka maneno mengi ya uganga katika mazingira mbalimbali.
Jabir kasimulia kuwa Mtume (Salallahu alaihi wasalam) aliharamisha uganga wa kienyeji. Ndipo familia ya Amr ibn Hazm ikaja kwa Mtume wa Allah na kusema: “Sisi tunayajua maneno ambayo tunayatumia kuponeshea maumivu ya kung’atwa na n’nge, lakini wewe umeyakataza.” Wakatamka maneno hayo ya tiba mbele yake, naye akasema, “sioni ubaya wowote wa jambo hili. Yeyote kati yenu anayeweza kumsaidia nduguye afanye hivyo.” (Muslim).
Auf ibn Malik Al-shja’ii naye kasimulia hivi: “Tulifanya tiba katika zama za ujahili na tukasema, “Ewe Mtume wa Allah! Nini rai yako kuhusu jambo hili?” Akasema, ‘hebu nifahamisheni tiba yenu’ Na kisha akasema, ‘hapana ubaya katika tiba ambayo haihusishi shirki’” (ushirikina). (Muslim).
Mtume (Salallahu alaihi wasalam) hakuzikataa Aina za tiba zilizokwishakuwepo katika zama za ujahili wala hakuwaamuru Masahaba wake kuacha kuzitumia. Badala yake upo ushahidi wa kutosha wa Hadith unaoonesha kuwa aliwaruhusu Waislamu kuchambua aina mbalimbali za tiba zilizokuwepo na kisha kuzikubali zile zisizohusisha mambo ya ushirikina au mambo yaliyoharamishwa ambayo yanaweza kusababisha jambo jingine la haramu.
Ruqya na Dua:
Ruqya ni sawa tu na dua. Wakati ambapo inapendelewa kutumia dua alizotufundisha Mtume (Salallahu alaihi wasalam), Wanazuoni wa Kiislamu wanakubaliana kuwa pia inajuzu kutumia dua ambazo hakutufundisha.
Sharti la kufanya hivyo ni kuwa dua hizo zisiwe na maneno ya haramu na wala zenyewe zisiwe dua za haramu au zinazokusudia jambo la haramu kama ilivyobainishwa na Hadith za Mtume (Salallahu alaihi wasalam). Anas kasimulia, “Mtu mmoja alikuja huku akihema na akaingia katika safu ya waumini na kusema, ‘Sifa njema ni za Allah, Ahimidiwe na atukuzwe kwa wingi.’ Mtume (Salallahu alaihi wasalam) alipomaliza Swala akauliza, ‘ni nani miongoni mwenu aliyetamka maneno haya?’ Watu wakanyamaza kimya. Mtume (Salallahu alaihi wasalam) akauliza tena, ‘nani kati yenu aliyetamka maneno haya?’ Mtu huyo akasema, ‘hakuna ubaya’. Halafu akasema, ‘nilikuja huku nikiwa na tatizo la kupumua, kwa hiyo nikatamka maneno hayo.’ Mtume (Salallahu alaihi wasalam) akajibu, ‘niliona Malaika kumi na wawili wakiangaliana kuwa nani kati yao ayachukue maneno hayo kuyapeleka kwa MwenyeziMungu.’ (Muslim)
Ule ukweli kuwa jamaa aliyetamka maneno hayo alinyamaza pale Mtume alipouliza swali mara ya kwanza, unaonesha kuwa alidhani kafanya kosa katika dua yake na akachelea kuwa huenda Mtume (Salallahu alaihi wasalam) asingeyaridhia yale aliyoyasema. Kwa hakika maneno haya ya mtu huyo yakaja kuwa mfano wa dua zinazokubalika ambazo zinampendeza Allah Taala.
Ingawaje inajuzu kuomba dua za aina hii ambazo hazikutoka kwa Mtume (Salallahu alaihi wasalam), lakini kama ilivyoelezwa, zisiwe na maneno ya haramu, zisisababishe jambo la haramu, kama vile kuacha kabisa dua ambazo zimetoka kwa Mtume (Salallahu alaihi wasalam). Ni bora zaidi kufuatisha dua alizotufundisha Mtume (Salallahu alaihi wasalam)]. Itazame Hadith hii ambayo inalibainisha jambo hili barabara.
Abu Huraira kasimulia kuwa Bedui mmoja aliingia msikitini wakati Mtume (Salallahu alaihi wasalam) alipokuwa amekaa. Kisha Bedui huyo akaswali rakaa mbili za Sala na kusema, ‘Ewe MwenyeziMungu, Mrehemu Muhammad na Unirehemu mimi na Usimrehemu mwingine yeyote pamoja nasi’. Mtume (Salallahu alaihi wasalam ) akasema, “umelifinya jambo hilo (yaani umezifinya Rehema za Allah) ambazo ni pana (nyingi) zaidi. (Ahmad na Abu Dawud).
Aina Mbili Za Ruqya:
1. Ruqya halali: Hii ni aina ya Ruqya aliyoitumia Mtume (Salallahu alaihi wasalam). Ruqya hii inajumuisha yafuatayo; kuomba dua zinazojuzu na kupuliza mikono na kuiparazia (kuipitisha) katika sehemu ya mwili iliyodhurika kama ilivyobainishwa na aya za Qur’an na Hadith Sahihi lakini pasina kutia nyongeza yoyote na bila kufanya jambo hilo kiajabu-ajabu (kiuganga-uganga).
2. Ruqya haramu: Hii ni Ruqya inayojumuisha maneno ya kishirikina, mauzauza (mayakayaka), au jambo lolote lilliloharamishwa katika Uislamu.
Ruqya halali:
Ibn Hajar kasema, “Wanachuoni wa Kiislamu wanaafikiana kuwa Ruqya ni halali maadam itimize masharti matatu:
Mosi, yatumike maneno ya MwenyeziMungu (yaani Qur’an) ikiwa ni pamoja na Majina au Sifa Zake.
Pili, Ruqya ifanywe kwa Kiarabu kinachoeleweka au hata kwa maneno ya lugha nyingine yanayoeleweka.
Tatu, wale wanaofanya ruqya lazima wawe waumini wenye yakini kuwa si ponyo linayoponya bali Allah (SW) ndiye anayesababisha ponyo kuponya. (Taz. Fath Al-Barii).
Na kuhusu dua au maombi, nayo ni halali maadam tu yasikiuke au kupingana na mafundisho ya Uislamu wala yasipelekee katika shirki. Kama ni kufanya Ruqya kwa dua ambazo hakufundisha Mtume (Salallahu alaihi wasalam), basi pasiwe na maneno ya ajabu-ajabu, wala isifanyike kiuganga-uganga kama wafanyavyo wanamazingaombwe au waganga wa kienyeji.
Ruqya ya maneno yasiyoeleweka, (maneno ya kupandisha mzuka) haifai kwani inaleta mambo ya bidaa na inaweza kuhalalisha kazi ya waganga matapeli wa kienyeji. Kwa sababu hizi, kuelewa maana ya Ruqya ni sharti la lazima katika kuitumia. Ikiwa ni hatua ya tahadhari, Ruqya ya maneno yasiyoeleweka imeharamishwa.
Ibn Qudama kasema, “Imam Ahmad alifahamishwa na mtu mmoja kuhusu mtu mmoja aliyedai kupoza uchawi kwa kuweka maji kwenye chungu na kusema maneno yasiyoeleweka pamoja na mambo mengine. Ndipo Imam Ahmad, kwa kutoliridhia jambo hili, akamshika mkono mtu huyo na kusema, “mimi silijui jambo hili (la kipuuzi)” (Al-Kafii).
Al-Bajii kasema, “Imam Malik aliona kuwa kutumia kifimbo cha chuma na chumvi wakati wa kufanya Ruqya ni jambo la kuchukiza (makruhu) na kutumia vifundo na nyuzi ni jambo la kuchukiza zaidi.” (AlMuntaqa, Sharh Al-Muwatta).
Wanazuoni wengine wamekataa matumizi ya hirizi na visu na mambo mambo mengine kama vile kuuchanja chale mwili wa mgonjwa, hayo ni mambo yaliyoigwa kwa wachawi.
Muislamu lazima awe makini mno juu ya mambo haya na mara zote arejee katika Qur’an na Sunna pale anapokutana na jambo geni ili aone kama jambo hilo ni halali kabla hajalifanya.
Mambo tata ambayo hayana ushahidi wa Qur’an na Sunna yakataliwe, la sivyo yanaweza kuwapelekea baadhi ya watu kuingia katika uchawi na uganga mbali ya kuwachanganya wale wasio na elimu ya kutosha.
Kuhusiana na uchawi MwenyeziMungu anasema,
“Wakafuata yale waliyoyafuata mashetani katika ufalme wa Suleiman; na Suleiman hakukufuru bali mashetani ndio waliokufuru, wakiwafundisha watu uchawi ulioteremshwa kwa Malaika wawili, Haruta na Maruta katika (mji wa) Babil. Wala (Malaika hao) hawakumfundisha yoyote mpaka wamwambie: “Hakika sisi ni mtihani basi msikufuru.” Wakajifunza kwao ambayo kwa mambo hayo walimfarakanisha mtu na mkewe. Wala hawakuwa wenye kumdhuru yeyote kwa hayo ila kwa idhini ya MwenyeziMungu. Na wanajifunza ambayo yatawadhuru wala hayatawafaa. Na kwa yakini wanajuwa kwamba aliyekhiyari haya hatakuwa na sehemu yoyote Akhera. Na bila shaka ni kibaya kabisa walichouzia nafsi zao laiti wangelijua (2:102).
Kuhusiana na aya hii, ibn Taimiyya anasema, “Wale (wanaofanya uchawi) wanajuwa fika kuwa hautakuwa na manufaa Akhera na kwamba wale wanaoufanya watakuwa miongoni mwa watakaopata hasara, lakini bado wanavutwa na maslahi yake katika dunia hii.” (Iqtidhaa’ Assirat Al-Mustaqiim).
Ar-Rabii naye kasema, ‘nilimuuliza Imam Shafii kuhusu Ruqya naye akasema, “Hakuna ubaya kufanya ruqya kwa kusoma Kitabu cha MwenyeziMungu na (kwa kutumia) aina zozote za dua anazozijua mtu...’ (Irshad As-Sarii).
Kwa hiyo mtu ajiepushe na utatanishi na badala yake aende kwenye msingi wa Ruqya, ili kujua rukia ni nini hasa. Kwamba Ruqya ni njia ya kumuomba Allah (SW) kwa utaratibu sahihi wenye ikhilasi na Imani thabiti kwa Allah.
Inaendelea …./4
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


